Uongozi wa klabu ya Mbeya City umetoa onyo kwa Yanga kuhusu kuwasajili wachezaji wake Raphael Daud na Kenny Ally ambao bado inawahitaji.
Akizungumza na gazeti hili, Ofisa Habari wa timu hiyo, Dismas Ten alisema wanazionya timu zinazoshiriki Ligi Kuu ya Tanzania Bara, hasa Yanga kuhusu kuwasajili wachezaji wake, ambao hawajamaliza mikataba yao.
“Sisi hakuna mchezaji ambaye kamaliza mkataba, wote ni mali yetu, hivyo tunashangaa kuhusu kiungo wetu Raphael Daud na nahodha Kenny Ally kuhusishwa na kujiunga na Yanga, kiukweli hizo taarifa hatuzijui ila kama Yanga wanawataka hao wachezaji walete barua rasmi,” alisema Ten.
Ten alisema kuwa endapo timu yoyote itawasajili wachezaji hao bila ya uongozi kujua, sheria zitachukua mkondo wake, lakini pia hawawezi kumzuia mchezaji kuondoka ila wanachotaka taratibu zifuatwe.
Kiungo Daud amefunga mabao manne kwenye mzunguko wa kwanza na yupo kwenye kiwango kizuri na nahodha Ally naye ni mchezaji muhimu katika nafasi ya kiungo mkabaji. Pia Ten alisema usajili wao wa wachezaji watakaoachwa na watakaosajiliwa kwenye dirisha dogo, utatolewa rasmi Novemba 30.
Dirisha la usajili lilifunguliwa Novemba 15, ambapo timu zinazoshiriki Ligi Kuu ziko katika mawindo ya wachezaji kwa ajili ya kuimarisha vikosi vyao kwa ajili ya mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Tanzania Bara unaotarajia kuanza Desemba 17.
Wakati huo huo, mshambuliaji wa zamani wa Azam FC, Kipre Herman Tchetche amesema kwamba hajazungumza na Simba wala Yanga kuhusu mpango wa usajili.
Mchezaji huyo wa Al Suwaiq ya Oman, alikaririwa na mtandao mmoja wa kijamii akisema kuwa hajawahi kufanya mawasiliano na klabu hizo na hiyo ndio kawaida yao kuzusha mambo. Lakini Kipre Tchetche amewataka Simba na Yanga waache porojo kwenye vyombo vya habari na kama kweli wanamtaka wawasiliane naye.
No comments:
Post a Comment