Thursday, September 8, 2016

MGANGA ACHOMWA MOTO BAADA YA KUMUUA MJUKUU WAKE.

Wananchi katika kijiji cha Kalundi Wilayani Nkasi Mkoani Rukwa wanadaiwa kumuua kisha kumteketeza kwa moto mganga wa kienyeji, Patrick Mwandaliwa (44) wakimtuhumu kumuua mjukuu wake, Silvia Mwanakatwe mwenye umri wa mwaka mmoja na nusu.

Kamanda wa polisi mkoa wa Rukwa, George Kyando alisema tukio hilo lilitokea Septemba 4, saa mbili usiku, kijijini Kalundi wilayani Nkasi mkoano humo.

Akisimulia mkasa huo kamanda Nkasi alidai usiku wa tukio Mwandaliwa alikutana na mpwa wake Maria Kapele (21) dukani kijijini humo akiwa amembeba mtoto wake wa kike mwenye umri wa mwaka mmoja na nusu.

Mwandaliwa alimuomba mpwa wake huyo mjukuu wake huyo kisha akaondoka naye mpaka nyumbani kwake, mpwa wake hakuwa na wasiwasi wowote kwakuwa aliyemchukua mwanae ni mjomba ake.

Maria alihisi ni mda mrefu umepita tangu mjomba ake amchukue mtoto wake ndipo alipomtuma mtoto wa jirani yake kwenda kumchukua, lakini alipofika kwa Mwandaliwa alikuta mlango umefungwa akarudi na kumtaarifu mama wa mtoto.

Inadaiwa kuwa mama mtoto alipofika kwa mjomba ake ampe mtoto, alikana na kusema yeye hana mtoto wake. Ndipo Mwandaliwa alipomsukuma mpwa wake na kuingia ndani na kufunga mlango.

Mwandaliwa alipanga magunia ya mahindi mlangoni akizuia mtu yoyote yule asiweze kufungua mlango, ndipo mama mtoto alipopiga mayowe kuomba msaada kwa watu.

Watu walikusanyika katika eneo hilo la tukio, kwa kuwa walikuwa wengi waliweza kuvunja mlango na kuingia ndani na kumkuta Mwandaliwa akiwa ameshika ndoo ya plastiki mkononi akiwa na mwili wa mtoto, tayari akiwa amekufa, akiwa amemtoboa shingoni kwa kitu cha ncha Kali.

Ndipo wananchi wakiwa na silaha za jadi walimvamia Mwandaliwa na kumpiga sana kisha kumchoma.

Mwili wa Mwandaliwa ulizikwa chini ya uangalizi wa askari kwa sababu wananchi waligoma kumzika.


No comments: