Thursday, November 24, 2016

POLISI MBARONI KWA KUMVUA NGUO MCHUNGAJI NA KUMPIGA PICHA ZA UTUPU.


Polisi wanne wametiwa mbaroni mkoani Kilimanjaro kwa tuhuma za kumvua nguo mchungaji mmoja na kumpiga picha za utupu na mtu mwingine ili wamtuhumu kwamba anafanya mapenzi ya jinsia moja.
Katika mkasa huo uliotokea ndani ya chumba cha hoteli moja wilayani Hai, polisi hao wanaidaiwa kumpiga picha na kisha kumtaka atoe Sh10 milioni ili kumaliza suala hilo. Alitoa Sh5.4 milioni na kuachiwa huru.
Ilivyokuwa
Katika tukio hilo linaloaminika kuwa lilitengenezwa na polisi hao kwa lengo la kujipatia fedha kutoka kwa mchungaji huyo ambaye jina lake na kanisa analohudumu tunalihifadhi kwa sasa, baada ya kuwakuta wawili hao ndani ya chumba, waliwaamuru wavue nguo wakiwatuhumu kufanya mapenzi ya jinsia moja na kuwapiga picha kwa kutumia simu zao.
Kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali, mchungaji huyo alilazimika kupigana na polisi hao kupinga kitendo hicho lakini alizidiwa nguvu na kuvuliwa nguo zote na kubaki na bukta tu.
Taarifa za awali zinasema, siku moja kabla ya tukio hilo, mchungaji huyo alikutana na dereva mmoja wa malori eneo la Njiapanda ya Himo ambaye alisema anafanya biashara ya pumba.
“Kwa maelezo ya mchungaji ni kuwa walipeana simu ili pumba hizo zikipatikana apigiwe. Siku iliyofuata kweli huyo mtu akampigia akisema amepata magunia 150,” mtoa habari wetu alidokeza.
Alisema mtu huyo alimtaka mchungaji afike Bomang’ombe ambako angempeleka kuziona pumba hizo ili kama akiridhika wafanye biashara.
“Yule bwana aliyejifanya ana pumba alimuomba mchungaji amsindikize ili achukue chumba kwa vile siku hiyo angelala hapo Bomang’ombe kusubiri wenzake kutoka Segera.”
Mchungaji na mtu huyo walifuatana hadi katika hoteli moja (jina tunalo) na mtu huyo anayetuhumiwa kupangwa alichukua chumba na mchungaji akaingia kukiona.
“Huyo bwana akaomba akanunue sigara ili akirudi ndiyo waende kuangalia mzigo lakini aliporudi tu, ndipo wakaingia na watu wengine kama watano au sita hivi,” alidokeza mtoa habari wetu.
Watu hao ambao baadaye wanne walibainika kuwa ni polisi, wanadaiwa kuwalazimisha mchungaji na mtu huyo kuvua nguo na kuwarekodi kwa picha wakiwatuhumu kufanya ushoga.
Inadaiwa kwamba walimchukua mchungaji na mtu huyo aliyekuwa naye, wote wakiwa nusu uchi hadi kituo cha Polisi cha Bomang’ombe.
Hata hivyo, badala ya kufungua jalada la uchunguzi, polisi hao wanadaiwa kuwahifadhi watuhumiwa upande wa nyuma ya kituo wakimtaka mchungaji awape fedha.
Inadaiwa kuwa walitaka wapewe Sh10 milioni lakini mchungaji aliwasihi kwamba alikuwa na Sh5 milioni, ambazo aliwapa lakini wakamtaka aongeze zifike Sh6 milioni.
Mchungaji huyo akiwa chini ya ulinzi kuanzia saa 10:30 jioni hadi saa tatu usiku, aliwapigia simu marafiki zake ambao baadaye walimtumia Sh400,000 kwa njia ya simu.
Kwa mujibu wa chanzo hicho, polisi hao walimchukua mchungaji akiwa na bukta hadi kwa wakala na kumshurutisha awape namba za siri ambazo aliwapa na wao kutoa pesa.
Baada ya kuwapa fedha hizo, walimrudisha hadi nyumbani kwa mmoja wa polisi hao na kumpa nguo zake lakini wakashikilia simu yake kwa sharti la kumrudishia kama tu angewaongezea Sh100,000.
“Baada ya kuachiwa ndiyo siku iliyofuata alitoa taarifa Takukuru ambao walichukua maelezo yake na viongozi wa juu wa Polisi wakajulishwa.”
Katika uchunguzi wa awali uliofanywa siku hiyo kati ya maofisa wa Polisi na Takukuru, ilithibitika kuwa hakuna jalada lolote lililokuwa limefunguliwa dhidi ya mchungaji wala mtu waliyekuwa naye.
Mbali na kutofunguliwa kwa jalada hilo, uchunguzi ulibaini kuwa ni kweli mchungaji huyo alikutwa katika nyumba hiyo ya kulala wageni na kuchukuliwa na polisi na pia muamala wa fedha kwenye mtandao wa simu ulipatikana.
“Wale polisi walikamatwa na kuwekwa mahabusu hadi leo (jana) walikuwa hawajatoka na tayari walishamrejeshea yule mchungaji pesa zake zote Sh5.4 milioni,” mtoa habari adokeza.
Pia, alidokeza kuwa simu yake ambayo polisi waliishikilia hadi atakapokamilisha malipo ya Sh100,000 amerudishiwa kimyakimya ili suala hilo lisije kuwagharimu.
Hata hivyo, mtu aliyekutwa akiwa na mchungaji huyo hajafahamika wala aliko huku taarifa nyingine zikidai huenda naye ni polisi.
Kaimu Kamanda Mkoa wa Kilimanjaro, Koka Moita alisema askari hao wanne wanashikiliwa kwa madai ya kumkamata mtu anayedaiwa kuwa mchungaji na kumtengenezea mazingira hayo.
“Ni kweli tumepata taarifa na tumezifanyia kazi haraka, kinachofuata sasa ni kumpata huyo anayedaiwa kuwa ni mchungaji ili tuweze kumuhoji athibitishe,” alisema.
Inadaiwa kuwa askari hao wamemshawishi mchungaji huyo akubali kuwasamehe na asiandike maelezo ya uhalisia wa tukio, jambo linaloelezwa kwamba amelikubali.

No comments: