Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam imesema Mkurugenzi wa Kampuni ya Group Six International, raia wa China, Jensen Hung (39) ametapeliwa zaidi ya Sh milioni 22 na mtu aliyejiita Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda.
Wakazi wa jijini humo na wageni wametahadharishwa kuwa makini.
Kwa mujibu wa Polisi, kumeibuka wimbi la wahalifu wanaotumia mbinu hususan majina ya viongozi wa serikali au watu mashuhuri na kujipatia fedha kwa njia ya kitapeli kinyume cha sheria za nchi.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kamanda wa Kanda hiyo, Kamishna wa Polisi, Simon Sirro alisema matapeli hao wamekuwa wakitumia zaidi majina ya viongozi haswa jina la Mkuu huyo wa Mkoa kwa lengo la kujipatia fedha.
“Hivi karibuni kumekuwa na malalamiko mbalimbali kutoka kwa raia wa kigeni kwamba kuna baadhi ya wahalifu wanaotumia vibaya jina la Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kuwa watoe kiasi cha fedha za kigeni na fedha za kitanzania kwa madai ya kuwasaidia wanafunzi kupata vyuo huko nchi za nje kama Ufilipino,” alisema Kamanda Sirro.
Alisema katika tukio la kwanza lilitokea Oktoba mosi, raia wa China, Marco Li (24) ambaye ni mfanyakazi wa Kampuni ya Group Six International mkazi wa Mikocheni B alipigiwa simu na mtu asiyefahamika kwa namba 0719340914 akijitambulisha kuwa yeye ni Makonda akimtaka atoe kiasi cha Dola za Marekani 3,500.
Alisema fedha hizo alidai kwamba ni kwa ajili ya msaada wa kusomesha mwanafunzi, aliyechaguliwa Chuo Kikuu cha Manila kilichopo nchini Ufilipino, ambapo Mkurugenzi wa Kampuni hiyo, Jensen Hung (39) pia mkazi wa Mikocheni B alikubali ombi hilo na kumtuma msaidizi wake aende kwa Makonda kwa ajili ya kujiridhisha.
"Alipofika kwenye ofisi ya Mkuu wa Mkoa hakuweza kuonana naye badala yake alipiga simu kwa namba tajwa hapo juu, ambapo mkuu wa mkoa feki alipokea simu na kumweleza kuwa yeye ana shughuli nyingi hivyo Oktoba 4, Marco Li alituma Sh 7, 595,000 kupitia benki,” alieleza Kamanda Sirro.
Alisema Oktoba 6, Jensen alitumia fursa hiyo kumuomba mkuu huyo wa mkoa bandia kwamba amsaidie kuongezwa muda wake wa kuishi nchini ambao ulikuwa umeisha na ndipo mtuhumiwa huyo akamtaka atoe kiasi Dola za Marekani 7,000 ambapo mlalamikaji alitoa kiasi cha Sh 15,260,000 kupitia akaunti ya Benki ya ECO.
Alisema Oktoba 25, mwaka huu mkuu huyo wa mkoa feki alimpigia simu mkurugenzi wa kampuni hiyo akimweleza kwamba suala lake la Uhamiaji limekamilika hivyo atoe Dola za Marekani 5,000 na ndipo walipogundua wametapeliwa baada ya kupiga simu kituo cha Polisi kuhakiki namba ya simu inayotumika kama ni ya Makonda na kujibiwa kuwa hiyo si namba yake.
Sirro alisema Agosti mosi mtu huyo alijaribu kumtapeli Kelvin Stander (54) raia wa Afrika Kusini akitumia namba 0719 340914, akijitambulisha kwamba ni Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda akiomba msaada wa Dola za Marekani 1,500 kama mchango wa kumpeleka mwanafunzi masomoni Chuo Kikuu cha Manila kilichopo Ufilipino.
Alisema tapeli huyo alitaka fedha hizo zitumwe kupitia akaunti namba 002345401590701 ya ECO benki ya Nairobi ikiwa na 'swift code' ECOTZTZ ,ndipo mlalamikaji akagundua haikuwa sahihi na kupiga simu iliyopo kwenye nyaraka iliyotumwa.
Alisema baada ya kupiga kupitia namba ya simu +25-257 56 04 iliyopo Ubalozi wa Ufilipino Nairobi na baada ya ufuatiliaji, waligundua kuwa taarifa zilizopo kwenye hati hiyo siyo sahihi.
“Agosti 4, mwaka huu mtuhumiwa alipigiwa simu na mlalamikaji kuwa taarifa zilizopo kwenye hati siyo sahihi lakini mtuhumiwa alisisitiza kwamba taarifa zipo sahihi na wao watume dola 1,500 na atatangaza kwenye vyombo vya habari siku itakayofuata kuwasifia kwa msaada waliojitolea,” alisema.
Aidha, alisema baada ya mlalamikaji kuwa na mashaka na watu hao, alipiga simu Polisi Kanda Maalumu na kuelezwa kwamba namba hiyo ya simu siyo ya mkuu wa mkoa halisi ndipo alipojiridhisha mtu huyo ni mdanganyifu.
“Wakazi wote wa Dar es Salaam wanapaswa kuwa makini na matapeli hao na wakiona dalili kama hizo wapige simu Polisi kwa msaada zaidi ili sheria ichukue mkondo wake,” alieleza Kamanda Sirro.
Tuesday, November 1, 2016
MCHINA ATAPELIWA MIL.22 NA KIJANA ALIYEJITAMBULISHA KWA JINA LA RC MAKONDA.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment