Thursday, October 27, 2016

JACOB ZUMA ASINZIA BUNGENI.

Macho ya wengi nchini Afrika Kusini jana yalikuwa kwenye Waziri wa Fedha Pravin Gordhan ambaye alikuwa akihutubu bungeni.

Uchumi wa Afrika Kusini umekuwa ukikabiliwa na matatizo na kumekuwa na maswali mengi kuhusu ufadhili wa elimu.

Wanafunzi katika vyuo vikuu vingi wamekuwa wakiandamana na kuzua vurugu kulalamikia viwango vya karo.

Bw Gordhan mwenyewe amejipata kwenye mzozo wa kisiasa na hivyo basi taarifa yake ya bajeti ya muda ilisubiriwa kwa hamu na ghamu.

Lakini asubuhi hii, habari zimeanza kuenea mtandaoni kwamba Rais Jacob Zuma huenda alisinzia (au kupumzisha macho kama wasemavyo Kenya) wakati wa hotuba ndefu ya waziri huyo.

Tovuti ya habari ya Times Live imesema alikuwa anasinzia.

Baadhi wamejaribu kutoa ufafanuzi, kwa njia ya ucheshi kuhusu alichokuwa akifanya rais huyo.

Tovuti ya habari ya Rand Daily Mail imeeleza mambo matano ambayo huenda yalikuwa yakitokea, na ambayo huenda Rais Zuma akatumia kujieleza:

Nilikuwa naangalia ujumbe kwenye TwitterSikio langu lilikuwa na mwasho kidogo, nilikuwa najikuna kwa kutumia begaNilikuwa najaribu kusikia kiranja wa ANC bungeni Jackson Mthembu alikuwa anasema nini nyuma yanguHuwa nakuwa makini zaidi nikiwa nimefunga macho.Kulala ni hali mbadala ya kuwa macho

Afisi ya Rais Zuma bado haijazungumzia habari hizo.

Kiongozi huyo si wa kwanza Afrika kupatikana hadharani akiwa amefunga macho.

Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe, ambaye ameongoza tangu 1980, amepatikana mara kadha.

Aprili mwaka huu, alionekana kana kwamba anasinzia wakati wa kikao cha wanahabari alipokuwa na Waziri Mkuu wa Japan Shinzo Abe:

Septemba 2012, alipigwa picha akiwa amesinzia katika mkutano wa viongozi wa nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa jijini New York.

Mwaka 2014, runinga ya NTV nchini Uganda iliashiria kwamba huenda Rais Yoweri Museveni, ambaye ameongoza tangu 1986, alisinzia bungeni.

Kituo hicho cha runinga kilisema alikuwa amefunga macho.

Msemaji wa serikali alisema kiongozi huyo alikuwa anatafakari wakati huo. Kituo cha NTV kilipigwa marufuku kuripoti kuhusu hafla za rais kwa muda.


No comments: