Mwanzilishi wa kampuni ya Facebook Mark Zuckerberg amezuru nchini Kenya katika ziara yake ya mataifa ya Bara la Afrika.
Zuckerberg aliwasili siku ya jumatano akitokea nchini Nigeria, alifanya kikao na Waziri wa habari nchini Kenya, Joseph Mucheru ambapo walizungumza kuhusu mtandao na mipango ya serikali kuhakikisha kila kijiji kimeunganishwa na mtandao.
Baadae Zuckerberg alielekea katika hoteli ya Mama Oliech katika chakula cha mchana ambapo kwa mara ya kwanza alikula ugali na samaki.
"Swala muhimu ninapozuru taifa lolote jipya ni kujaribu kula chakula chao, nilipenda sana Ugali na samaki mzima wa Tilapia" alisema Zuckerberg.
Friday, September 2, 2016
MARK ZUCKERBERG AONESHA UTOFAUTI WAKE AFRIKA.
MELANIA TRUMP ALISHITAKI GAZETI LA DAILY MAIL LA UINGEREZA.
Melania Trump amelishitaki gazeti la Daily Mail la Uingereza pamoja na mwanablogu wa Marekani akitaka alipwe $150m (£114m) kuhusiana na tuhuma kwamba alikuwa kahaba miaka ya 1990, wakili wake amesema.
Gazeti la Daily Mail lilidokeza kwamba huenda Trump alifanya kazi ya muda kama kahaba New York, na kwamba alikutana na mumewe Donald Trump ambaye kwa sasa anawania uraisi mapema kuliko inavyodhaniwa.
Mwanablogu Webster Tarpley aliandika kwamba Bi Trump anahofia sana maisha yake ya awali yasifichuliwe kwa umma.
Madai hayo ni uongo mtupu, wakili wake Charles Harder amesema.
"Washtakiwa walitoa tuhuma kadhaa kuhusu Bi Trump ambazo ni za uongo 100% na kumharibia sana sifa" Bwana Harder alisema.
Bi Trump 46 alizaliwa Slovenia na akahamia Marekani kufanya kazi kama mwanamitindo miaka ya 1990. Aliolewa na Trump 2005.
Gazeti la Daily Maily lilinukuu madai yaliyokuwa yamechapishwa na jarida moja la Slovenia kwa jina Suzy kwamba wakala wa uanamitindo ambaye Bi Trump alikuwa akifanyia kazi wakati huo pia alihudumia kama wakala wa kutafutia kazi makahaba, nyaraka za mahakama zinaonesha.
Gazeti hilo pia lilimnukuu mwanahabari wa Slovenia Bojan Pozar, ambaye aliandika kitabu kuhusu maisha ya Bi Trump ambacho hakijaidhinishwa, ambaye alidai kwamba Melania alipigwa picha za utupu New York mwaka 1995 na akadai kwamba mwanamke huyo alikutana na Trump miaka mitatu kabla ya wakati ambao inadaiwa walikutana, ambayo ni mwaka 1998.
Wakili wake anasema alihamia Marekani mwaka 1996.
Tarpley alidai kuwa Melania ana wasiwasi sana huenda wateja wake matajiri wa wakati huo wakafichua siri yake na kwamba alikuwa na mfadhaiko.
Thursday, September 1, 2016
TANZANIA YAWEKA HISTORIA KWA TUKIO LA KUPATWA KWA JUA.
Wageni kutoka mataifa mbalimbali ya Afrika na Ulaya, pamoja na mwanasayansi wa anga wapo katika mji wa Rujewa mkoani Mbeya, kusini magharibi mwa Tanzania, kushuhudia tukio la kihistoria la kupatwa kwa jua kwa kiwango cha asilimia 97 kwa mujibu wa wataalamu wa masuala ya anga.
Tukio kama hilo hutokea baada ya miaka mingi, ambapo tukio la mwisho lilikuwa mwaka 1977.
Wednesday, August 31, 2016
WAZIRI AUAWA KOREA KASKAZINI BAADA YA KUONEKANA AKISINZIA MKUTANONI.
Serikali ya Korea kusini imesema kuwa waziri wa elimu nchini Korea kaskazini ameuawa na maafisa wa serikali.
Waziri huyo wa elimu Kim Yong-jin anadaiwa kusinzia katika mkutano wa kiongozi wa nchi hiyo Kim Jong-un.
Baadhi ya ripoti zinasema waziri huyo ambaye amekuwa pia akihudumia kama mmoja wa manaibu wa waziri mkuu, alitekwa na usingizi wakati wa mkutano huo jambo ambalo lilichukuliwa kama kumkosea heshima kiongozi huyo.
Maafisa wa Korea kusini wamesema wanaamini waziri huyo aliuawa kwa kupigwa risasi mwezi Julai.
Serikali hiyo inasema maafisa wengine wawili walilazimishwa kwenda kuishi maeneo ya mashambani, "kupewa upya mafunzo".
Korea kusini iliwahi kutoa taarifa kwamba kiongozi wa jeshi la Korea kaskazini Ri Yong-gil alikuwa ameuawa mwezi February mwaka huu.
Lakini mwezi Mei mwaka huu, ilibainika kwamba bado yupo hai na alikuwa akihudhuria mikutano na hafla za serikali.
Mara ya mwisho Korea kaskazini kutangaza hadharani kwamba ilikuwa imemuua afisa mkuu serikalini ilikuwa ni mwaka 2013 wakati mjombaake Rais wa nchi hiyo Chang Song-Thaek aliuawa mwaka 2013.
Tangazo la kifo cha Kim Yong-jin limetolewa na wizara ya muungano ya Seoul na limetolewa siku chache baada ya taarifa za gazeti moja kusema maafisa wawili wakuu wa Korea kaskazini waliuawa kwa kulipuliwa kwa makombora ya kutungua ndege.
Gazeti hilo lilisema wawili hao waliuawa mapema mwezi huu.
Watu zaidi ya kumi wameuawa tangu Kim Jong-un achukue hatamu miezi mitano iliyopita.
Baadhi ya wachanganuzi wa masuala ya siasa wanasema huenda kiongozi huyo, mwenye umri wa miaka 32 hutumia njia ya kuwaua watu hadharani kusisitiza udhibiti wake kama kiongozi.
Mapema mwezi huu, Naibu balozi wa Korea kaskazini nchini Uingereza aliikimbia nchi yake na kuhamia rasmi kusini.
RAIS MAGUFULI AFANYA UTEUZI MWINGINE.
Rais Dkt. John Pombe Magufuli amemteua Doto James kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango.
Taarifa ya Ikulu jijini Dar es salaam imesema kabla ya uteuzi huo Doto James alikuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango (Sera).
Doto James ataapishwa Septemba mosi, ikulu jijini Dar es salaam.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo kufuatia uteuzi huo aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Dkt. Servacius Likwelile atapangiwa kazi nyingine.
CHADEMA WASITISHA MAANDAMANO YA UKUTA.
Chama pinzani cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimesitishwa leo maandamano yaliyopangwa kufanyika siku ya jana.
Viongozi wa upinzani wakiwemo Edward Ngoyai Lowasa wa Chadema wametangaza hatua hiyo kwenye kikako na waandishi wa habari jijini Dar es salaam.
Wamesema wamehairisha maandamano hayo kwa kipindi cha mwezi mmoja baada ya kusikia ombi la viongozi wa kidini na wadau wengine waliowaomba kukumbatia na kuyapa muda mazungumzo.
Viongozi wa Chama hicho walikuwa wameitisha maandamano na mikutano ya kisiasa Septemba mosi, kupinga walichosema kuwa ni ukandamizwaji unaoendelezwa na serikali.
Baada ya mkutano wa kikao cha Kamati kuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) mwishoni mwa Julai, viongozi walisema "yapo matukio ambayo yamekuwa yakifanywa na kukandamiza demokrasia na misingi ikipuuzwa na kudharauliwa".
"Si nia ya Chadema kugombana na serikali bali ni kazi ya chama pinzani kusaidia serikali iongoze kwa kufata misingi ya katiba" chama kilisema.
Maandamano hayo yalipewa jina la UKUTA, ikisimamia Umoja wa Kupambana na Udikteta Tanzania.
Serikali ilipiga marufuku mikutano yote ya kisiasa ya hadhara na ukumbini. Baadhi ya viongozi wa upinzani wamekamatwa na kuzuiliwa kwa muda.
KODI ZA SIMU ZAONGEZA KIPATO NCHINI.
Sheria ya fedha ya mwaka 2016 iliyopitishwa kuhusu utozaji wa ushuru kwenye ada ya kutuma na kupokea fedha kwenye miamala ya benki na simu, imeanza kuzaa matunda kutokana na ongezeko la mapato lililoanza kushuhudiwa kutoka kampuni za simu.
Kamati ya kudumu ya Bunge ya miundombinu iliyokutana jana na Mamlaka ya Mawasiliano (TCRA) iliambiwa kutokana na sheria hiyo iliyopitishwa na Bunge baada ya kupitisha bajeti ya mwaka huu, mwezi uliopita serikali imeshuhudia ongezeko kubwa la mapato yaliyotolewa na kampuni za simu.
Taarifa hiyo ilitolewa jana na kamati ya kudumu ya Miundombinu, imeonesha kampuni ya Vodacom ilikuwa ikitoa kodi ya ushuru wa bidhaa kwa fedha zinazotumiwa kwa wastani wa Sh.milioni 360 kwa mwezi, lakini baada ya mabadiliko ya sheria Julai pekee mwaka huu imelipa Sh.bilioni 1.9.
Mwakilishi wa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato (TRA), Godwin Barongo aliiambia kamati hiyo kuwa kwa upande wa kampuni ya Tigo walikuwa wanatoa wastani wa sh.milioni 250 kwa mwezi lakini sasa wametoa jumla ya sh.bilioni 1.48.
Barongo ambaye ni Meneja msaidizi kitengo cha walipa kodi wakubwa TRA alikuwa akizungumzia namna mtambo maalumu wa kusimamia mawasiliano na udhibiti wa mapato yatokanayo na simu (TTMS) unaosimamiwa na mamlaka ya mawasiliano (TCRA) ulivyowezesha kufanikisha ukusanyaji mapato.
"Pamoja na mabadiliko ya sheria yaliyoanza mwenzi Julai mwaka huu, kampuni za simu zilikuwa zikitoza transfer, lakini sheria ilikuwa haigusi kwenye kutoa. Baada ya hiyo tuligundua kuwa sasa kamisheni nyingi zilipelekwa kwenye kutoa kwa sababu hakuna tozo na kwenye transfer zinapungua" alisema Barongo.
Aliendelea kusema "kwa hiyo mabadiliko haya ya sheria ya sasa hivi ambayo tunatoza kwenye kuweka na kutoa, yametusaidia". Makamu mwenyekiti wa kamati ya kudumu ya Bunge ya miundombinu, Selemani Kakoso alisisitiza kuwa wabunge wanategemea Wizara ya miundombinu kupitia sekta ya mawasiliano, ichangie mapato mengi kwa serikali.