Thursday, October 6, 2016

HABARI NJEMA KWA WAKAZI WA DAR ES SALAAM KUWEKEWA HUDUMA YA BURE YA WIFI.


Makamu wa rais nchini Mhe. Samia Suluhu Hassan ametangaza mpango wa kuzindua mradi ambao utapelekea kuwekwa kwa huduma ya mtandao wa WI-FI katika maeneo ya umma na yale ya burudani mjini Dar es Salaam.

Utekelezaji wa mradi huo wa kampuni ya mawasiliano nchini humo utapanua huduma za mawasiliano ili kuweza kuwafikia watu wengi zaidi na hivyo basi kuimarisha uchumi.
''Tunawapongeza kwa kutekeleza mradi huu na tunatumai upandaji wa miti katika maeneo tofauti mjini ikiwemo maeneo ya burudani, watu wataweza kupata huduma ya mtandao ''.
Kwa upande wake Kamishna wa Jimbo la Dar es Salaam, Paul Mkonda amesema kuwa mradi huo ni mmoja wa awamu tano za juhudi za serikali kuimarisha huduma kadhaa hususani mawasiliano na huduma za mtandao kwa wote.

Utekelezaji wa mradi huo ndio mwanzo wa safari ya kujenga miji na miji mikuu katika kiwango cha Smart City nchini Tanzania.

TYSON AKILI KUTUMIA COCAINE ILI KUKABILIANA NA UGONJWA WA KIAKILI.


Bingwa wa ndondi katika uzani mzito duniani, Tyson Fury amesema amekuwa akitumia Cocaine ili kumsaidia kuyakabili matatizo ya kiakili.

Bondia huyo wa Uingereza amesema kuwa amekuwa akiugua ugonjwa wa kiakili kwa miaka kadhaa na hajafanya mazoezi tangu mwezi Mei. Nimekuwa nje nikilewa, Jumatatu hadi Jumapili na kutumia Cocaine, Fury aliliambia jarida la Rolling Stones.

Hatua hiyo inajiri siku mbili baada ya Fury kudai katika mitandao ya kijamii kwamba amejiuzulu, kabla ya kukana madai hayo saa tatu baadaye akisema alikuwa akifanya utani.

Akizungumza kuhusu maswala ya afya yake Fury aliongezea ''siwezi kukabiliana na matatizo haya na kitu kinachonisaidia ni wakati ninapokunywa ili nitoe matatizo hayo akilini, wanasema nina ugonjwa wa kiakili, nahisi huzuni, ningependa mtu aniue kabla ya kujiua.


SAMSUNG GALAXY NOTE 7 YALIPUKA NDANI YA NDEGE.


Simu ya kampuni ya Samsung aina ya Galaxy Note 7, ambayo ilikuwa imethibitishwa na kampuni hiyo kuwa ilikuwa salama, imeshika moto kwenye ndege nchini Marekani.

Simu hiyo inadaiwa kushika moto ikiwa na abiria aliyekuwa kwenye shirika la ndege la Southwest Airlines. Shirika hilo limesema abiria waliokuwa kwenye ndege moja yake, iliyokuwa imepangiwa kusafiri kutoka Louisville, Kentucky hadi Baltimore, Maryland waliondolewa kwenye ndege kwa dharura kabla ya ndege hiyo kupaa Jumatano.

Kampuni ya Samsung iliwashauri watu waliokuwa wamenunua simu za Note 7 kuzirejesha kwa kampuni hiyo baada ya kugunduliwa zilikuwa na tatizo kwenye betri zake. Samsung inasema bado inachunguza kisa hicho cha Jumatano.

''Tunashirikiana na maafisa wa serikali na maafisa wa shirika la Southwest kupata simu hiyo na kuthibitisha chanzo cha moto huo'' kampuni hiyo imesema kupitia taarifa.
Msemaji mmoja wa shirika la Southwest amesema '' abiria mmoja alitufahamisha kuhusu moto uliokuwa unafuka kutoka kwa simu. Abiria wote na wahudumu wa ndege waliondolewa salama kutoka kwenye ndege''.

Mmiliki wa simu hiyo Brian Green akizungumza na Jordan Golson wa shirika la The Verge, amesema alinunua simu hiyo tarehe 21 Septemba.

Amesema simu hiyo ilikuwa na alama ya mraba ya rangi nyeusi kwenye pakiti yake, alama ambayo iliongezwa na kampuni ya Samsung kutofautisha kati ya simu zilizokuwa zimeuzwa awali ambazo zilidaiwa kutokuwa salama na simu mpya zilizokuwa zimechunguzwa.

WATU SITA WAUAWA NA AL-SHABAB NCHINI KENYA.


Watu sita wameuawa baada ya watu wenye silaha kushambulia mtaa mmoja mjini Mandera, Kaskazini Mashariki mwa Kenya. Taarifa zinasema washambuliaji hao walivamia eneo lenye nyumba za makazi Bulla usiku wa manane.

Gavana wa jimbo la Mandera, Ali Roba ameandika kwenye twitter kwamba watu sita wameuawa na mmoja kujeruhiwa, amesema watu 27 kati ya 33 waliokuwa kwenye plot hiyo wameokolewa na maafisa wa usalama.

kituo kimoja cha redio kinachojihusisha na kundi la Al-shabab kimesema wanamgambo hao ndio waliotekeleza shambulio hilo. Gazeti la Daily Nation limeripoti kuwa watu walioshambulia walikuwa watu kutoka maeneo mengine.

Gazeti la Standard nalo linasema kuwa walioshambuliwa walirusha guruneti kwanza na kisha wakaingia ndani na kufyatulia risasi waliokuwemo.

Roba alisema dalili zote zinaashiria wavamizi hao walikuwa wa kundi la Al-shabab. Eneo la Mandera limekuwa likishambuliwa mara kwa mara na wapiganaji wa Al-shabab kutoka Somalia.

Kenya ilipeleka vikosi vyake vya jeshi nchini Somalia mwaka wa 2011 ikitaka kuzima mashambulizi ya mara kwa mara na kuisaidia serikali inayoungwa mkono na umoja wa mataifa.


Monday, September 19, 2016

TANZIA: NGULI WA MUZIKI AFRIKA KUSINI MANDOZA AFARIKI DUNIA.

Mandoza

Nguli wa muziki nchini Afrika kusini Mduduzi Tshabalala maarufu kama Mandoza amefariki baada ya kuugua saratani kwa kipindi cha mwaka mmoja.

Amefariki dunia akiwa na miaka 38.

Mandoza alisifika kwa album kadhaa za mziki aina ya kwaito, aina ya mziki wa Afrika kusini ambao hukaribiana sana na Hip hop.

Nyimbo zake nyingi zilivuma zikiwemo nyimbo kutoka albamu yake ya kwanza Nkalkatha. Familia ya Mandoza imesema kuwa mwanamziki huyo aligundulika kuwa ana saratani baada ya kuanza kuumwa na kichwa sana pamoja na kutatizwa na macho mwaka mmoja uliopita.


RADI YAUA WATU NA WENGINE KUJERUHIWA SHINYANGA.

Kamanda Mkuu wa polisi mkoani Shinyanga Muliro Jumanne.

Watu wawili wamepoteza maisha na wengine watano kujeruhiwa baada ya kupigwa na radi wakiwa wamejikinga na mvua chini ya mti kando ya malambo ya kunyweshea mifugo katika kijiji cha Ntundu kata ya Busangi katika halmashauri ya Msalala wilaya ya Kahama, mkoa wa Shinyanga.

Kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga, Muliro Jumanne alisema ajali hiyo ilitokea juzi 8:30 mchana katika kijiji hicho wakati mvua ilipokuwa ikinyesha, ndipo watu hao wakaamua kujikinga kwenye mti na radi ikapiga na kusababisha vifo vyao.

Aliwataja waliokufa kuwa ni Fikiri Paschal (35) na Maneno Luzalia (16), wakati waliojeruhiwa na kupata mshituko baada ya radi kupiga ni watano ambao ni Mhoja Pasiani (32), Abel Feleshi (12), Nhungwa Jeremiah (22), Juma Mussa (16) na Paschal Mabula (11) ambaye ni mwanafunzi wa Ntundu.

Aliwataka wananchi kutokaa karibu na miti hasa kipindi hiki cha mvua za masika zinapokaribia kunyesha kwa wingi ili kuepuka tukio kama hilo ambalo limepoteza maisha ya watu, huku akifafanua kuwa katika mfumo wa umeme pia kuna madhara.


WAZIRI MKUU KASSIM MAJALIWA ASISITIZA KUWA HALI YA UCHUMI KWA SASA NI SHWARI.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa

Serikali imesema hali ya uchumi kwa sasa ni shwari kabisa na inaendelea kuimarika, si mbaya kama inavyodhaniwa na kupotoshwa na baadhi ya watu.

Aidha imesema imejipanga vizuri katika kuimarisha uchumi endelevu, usimamizi thabiti wa raslimali za umma na ujenzi wa miundombinu bora yenye kuimarisha lengo la kujenga uchumi wa viwanda chini ya mpango wa pili wa maendeleo ya miaka mitano.

Hayo yalisemwa bungeni jana na Waziri Mkuu alipokuwa akielezea mwenendo na mwelekeo wa hali ya uchumi nchini wakati akihairisha vikao vya bunge vya mkutano wa nne wa bunge la 11 lililoketi kwa wiki mbili kuanzia Septemba 6.

Alisema katika siku za hivi karibuni kumekuwepo na wasiwasi kuhusu mwenendo wa uchumi, hususani mtiririko wa fedha kwenye uchumi wa taifa, hivyo alitumia fursa hiyo kuwahakikishia wabunge na watanzania kwa ujumla kuwa mwenendo wa uchumi ni wa kuridhisha na unaendelea kuimarika.

Aliongeza kuwa tathimini iliyofanyika kuhusu viashiria vya uimara wa sekta ya fedha inaonesha kuwa benki nchini zipo salama, zina mitaji ya kutosha na mwenendo wa sekta ya fedha ni wa kuridhisha.