Thursday, September 8, 2016

BINTI ANAYEANDIKA KWA KUTUMIA ULIMI WAKONTA KAPUNDA APATA VIFAA.

Wakonta Kapunda

Unamkumbuka Wakonta Kapunda? Binti mtanzania mwandishi wa miswada ya filamu anayeandika kwa kutumia ulimi?

Wakonta alipata ajali siku ya mahafali yake ya kidato cha sita miaka minne iliyopita. Ajali hiyo ilimuacha akiwa amepooza kuanzia shingoni na kushuka chini na kumfanya kutoweza kutumia mikono yake kuandika.

Wiki kadhaa zilizopita, BBC iliporusha habari yake msamaria mwema mmoja aliguswa na kumsaidia.

Kupitia kipindi cha Televisheni Focus on Africa katika BBC World Service mwanadada Olivia Soko kutoka Afrika ya Kusini aliguswa kufanya kitu kumsaidia Wakonta.

Akiwa mkurugenzi wa kampuni ya WhirlMarket  Technologies, Olivia alijitolea kutoa msaada wa programu ya kompyuta iitwayo Nuance Dragon Naturally Speaking.

Jinsi programu hii inavyofanya kazi ni kwamba mtumiaji yeye anazungumza anachotaka kukiandika kupitia kipaza sauti chake halafu programu hiyo inaandika yenyewe katika kompyuta ya mtumiaji.

Wakonta alijaribu kuitumia jana akaifurahia, lakini bila shaka atahitaji muda zaidi ili aizoee vizuri.


No comments: