Saturday, October 8, 2016

VALENCIA AWATOROKA MAPOLISI.

enner_valencia-496713
Mshambuliaji wa kimataifa wa Ecuador anayeichezea klabu ya Everton ya England kwa mkopo akitokea West Ham United Enner Valencia amerudi kwenye headlines baada ya kuwakwepa mapolisi waliokuwa wanasubiri mechi imalizike wa mkamate.
Valencia alifanikiwa kufanya hivyo  dakika ya 82 katika mchezo wa kuwania kufuzu kucheza Kombe la dunia 2018 dhidi ya Chile mchezo ambao ulimalizika kwa Ecuadorkuondoka na ushindi wa goli 3-0, Valencia mwenye umri wa miaka 26 anakabiliwa na kesi ya kutakiwa kulipa dola 17000 ambazo ni zaidi ya Tsh milioni 30 kama gharama za matunzo ya mtoto wake wa kike mwenye umri wa miaka mitano aliyezaa na mke wake wa zamani
Maafisa wa mahakama ambao wamejaribu kutaka kumkata Valencia kwa zaidi ya mara moja, safari hii aliwakimbia kwa staili ya kujifanya ameumia dakika ya 82 na kutolewa nje akiwa kawekewa mashine ya Oxygen na kukimbizwa katika ambulace na kuondolewa uwanjani haraka na mapolisi kushindwa kumtia nguvuni.

SERIKALI YAPINGA KUKODISHWA KWA YANGA.

                                                                  YUSUF MANJI.

Serikali kupitia Baraza la Michezo la Taifa (BMT) imesema kuwa mkataba wa Mwenyekiti wa Yanga, Yusuf Manji kukodishwa klabu hiyo ni batili. Tamko hilo limetolewa jana na Kaimu Katibu Mkuu wa BMT, Mohamed Kiganja baada ya juzi kusambaa kwa taarifa ya mkataba wa Yanga katika mitandao ya kijamii.

Suala la Yanga kukodishwa timu lilianza mchakato tangu Manji aitishe mkutano mkuu wa dharura miezi miwili iliyopita, akiomba ridhaa ya wanachama wa klabu hiyo kumkodisha timu na nembo kwa miaka 10, ombi ambalo lilipitishwa na kurudishwa katika bodi ya wadhamini kwa ajili ya kufanyiwa kazi na juzi kupitishwa kwa makubaliano hayo.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kiganja alisema wanaunga mkono suala la mabadiliko, lakini lazima yafuate sheria na taratibu zilizowekwa ili kukamilisha mabadiliko yoyote.

“Mimi sipingi klabu zetu kufanya mabadiliko isipokuwa najaribu kukumbusha zifuate utaratibu wa kisheria, kwa sababu unapobadilisha jina au kufanya marekebisho yoyote ni lazima vikasajiliwe na kutambulika,”alisema.

Kiganja alisema hata Bodi ya Yanga iliyohusika kuruhusu timu hiyo kukodishwa haitambuliki kwa Msajili, kwa vile wajumbe wake wengi ni wale waliochaguliwa kwa mpito. Alisema bodi ya wadhamini iliyoundwa Julai 5, 1973 ni wawili tu wanaotambulika waliopo hadi sasa ambao ni Jabir Katundu na Juma Mwambelo.

Lakini, Mwembelo amekuwa ahusishwi tena katika mambo yanayoendelea ya timu hiyo. Bodi ya mpito, ambayo Kiganja alisema hawakusajiliwa wala kupitishwa kwenye mkutano mkuu kutokana na taratibu ni George Mkuchika, Fatuma Karume, Francis Kifukwe, Amri Ramadhan, Juma Kambi na Abeid Mohamed.

Katibu huyo alifafanua taratibu zinazotakiwa kufuatwa ili timu ikodishwe kuwa ni kutumia vikao, ambapo cha kwanza ikiwa ni Kamati ya Utendaji ya Klabu itakayochambua hoja na kukubaliana au kutokukubaliana kisha kupeleka katika kikao cha ngazi za juu.

Pia, alisema baadaye hoja inapelekwa kwenye mkutano mkuu wa wanachama wote uwe wa dharura au kawaida ili kujadiliana hoja husika, kisha baada ya kukubaliana au kutokukubaliana inapelekwa kwa Baraza la wadhamini lenye uwezo wa kuingia kwenye maamuzi makubwa, na mwisho inapelekwa kwa msajili.

“Kwa mujibu wa sheria ya BMT ya mwaka 1967 kifungu namba 11 (1) kinaeleza chama chochote kinachofanya mabadiliko ya jina, anuani, madhumuni au kifungu chochote cha Katiba yake kitatakiwa kipate idhini ya msajili,”alisema.

Alisema kifungu namba 11 (3) msajili anaweza kuyakataa maombi ya kubadili kifungu chochote cha katiba kama ataona kuwa mabadiliko yanaweza kuhatarisha usalama na kuvuruga amani, au kama kuna malengo ya kuwanufaisha wachache au kama hayazingatii sera za michezo na sheria za BMT.
Alisema baada ya hatua hizo kukamilika, inabidi kufanya marekebisho ya Katiba ambayo yatapitia kwenye taratibu za klabu, na ndipo klabu husika itakuwa imepata baraka za serikali.


Katibu huyo aliweka wazi kuwa amezungumza hayo kwa kuwa yeye ni kiongozi na mlezi wa vyama vya michezo nchini na kwamba, maelezo yake hayalengi kuwakatisha tamaa wale walionesha nia ya kuwekeza kwenye michezo bali kuwambushana mambo ya msingi kwa manufaa

MWANAMKE ALIYEMNYOFOA ULIMI KIJANA AFIKISHWA MAHAKAMANI.


Mwanamke anayedaiwa kumng'ata ulimi kijana Saidi Mnyambi (26) siku 28 zilizopita, kwa kile kilichodaiwa kutaka kufanya naye mapenzi kwa nguvu, hatimaye amefikishwa katika Mahakama ya wilaya ya Singida.

Mwanamke huyo, Mwajabu Jumanne (36) mkazi wa eneo la Mandewa nje kidogo ya mji huu amefikishwa mbele ya Hakimu Flora Ndale akishitakiwa kwa kosa la kujeruhi kwa kunyofoa theluthi moja ya ulimi wa kijana Mnyambi wakati wakipeana denda.

Wakili wa Serikali, Michael Ng'hoboko alidai mbele ya hakimu Ndale kuwa Septemba 12 mwaka huu majira ya saa 2.45 usiku katika eneo la Mandewa Manispaa ya Singida, kwa makusudi, mama huyo alimng'ata ulimi Mnyambi na kumsababishia jeraha na maumivu makali.

Mwendesha mashitaka huyo alidai kuwa mshitakiwa Mwajabu alitenda kosa hilo kinyume na kifungu namba 225 cha Kanuni ya adhabu Sura ya 16 Sheria za nchi kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.

Mshitakiwa alikana kosa na kesi hiyo iliahirishwa hadi Oktoba 24 itakapotajwa tena.

Mshitakiwa yupo nje kwa dhamana ya watu wawili waliotoa ahadi ya Sh milioni moja kila mmoja

Friday, October 7, 2016

HABARI YA KUSIKITISHA YA KIJANA ALIYETOLEWA MACHO MAENEO YA BUGURUNI JIJINI DAR ES SALAAM HAWEZI KUONA TENA.


Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Paul Makonda ametoa majibu kuhusu hatma ya kijana Said Ally aliyetobolewa macho maeneo ya Buguruni Sheli na kusema hatoweza kuona tena.

Makonda ametoa hayo majibu yake ofisini kwake asubuhi ya leo, Ijumaa;
''Majibu yametoka na Said ameturuhusu tuyaweke wazi, majibu ni mabaya ila tumeyapokea, itabidi tukubaliane na matokeo kwamba ndugu yetu hatoweza kuona tena kwa maisha yake yote'' alisema Makonda.
''Serikali ya mkoa imejitolea kumpatia matibabu ya macho bandia kwa ajili ya kutengeneza shepu ya uso wake tena, kumpatia elimu ya kusoma tena kujifunza kwa alamaili aweze kuendana na mazingira na pia Serikali ya mkoa imetoa gari kwa ajili ya kumsaidia kipindi chote atakachokuwa kwenye matibabu yake'' alisema.
Pia Makonda amesema serikali itatoa kiasi cha shilingi Milioni 10 kama sehemu ya mtaji wake. Kabla ya kupatwa na ulemavu huo Said alikuwa kinyozi hivyo kuna mdogo wake yupo atamsaidia kwakuwa mwanzoni walikuwa wakifanya kazi pamoja.



 

FAMILIA YA MWANASOKA DAVID BECKHAM IKIWA NCHINI KENYA.

Star wa soka duniani, David Beckham akiwa na familia yake nchini Kenya wakishiriki kampeni ya Beyond Zero inayosimamiwa na First Lady wa Kenya Margaret Kenyatta.
Picha zinamuonesha Mke wa Beckham, Victoria akiwa maeneo ya Kiambu siku ya Alhamisi akiongozana na mtoto wake wa kiume BrooklynVictoria Beckaham ambaye ni Balozi wa UNAIDS ametoa msaada wa Mobile Clinic na Gari moja ya kubeba wagonjwa.



F

SIMBA YAMUOMBA RADHI RAIS MAGUFULI KWA VURUGU NA UHARIBIFU WA UWANJA TAIFA.

                                         OFISA HABARI WA SIMBA, HAJI MANARA.
Rais wa Simba, Evans Aveva na Kamati yake ya Utendaji kwa niaba ya benchi la ufundi, mashabiki na wanachama wa klabu hiyo wameomba radhi kwa Rais John Magufuli kutokana na vurugu za Uwanja Taifa Dar es Salaam mwishoni mwa wiki iliyopita.

Simba ilicheza mechi ya Ligi Kuu na Yanga, lakini mashabiki wake walifanya vurugu na kung’oa viti vya uwanja huo wakipinga bao la kuongoza la Amisi Tambwe baada ya mchezaji huyo kushika mpira kwa mkono kabla ya kufunga. Tukio hilo lilisababisha vurugu kubwa iliyosababisha polisi kupiga mabomu ya machozi ili kutawanya mashabiki.

Serikali imetangaza kuufungia uwanja huo kwa timu hizo.

Akizungumza na wandishi wa habari jana, Ofisa Habari wa Simba Haji Manara alisema kwa moyo wa dhati na unyenyekevu mkubwa wameona umuhimu wa kuomba radhi kwa kitendo cha mashabiki wachache kuharibu rasilimali ambazo zimejengwa na kodi za Watanzania wote.

“Rais ndiye msimamizi wa rasilimali za nchi hii hivyo tumemwandikia barua Waziri wa Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo, Nape Nnauye tukamwomba atuombee radhi kwa Rais kwa kitendo cha mashabiki wetu kung’oa vitu kwenye mchezo uliochezwa Oktoba mosi dhidi yetu na Yanga,” alisema Manara.

Manara alisema wakati wao wakiwa wamekaa jukwaa kuu na kuona tukio lile likitendeka walitamani kuruka kwenda kuwasihi mashabiki wasing’oe viti na kuahidi kuwa halitatokea tena kwani limeshusha thamani ya klabu.

Pia Manara aliiomba serikali kupitia kwa Meneja wa Uwanja wa Taifa kufunga kamera ili kusaidia kubaini waharibifu kwani endapo kamera zingekuwa zinafanya kazi wangewabaini mashabiki hao na kuwachukulia hatua.

Manara alifika mbali na kuomba polisi wanaolinda usalama wakati mechi zikichezwa wawe wanatazama mashabiki kuliko ilivyo sasa wanatazama mechi na kusahau majukumu yao.
Katika hatua nyingine, Simba imeilalamikia TFF (Shirikisho la Soka Tanzania) na Bodi ya Ligi kwa kutokuwa makini katika kupanga waamuzi wenye weledi wa sheria 17 za soka hasa kwenye mechi kubwa ya Simba na Yanga.

“Haiwezekani mwamuzi (Martin Saanya) anatoka kufungiwa mwaka mmoja na anapewa kuchezesha mechi kubwa kwenye ukanda huu wa Afrika Mashariki na Kati, huko ni kukosekana kwa umakini kwa vyombo vinavyosimamia soka nchi hii,” alisema Manara.


“Mwamuzi alishindwa kumudu mchezo alikuwa anatoa maamuzi ambayo yalionekana dhahiri kuwa na faida upande wa pili hili ni suala ambalo linatakiwa kutazamwa kwa makini,” alisema Manara.

WALIMU WALIOMPIGA MWANAFUNZI KIPIGO CHA MWIZI, WATOROKA.

                                             WAZIRI WA ELIMU JOYCE NDALICHAKO
Walimu wanafunzi wanne wa Chuo Kikuu cha Elimu Dar es Salaam (Duce) na cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere waliohusika kumpiga vibaya mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Mbeya wamefukuzwa chuo huku Jeshi la Polisi mkoani Mbeya likiwashikilia kwa mahojiano walimu wengine watano wa shule hiyo kutokana na tukio hilo.

Aidha, serikali imemvua madaraka Mkuu wa shule hiyo, Magreth Haule kwa kutochukua hatua baada ya kitendo hicho kufanyika shuleni hapo Septemba 28, mwaka huu.

Hatua hizo zimechukuliwa baada ya jana katika mitandao ya kijamii kusambaa kipande cha video kikionesha walimu zaidi ya watatu wakiwa eneo la ofisi wakimshambulia kwa kumpiga makofi, mateke na fimbo sehemu mbalimbali za mwili hasa kichwani mwanafunzi Sebastian Chinguku.
Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako ametangaza kuwafukuza chuo walimu wanafunzi hao walioshiriki kitendo cha kumpiga mwanafunzi huyo wa kidato cha tatu wa Shule ya kutwa ya Sekondari ya Mbeya.

Walimu hao ni Frank Msigwa (anayedaiwa kumpiga zaidi mwanafunzi huyo kwa makofi kichwani), John Deo na Sante Gwamaka wote wa Duce na Evans Sanga wa Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere.

Akizungumza na vyombo vya habari jijini Dar es Salaam jana, Profesa Ndalichako alisema kitendo hicho ni cha kikatili, jinai na kuwa walimu hao wanafunzi hawafai kuendelea na taaluma hiyo ya ualimu na kuwa hatua zaidi za kisheria zinaendelea kuchukuliwa dhidi yao.

Profesa Ndalichako alisema kwa mujibu wa taratibu za vyuo vikuu kitendo kilichofanywa na walimu wanafunzi hao ni kosa la jinai na kuwa hakiwezi kufumbiwa macho. Alitoa onyo kali kwa wanafunzi wanaokwenda kwenye mafunzo kwa vitendo na kwenda kinyume cha taaluma yao kuwa wanapoteza sifa hivyo amewataka kuzingatia maadili ya fani na taaluma wanazosomea.

Mkoani Mbeya, Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Dhahiri Kidavashari alisema wanawashikilia walimu wa shule hiyo watano kwa mahojiano kuhusu tukio hilo. Hata hivyo, alisema si kwamba walimu hao wanaohojiwa ndio waliohusika na tukio hilo bali wameanza na wale waliopo ili kupata taarifa zaidi.
“Hatuwezi kusema sasa hivi kama wale walimu ndio walioonekana katika kipande cha video kinachosambaa mitandaoni kwa kuwa hili ni suala la mahojiano, tunaamini hawa tulionao wanaweza wakatupa mwanga,” alisema.

Akieleza sababu ya adhabu hiyo, Kamanda alisema katika mahojiano ya awali imebainika kuwa mwalimu wa Kiingereza alitoa kazi, lakini baadhi ya wanafunzi hawakufanya baadaye mwalimu huyo aliwapa adhabu ya kupiga magoti, lakini mwanafunzi huyo alionekana kupinga kwa kueleza ana tatizo la goti hatoweza kufanya adhabu hiyo na mwalimu aliamua kumpeleka ofisini na kumpiga kwa kumchangia.

“Mwalimu aliwaadhibu wanafunzi darasani na alipotaka kumuadhibu mwanafunzi huyo mbele ya darasa, alionesha kupinga kupigwa mbele ya wanafunzi wenzake ndipo alipoamua kumpeleka ofisini na kutokea tukio linalosambaa,” aliongeza Kidavashari.

Katika taarifa yake, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba, alisema Septemba 28 mwaka huu, mwanafunzi Chinguku wa kidato cha tatu wa Shule ya Sekondari Mbeya, mkazi wa Uyole, alipigwa na walimu watatu.

“Nimeelekeza vyombo vya dola Dar es Salaam wawatafute chuoni kwao hao walimu kuhusiana na shambulio hilo kwa mwanafunzi huyo,” ilisema Mwigulu.

Naye Waziri katika Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), George Simbachawene ameagiza mamlaka za nidhamu kumvua madaraka Mkuu wa Shule hiyo, Haule kwa kushindwa kuchukua hatua na kutoa taarifa mara baada ya tukio hilo kufanywa na walimu hao shuleni hapo.

"Kwa kuwa waliotenda kosa hili wametoweka tangu Septemba 29, 2016 na hawajulikani walipo, nimesikitishwa kwa kitendo cha mwalimu mkuu wa shule hiyo, Magreth Haule kutochukua hatua. Hii inaonesha kulikuwa na dalili za kutaka kulificha tukio hili baya.

“Na kwa sababu hiyo, pamoja na kwamba wanaendelea kuhojiwa na Polisi, naagiza mamlaka yake ya nidhamu kumvua madaraka mkuu huyo wa shule," alisema Simbachawene katika taarifa yake kwa umma jana. Katika hatua nyingine, Rais wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Gratian Mukoba amelaani kitendo kilichofanywa na walimu hao na kukieleza kuwa ni cha mwituni na cha kinyama kwa kuwa hakuna adhabu kama hiyo katika utumishi wa ualimu.

"Nami nimeona hiyo video katika mitandao ya kijamii, kuna sheria za adhabu za viboko lakini si hii walioifanya hao walimu vijana maana walikuwa wakipiga makofi, ngumi, mateke, ngwara. Hizi hazipo kwenye ualimu, lazima wafuate sheria zinazosimamia utumishi wa walimu," alisema Mukoba.
Alishauri vyuo vya ualimu viweke mkazo katika kufundisha walimu vijana namna ya kuwa zaidi ya walimu, kuwa na uvumilivu, subira na kuzingatia sheria. Wafunzwe kisaikolojia kukubali kuwa hawaishii kuwa walimu bali wanaingia kwenye kundi la malezi.

Alisema kwa tukio hilo, ni lazima sheria ichukue mkondo wake ili iwe fundisho kwa wengine wenye tabia hizo hasa walimu vijana kwa kuwa kitaaluma ni tukio la kinyama lisilokubalika.
“Hata kama mwanafunzi ana makosa, amevuta bangi, huwezi kumuadhibu vile, maana pale hujui nani kavuta bangi nani mzima,” alisema Mukoba.

Awali, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Amos Makalla alisema serikali inalifuatilia kwa karibu tukio la kupigwa kama mwizi mwanafunzi huyo wa shule hiyo ya jijini Mbeya na kusema tayari baadhi ya walimu akiwemo mkuu wa shule, wanashikiliwa na Polisi.

Makalla alibainisha hayo jana kwenye Maadhimisho ya Siku ya Fimbo Nyeupe Duniani yaliyofanyika kitaifa mkoani Mbeya na kusisitiza kuwa walimu waliohusika na tukio la kumpiga mwanafunzi wao kama mwizi wanasakwa na lazima watapatikana.

Alisema Septemba 26, mwaka huu, mwalimu aliyekuwa katika mafunzo kwa vitendo katika shule ya Sekondari ya Mbeya Day aliyemtaja kwa jina la Frank Msigwa alitoa kazi kwa wanafunzi darasani na Septemba 28 alipokuwa akisahihisha kazi zilizofanyika alibaini baadhi ya wanafunzi hawakufanya.
Makalla alifafanua kuwa miongoni mwa wanafunzi aliobaini hawakufanya kazi yake ni pamoja na Chinguku na ndipo aliwatoa nje ya darasa na kuwapa adhabu ya kupiga 'push up' lakini mwanafunzi huyo akagoma akidai kuwa na matatizo ya kiafya katika mbavu zake.

Alisema baada ya kugomea adhabu hiyo mwalimu aliwaamuru wapige magoti lakini pia mwanafunzi huyo aligoma akisema ana matatizo ya goti katika moja ya miguu yake ndipo mwalimu alilazimika kutoa adhabu ya kuwachapa viboko viwili kila mmoja na aliwapiga wote isipokuwa Chunguku ambaye kama alivyofanya kwenye adhabu za kwanza hii pia alikataa.

Alisema baada ya hapo mwalimu huyo alilazimika kwenda kuwaita wenzake wawili ambao nao walikuwa kwenye mafunzo ya ualimu kwa vitendo shuleni hapo na wakambeba mwanafunzi huyo hadi ofisini kwao ambako huko ndiko walianza kumchapa kwa kumchangia kama inavyooneshwa kwenye kipande cha video kilichosambazwa kwenye mitandao ya kijamii.


Kwa mujibu wa Makalla, walimu waliotenda kitendo hicho walitoroka na hawajulikani walipo. Alisema serikali inaendelea kuwasaka huku walimu wengine wakihojiwa Polisi.