Thursday, November 24, 2016

PANYA BUKU KUPIMA SAMPULI ZA UGONJWA WA KIFUA KIKUU (TB).

Mkurugenzi wa Uhakiki Ubora wa Huduma za Afya, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Mohamed Ally Mohamed (kushoto) akikata utepe kuashiria uzinduzi wa kituo cha ugunduzi wa Kifua Kikuu kwa kupitia panya buku (Apopo) kilichopo Dar es Salaam. Wengine ni Mwalimu wa panya, Ezekiel Mwakyonde (aliyemshika panya) na Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo, Dk Abdu Hayghaimo. Sherehe hizo zilifanyika jana. (Picha na Yusuf Badi).
Maabara ya kupima sampuli za ugonjwa wa kifua kikuu (TB) kwa kutumia panya buku wa Mradi wa Apopo ulio chini ya Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA), imezinduliwa jijini Dar es Salaam, huku ikielezwa kuwa panya mmoja ana uwezo wa kupima sampuli 100 ndani ya dakika 20.
Uzinduzi wa maabara hiyo ulifanywa jana na Mkurugenzi wa Uhakiki Ubora wa Huduma za Afya wa Wizara ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Mohamed Mohamed kwa niaba ya waziri wa wizara hiyo na uzinduzi ulioshuhudiwa na wadau mbalimbali pamoja na wananchi.
Akielezea mradi huo wa kupima vimelea vya kifua kikuu kwa kutumia panya waliofunzwa, Meneja Mradi, Dk Georgies Mgode alisema panya hao wana uwezo wa kubaini harufu ya vimelea vya ugonjwa huo ndani ya sekunde.
Aidha, alisema kwa dakika 20 panya anaweza kupima sampuli 100 wakati sampuli kama hizo zingepimwa kawaida kwenye maabara zinazotumia hadubini kwa siku nne, hivyo majibu hadi yafike kwa mgonjwa yanaweza kuchukua siku saba ili hali kwa kutumia panya mgonjwa ndani ya siku moja anapata majibu na kuanza tiba.
“Ni kweli hawa panya wana faida kubwa kwenye ugunduzi wa vimelea vya ugonjwa wa TB, kwa sababu wana uwezo ndani ya sekunde wakabaini maambukizi ya kwa mgonjwa wakati mtu wa maabara anatumia zaidi ya siku moja kupata majibu,” alisema Dk Mgode.
Alisema kwa kuzinduliwa kwa maabara hiyo itakayokuwa na panya buku 10 jijini Dar es Salaam ni hatua ya mafanikio ya harakati za vita dhidi ya ugonjwa huo hasa kwa kuwa jiji hilo ndilo linaongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya watu, kuliko maeneo mengine na pia ni moja la miji yenye idadi kubwa ya wagonjwa wa kikua kikuu.

No comments: