Sunday, September 4, 2016

MJANE AUAWA KWA KUNYOFOLEWA VIUNGO.

Mjane mwenye umri wa miaka 46, Veronica Dala ameuawa na watu wasiofahamika kwa kukatwa na mapanga mwilini. Aidha mjane huyo amenyofolewa baadhi ya viungo vya mwili wake.

Tukio hilo limetokea asubuhi ya Septemba mosi mwaka huu katika kijiji cha Ilagaja kata ya Mangoye wilayani Nzega Mkoa wa Tabora baada ya wahalifu hao kuvamia nyumba ya mjane huyo kisha kuanza kumshambulia kwa mapanga.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti majirani na ndugu wa mjane huyo walisema walipata taarifa ya kuwa ameuawa na watu wasiojulikana asubuhi ya tukio hilo.

Luhaga Jilala ambaye ni ndugu wa mjane huyo, alisema taarifa hizo alizipata asubuhi kuwa ndugu yake ameuawa. Hata hivyo chanzo cha mauaji hayo bado hakijajulikana.

Mwenyekiti wa kijiji hicho Juma Seleli alisema tukio hilo ni la pili kutokea miaka kadhaa iliyopita alivamiwa na waharifu na kumjeruhi vibaya.

Alisema kijiji hicho kimejipanga kuhakikisha wanafanya doria za mara kwa mara ili kuhakikisha wanaimarisha ulinzi wa kijiji na wananchi wake.

Diwani wa kata hiyo, Henerico Kanoga alisema atahakikisha wananchi wanafanya uchunguzi kwa kupiga kura za maoni ili kuwapata watu wanaoshiriki kufanya uharifu huo wa kikatili.

Mwenyekiti wa ulinzi na usalama, Mkuu wa Wilaya ya Nzega, Godfrey Ngupulla alisema serikali ya Wilaya imepanga mipango ya mkakati wa kuhakikisha wananchi wanatoa ushirikiano wa kutosha ili kutokomeza mauaji.

Alisema Wilaya ina mpango wa kuanza kupiga kura za maoni kwa wananchi ili kubaini wote wanaoshirikiana na waharifu hao na kuongeza kuwa mwananchi atakayetoa taarifa dhidi ya waharifu hao, siri zote zitatunzwa ili kulinda usalama wake.

Polisi mkoani Tabora imekiri mauaji hayo na kuahidi kufanya msako mkali kwa ajili ya kuwakamata na inawashikiria watu wawili kwa ajiri ya mahojiano.


No comments: