KATIKA dunia ya soka inafahamika kazi ya kocha ni kuajiriwa na kutimuliwa.
Lakini wengi wanaoondoka kwenye timu hutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kufanya vibaya, kustaafu na wengine wakisaka changamoto kwingine. Hivi karibuni kocha wa Yanga, Hans van Pluijm aliandika barua ya kujiuzulu kuifundisha timu hiyo baada ya kubaini mabosi wake walifanya mazungumzo na kocha wa Zesco ya Zambia, George Lwandamina pasipo kumshirikisha. Alikuwa akiona taarifa kwenye vyombo vya habari juu ya mabadiliko mapya kwenye benchi la ufundi, lakini hakuelezwa kinachoendelea.
Awali, taarifa hizo zilikuwa zikionesha kuvunjwa kwa benchi zima la ufundi na baadaye zikawepo taarifa kuwa Pluijm huenda akawa Mkurugenzi wa Ufundi na nafasi yake kuchukuliwa na kocha huyo wa Zesco. Mabadiliko hayo ya ghafla yalipokewa kwa mitizamo tofauti wengine wakiona ni sawa, wengine wakihuzunika na mwisho wa siku kocha huyo kipenzi cha Wanayanga anaondoka.
Pluijm kama kocha aliyeleta mafanikio makubwa kwa kipindi kifupi ndani ya timu hiyo hakupaswa kufanyiwa alivyofanyiwa, kusoma taarifa za kutemwa kwake kwenye vyombo vya habari, kwani timu hiyo imekuwa ikifanya vizuri chini yake kwa muda mrefu. Lakini Yanga ndio yenye uamuzi kwa kuwa ndiyo inayomlipa mshahara kwa hivyo pengine kuna kitu ambacho imedhamiria kukifanya katika kuboresha zaidi benchi lake la ufundi.
Au pengine kuna mambo ambayo yapo nyuma ya pazia yasiyojulikana kuhusu Pluijm ndio maana hata uongozi wa klabu hiyo umeona kuna haja ya kuachana naye kutafuta wengine ambao ni wazuri zaidi yake. Inadaiwa pia sababu ya kumuondoa kocha huyo ni timu kushindwa kufika nusu fainali ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu ambapo Yanga iliishia kwenye hatua ya makundi katika kombe la Shirikisho Afrika baada ya kuondolewa na Al Ahly kwenye Ligi ya Mabingwa.
Pluijm anaondoka lakini atakumbukwa kwa mambo mengi ndani ya Ligi Kuu soka Tanzania bara, lakini pia hata kwa vyombo vya habari kutokana na jinsi alivyoishi nao kwa muda mrefu. Kwa upande wa vyombo vya habari. Pluijm atakumbukwa kwa kuwa miongoni mwa makocha wa kigeni walioonyesha ushirikiano wa hali ya juu pindi zilipokuwa zikihitajika taarifa mbalimbali kuhusu timu au yeye mwenyewe.
Wakati wowote akitafutwa Kocha huyo iwe kwenye mitandao ya kijamii, au amepigiwa simu au amekutana na waandishi na akaulizwa maswali basi amekuwa akionesha ushirikiano katika kujibu. Tofauti na makocha wengine baadhi ambao timu zao zinapofanya vibaya hutawaona kwenye mkutano na waandishi wa habari wamekuwa na jazba ya kufungwa. Pluijm ni aina ya Kocha mwenye weledi wa hali ya juu na mwenye uvumilivu hata kama timu yake imepoteza ni lazima atajitokeza kwa vyombo vya habari kujibu maswali yao.
Mbali na ushirikiano huo kwa vyombo vya habari, atakumbukwa kwa kuleta changamoto kwenye ligi na kuifanya Yanga leo inaitwa wa kimataifa kutokana na rekodi bora aliyoiweka. Pluijm alijiunga na Yanga mwaka 2014 akimpokea Mholanzi mwenzake, Ernie Brandts aliyetimulia baada ya kushindwa kufanya vizuri mechi ya mtani jembe dhidi ya Simba. Alikwenda Al Shoalah FC ya Saudi Arabia na nafasi yake ikachukuliwa na Mbrazili, Marcio Maximo ambaye naye alifanya kazi kwa nusu msimu kabla ya Pluijm kurejeshwa Januari mwaka jana.
Anaondoka Jangwani baada ya kuiongoza Yanga katika mechi 124, akishinda 77, sare 25 na kufungwa 22. Pluijm anaondoka baada ya msimu mzuri uliopita, akibeba mataji yote matatu, Ngao ya Jamii, Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), maarufu kama Kombe la Azam Sports Federation (ASFC). Aliifikisha Yanga hatua ya makundi ya michuano ya Afrika kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1998 na mara ya pili kihistoria.
Yanga ilifika hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho mwaka huu baada ya mwaka 1998 kufika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa. Mara nyingi Yanga ilikuwa ikishiriki michuano hiyo ya kimataifa lakini iliishia kwenye hatua ya makundi. Ni dhahiri kuwa alipoifikisha timu hiyo, anaiacha ikiwa inajivunia mafanikio yake. Kutokana na mafanikio hayo, Pluijm alishinda tuzo ya kocha bora wa Ligi Kuu Tanzania Bara mwishoni mwa msimu uliopita.
Chini yake, kuna wachezaji walionekana kung’ara akiwemo Juma Abdul aliyeibuka mchezaji bora msimu uliopita, Simon Msuva msimu wa mwaka juzi alikuwa mfungaji bora, Amis Tambwe msimu uliopita alikuwa mfungaji bora, Thaban Kamusoko alikuwa mchezaji bora wa kigeni. Hiyo yote ni kwa sababu aliwaamini na kuwapa kazi chini ya mfumo wake na wakaweza kutekeleza. Mfumo wake pia ulileta changamoto kwa timu pinzani ambazo zilishindwa kutamba mbele yake.
Kocha huyo alikuwa akipenda kutumia mbinu za kushambulia na kasi ambayo iliwawezesha kupata magoli mengi katika baadhi ya mechi kadhaa na hatimaye kuchukua mataji. Pluijm hakuwa rafiki upande wa vyombo vya habari pekee, bali hata mashabiki wa klabu hiyo walionesha wazi kumkubali na ndio maana amekuwa akiwasiliana nao kwenye mtandao wa kijamii wa facebook mara kwa mara. Historia Pluijm alizaliwa miaka 67 iliyopita Uholanzi. Enzi zake alicheza soka katika nafasi ya mlinda mlango.
Aliwahi kudakia kwa miaka 28 klabu ya FC Den Bosch akicheza mechi 338 ndani ya misimu 18 na baadaye alistaafu baada ya kuumia goti. Alianza kazi ya ukocha kwenye timu hiyo na kutwaa ubingwa wa Daraja la Kwanza na kupanda Ligi Kuu ya nchini humo. Aprili mwaka 1995, alisaini mkataba wa miaka miwili na SBV Excelsior kabla ya kutimuliwa Januari 1997 na nafasi yake ikachukuliwa na msaidizi wake, John Metgod.
Hiyo ilifuatia timu hiyo ya Rotterdam kushinda mechi mbili tu na sare tatu katika mechi 17 za msimu mzima. Baada ya kufanya vibaya Ulaya, alihamia Afrika mwaka 1999, alipokwenda kufundisha Ashanti Gold SC ya Ghana. Pia, aliwahi kuifundisha Saint-George ya Ethiopia kabla ya mwaka 2010 kujiunga na B-Juniors Feyenoord ya Ghana. Mwaka 2012 alijiunga na Berekum Chelsea ambako pia alifukuzwa na kuhamia Medeama ya Ghana, nako hakudumu baada ya kufanya vibaya pia. Nenda Pluijm na kila la heri katika safari nyingine!
Saturday, October 29, 2016
PLUIJM:KWELI SHUKRANI YA PUNDA NI MATEKE.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment