Timu ya Kabaddi ya wanaume na wanawake ya Tanzania itashiriki Kombe la Dunia la mchezo huo nchini India katika jimbo la Punjab kuanzia keshokutwa hadi Novemba 17 mwaka huu.
Balozi wa India nchini, Sandeep Arya alisema hayo jana jijini Dar es Salaam na kuongeza kuwa watakaoenda nchini India kushiriki Kombe la Kabaddi kutoka Tanzania ni jumla ya watu 34.
Alisema Kabaddi ni mchezo maarufu katika jimbo la Punjab na mikoa mingine ya India na kombe hilo litafanyika katika sehemu tofauti 14 katika jimbo hilo.
Alisema timu 13 zinatoka katika sehemu mbalimbali duniani zitashiriki na kwa upande wa wanaume zinatoka Marekani, Uingereza, Hispania, Dernmark, Iran, Argentina, Canada. Kenya, Sweden, Australia, Tanzania, Sierra Leone na India.
Alisema timu 10 zitashiriki kwa upande wa wanawake ambazo ni Marekani, Uingereza, Dernmark, New Zealand, Mexico, Kenya, Sierra Leone, Australia, Tanzania na India.
Arya alisema Serikali ya India inafurahia kwa timu za Tanzania kushiriki katika sehemu zote mbili yaani timu ya wanawake na wanaume.
Alisema safari na maandalizi ya timu ya Kabaddi yamewezeshwa na kudhaminiwa na Serikali ya Jimbo la Punjab nchini India na kwamba kwa wiki mbili timu hiyo imekuwa ikifundishwa na kufanya mazoezi yake katika kituo cha utamaduni wa India kwa ajili ya maandalizi ya kombe hilo la dunia.
Katibu Mkuu wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Mohamed Kiganja alisema timu hiyo itaondoka keshokutwa na kuwataka wachezaji kwenda kuiwakilisha vyema Tanzania kwani fursa waliyoipata ni nafasi ya pekee.
Kaimu Mkurugenzi wa Michezo, Alex Kenyenge alisema michezo hiyo ni ya jadi kwa India na kutoa viongozi mbalimbali nchini kuona ni jinsi gani ya kutumia michezo ya jadi iliyopo nchini kwa ajili ya kuitangaza Tanzania katika nyanja mbalimbali.
Kiongozi wa timu ya Tanzania, Abdallah Mustafa alisema timu hiyo ilianza mazoezi na baadaye kuletewa makocha kutoka nchini India na kuahidi kuiwakilisha vyema Tanzania na kuleta ushindi.
No comments:
Post a Comment