Wednesday, November 2, 2016

VYUO VIKUU 15 MATATANI.


Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Maimuna Tarishi
Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Maimuna Tarishi
Serikali imetoa siku mbili kwa vyuo vikuu 15, kuwasilisha matokeo ya mitihani kwa mwaka wa masomo 2015/2016 ya wanafunzi wanufaika na mikopo wanaoendelea na masomo ili kupangiwa mikopo kwa mwaka wa 2016/2017.
Vyuo hivyo vilivyokuwa viwasilishe matokeo hayo siku 30 kabla ya kufunguliwa, vimepewa siku hizo kuanzia jana, kabla serikali haijachukua hatua zozote.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Maimuna Tarishi alisema hayo jana, alipotembelea ofisi za Bodi ya Mikopo kwa Wanafunzi wa Elimu ya Juu.
Alisema serikali iko katika hatua za mwisho za upangaji na utoaji wa mikopo kwa wanafunzi wanaoendelea na masomo.
Tarishi alisema baadhi ya vyuo vimeshindwa kuwasilisha matokeo ya mitihani kwa wanafunzi wanaoendelea ili wapangiwe mikopo kwa mwaka unaoendelea, kwani utaratibu lazima vyuo kuwasilisha matokeo kuonesha wanafunzi wangapi wana sifa za kuendelea kupewa mikopo.
“Mikopo haiwezi kutolewa tu kwa kila mwanafunzi, hata kama ameamua kuacha masomo, hivyo vyuo vina wajibu wa kuthibitisha kuwa wanafunzi wanaowaleta bado ni wanafunzi sahihi na wanaendelea na masomo,” alisema Katibu Mkuu huyo.
Alivitaja vyuo ambavyo havijawasilisha matokeo hayo kuwa ni Vyuo vya Elimu ya Biashara (CBE) Dar es Salaam, Mwanza na Dodoma, Chuo Kikuu cha Bagamoyo (UOB), Chuo Kikuu cha St. John Kituo cha St Mark Dar es Salaam (SJUTDSM), Chuo cha St. John Tanzania (SJUT) na Chuo Kikuu cha Tumaini Mbeya (TUMAMBEYA).
Vingine ni Chuo cha Maendeleo ya Jamii (CDTI), Chuo cha United African University of Tanzania (UAUT), Chuo Kikuu cha Teofilo Kisanji (TEKU), Chuo Kikuu Cha Kumbukumbu ya Hubert Kairuki (HKMU), Chuo Kikuu cha Mtakatifu Joseph cha Tiba ya Sayansi (STJCAHS), Chuo Kikuu cha Mtakatifu Joseph Kituo cha Makambako na Chuo Kikuu cha Zanzibar (ZU).
Katibu Mkuu huyo pia alitaka vyuo hivyo kuimarisha mifumo yao ya kuandaa na kuwasilisha matokeo ya mitihani kwa wakati na kwa ukamilifu katika siku zijazo ili kuondoa usumbufu. Akizungumzia hatua watakazochukua wasipotimiza agizo hilo, alisema wanawaagiza kutekeleza maagizo hayo kwa siku walizopewa.
Alisema ana uhakika kauli hiyo inawatosha waungwana hao, kutimiza wajibu wao.
Awali vyuo vyote vya elimu ya juu, vilikumbushwa umuhimu wa kuwasilisha matokeo, kabla havijafunguliwa, ikiwemo serikali kufanya mkutano na Makamu Wakuu wa vyuo vyote vya elimu ya juu mkoani Dodoma na kusisitiza umuhimu wa vyuo kuwasilisha matokeo na nyaraka nyingine muhimu, kabla ya vyuo kufunguliwa.
Alisema Serikali ya Awamu ya Tano, imejipanga kikamilifu na imetenga fedha za kutosha na tayari imetoa Sh bilioni 80.89 kwa ajili ya mikopo ya wanafunzi, wanaonufaika na mikopo hiyo kwa robo ya kwanza ya mwaka.
Alisema kati ya kiasi hicho, tayari Sh bilioni 45.2 zimekwishalipwa na kiasi kilichosalia, kitalipwa kwa vyuo baada ya kupokea matokeo kikamilifu. Pia aliwatoa wasiwasi wanafunzi wa mwaka wa kwanza waliokosa mikopo, kupeleka malalamiko katika dirisha maalum la malalamiko, lililofunguliwa na Bodi ya Mikopo kuanzia juzi na serikali ni sikivu, itafanyia kazi.
Katika siku za hivi karibuni, wanafunzi wa elimu ya juu katika vyuo mbalimbali wanaoendelea na masomo, wamekuwa wakilalamika kucheleweshwa kwa mikopo ya elimu ya juu ; huku wanaoanza mwaka wa kwanza, wakilalamikia kukosa mikopo hiyo.
Imeelezwa kuwa baada ya kufanyika uchambuzi, wanafunzi 20,183 wanaoanza mwaka wa kwanza katika vyuo mbalimbali wamepatiwa mikopo; huku wakitarajia kutoa mikopo kwa wanafunzi 93,295 wanaoendelea na masomo.
Katika hatua nyingine, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Ajira, Kazi, Vijana na Walemavu, Jenista Mhagama amesema serikali kwa sasa inaandaa taarifa kuhusu mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu; na ikishakamilika itawasilisha bungeni, kama walivyoomba wabunge.
Alitoa ufafanuzi huo baada ya Mwenyekiti wa Bunge, Najma Giga kujibu mwongozo uliotolewa na Mbunge wa Mwibara, Kange Lugola (CCM) kuomba mwongozo bungeni, akitaka leo serikali ilete taarifa kuhusu mikopo inayotolewa na Bodi ya Mikopo, kwa kile alichoeleza kuwa wanafunzi wengi walioomba mikopo wakiwa na vigezo, hawajapata. Jenista alisema kwa sasa serikali inaandaa taarifa hiyo na ikikamilika, italetwa bungeni kama wabunge walivyoomba.
Akiwasilisha Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na serikali pamoja na mwongozo wa kuandaa mpango na bajeti ya serikali kwa mwaka wa fedha 2017/18, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango alisema Serikali itadhibiti utoaji wa mikopo kwa wanafunzi wa vyuo vikuu, kwa kuhakikisha kuwa wanafunzi waliokidhi vigezo pekee, ndio wananufaika kwa mikopo hiyo.
Awali, Mhagama alisema serikali haifanyi kazi kwa miujiza, bali kwa kutumia mgangilio wa bajeti iliyowekwa na uthibitisho kwamba serikali inafanya kazi kwa mipango, imeweza kutekeleza kutoa elimu bure ikiwa ni utekelezaji wa Ilani ya CCM.
Mhagama alitoa kauli hiyo baada ya Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni na Mbunge wa Hai, Free Mbowe (Chadema) kuuliza swali la nyongeza lililotokana na swali la msingi la Mbunge wa Shinyanga Mjini, Stephen Masele (CCM) kutaka kujua Serikali itaanza kutekeleza lini ahadi ya Sh milioni 50 kwa kila kijiji na mtaa ili kutatua tatizo la ajira na mitaji kwa vijana na akina mama.
Akifafanua zaidi, alisema kamwe serikali haijiendeshi kwa miujiza bali kwa kutumia mipango iliyojiwekea katika bajeti zake.
“Kuthibitisha jambo hili linatekelezeka, Serikali ya CCM kupitia Ilani yake tumeweza kutoa elimu bure, kuwashangaza Watanzania miradi mikubwa mbalimbali imetekelezwa ikiwemo kununua ndege (mbili za Dash 8, Q400 zilizotengenezwa na Bombardier), Ilani inatekelezwa kwa mambo mengi mbalimbali,” alisema akimjibu swali la nyongeza Mbunge wa Hai, Freeman Mbowe (Chadema) kuhusu Sh milioni 50 zilizoahidiwa kwa kila kijiji nchini.
Jenista alisema fedha zote zinazoahidiwa na serikali zikiwemo Sh milioni 50, zitatolewa na Watanzania watazipata.
Imeandikwa na Gloria Tesha, Dodoma na Theopista Nsanzugwanko, Dar.

ARSENAL WAPANDA KWENYE CHATI.

Mesut OzilMesut Ozil alifunga bao la dakika za mwisho na kuwawezesha Arsenal kutoka nyuma 2-0 na kulaza Ludogorets Razgrad ya Bulgaria na kuwafikisha hatua ya mondoano Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya.
Ozil alionekana kutulia alipokimbia langoni, akampiga chenga kipa na mabeki wawili na kisha akatumbukiza mpira kimiani.
Awali, matumaini ya Arsenal kurudia ushindi wao mkubwa wa 6-0 mechi ya kwanza yalizimwa Jonathan Cafu alipowaweka Ludogorets mbele baada ya frikiki ya Wanderson.
Cafu alisaidia ufungaji wa pili alipomzidi ujanja Kieran Gibbs na kumpa mpira Claudiu Keseru aliyefunga na kuwashangaza Arsenal.
Granit Xhaka aliokoa jahazi upande wa Arsenal kwa kombora la kutoka hatua 15 kutoka kwa goli baada ya kupokea krosi kutoka Ozil na kufufua matumaini ya Arsenal kwa bao moja.
Olivier Giroud naye alifunga kwa kichwa kutoka kwa mpira uliotoka kwa Aaron Ramsey na kusawazisha.
Kipa wa Arsenal David Ospina alifanya kazi ya ziada kuokoa mpira mara mbili kutoka kwa Wanderson kabla ya Ozil kufunga.
Arsenal sasa wamefika hatua ya 16 bora na wameendeleza msururu wao wa kutoshindwa hadi mechi 15.
Group A

MATOKEO Kamili: Mechi za Ligi ya Mabingwa Ulaya

KUNDI A
Basel 1-2 Paris Saint Germain
Ludo Razgd 2-3 Arsenal
KUNDI B
Besiktas 1-1 Napoli
Benfica 1-0 Dynamo Kiev
KUNDI C
Bor Monchengladbach 1-1 Celtic
Manchester City 3-1 Barcelona
KUNDI D
Atletico Madrid 2-1 FC Rostov
PSV Eindhoven 1-2 Bayern Munich
Mesut Ozil

WALIOHUSIKA NA KIFO CHA MASHALI WASAKWA.



Wakati mwili wa bondia Thomas Mashali ukitarajiwa kuzikwa leo, watu wanne wanasakwa na polisi wakituhumiwa  kuhusika na kifo chake.
Ndugu wa Mashali, Emmanuel Mashali akiwa nyumbani kwao, Tandale kwa Mtogole, Manispaa ya Kinondoni jijini Dar es Salaam alisema kwamba ndugu yao ataagwa leo saa 7:00 mchana na  kuzikwa jioni kwenye makaburi ya Kinondoni.
“Tunajaribu kuomba kutumia Viwanja vya Leaders Club kufanya shughuli za kuaga, kama itashindika shughuli hiyo itafanyika kwenye Viwanja vya Shule ya Msingi Tandale,” alisema Emmanuel na kuongeza: “Shughuli ya kuaga mwili itaanza saa 7:00 mchana na saa 10:00 jioni tutamuhifadhi ndugu yetu kwenye makaburi ya Kinondoni.”
Akizungumzia kifo  hicho, Emmanuel alisema taarifa za awali walizopata ni kwamba bondia huyo alipigwa na watu kadhaa baada ya kumpigia yowe za mwizi.

MBUNGE AKAMATWA NA BUNDUKI 11.



 Kikosi kazi maalumu kilichoundwa na Serikali kupambana na tatizo sugu la ujangili, kimenasa bunduki 11 ambazo zinasadikiwa kutumika kufanya ujangili na kukamata watu wanne zaidi.
Taarifa zilizopatikana jana zimelidokezea gazeti hili kuwa bunduki hizo zilikamatwa nyumbani kwa mbunge wa CCM (jina tunalihifadhi) ambaye bado anasakwa na kikosi kazi hicho.
Matukio hayo yamekuja siku chache baada ya Rais John Magufuli kutaja jina la mtu anayeitwa Mpemba kuhusika na ujangili kwa muda mrefu wakati alipotembelea ofisi za Wizara ya Maliasili na Utalii na kushuhudia pembe 50 za ndovu zilizokamatwa na watumishi wa wizara hiyo.
Siku hiyo, Rais aliwaambia watu aliowaita “vijana” waendelee na kazi yao ya kukamata wauaji wa tembo, akiwahakikishia kuwa Serikali ipo na kuwataka wasiogope mtu yeyote yule.

LADY JAY DEE KIZIMBANI.

Mahakama ya Wilaya Kinondoni imemtia hatiani mwanamuziki nyota wa kike nchini Judith Wambura (Lady Jay Dee) kwa kutoa maneno ya kashfa dhidi ya Joseph Kusaga na Ruge Mutahaba.
Mahakama hiyo imemuamuru aombe radhi kupitia kwenye chombo cha habari chenye "coverage" pana nchini kote na ikiwezekana duniani.
Katika hati ya madai hayo, mwanamuziki huyo anashtakiwa na viongozi wa Clouds Media Group ambao ni Ruge Mutahaba na Joseph Kusaga kwa kuuchafua uongozi wa kampuni hiyo na viongozi wake kupitia mitandao ya kijamii katika malumbano makali kati ya pande hizo mbili.
Mei 2013, Clouds Media Group na Ruge walimburuza Jay Dee mahakamani kwa kile walichodai kwamba alikuwa akiwatukana kwenye mitandao ya kijamii.

Tuesday, November 1, 2016

FARAJA NYARANDU AHAMASISHA WATANZANIA KUACHA KUMSEMA VIBAYA MISS TANZANIA 2016.

Aliyewahi kuwa Miss Tanzania, Faraja Nyalandu amemkingia kifua mshindi wa mwaka huu Diana Edward akisema hata yeye aliposhinda alizushiwa mambo mengi, lakini anashukuru kwa kuwa yalimjenga.

Katika waraka wake wenye maneno 223 aliouweka kwenye mtandao wa Instagram, mrembo huyo alisema alikaribishwa katika dunia ya umaarufu kwa kashfa lakini kwa msaada wazazi wake alifanikiwa kusimamia malengo yake.

Alimtaka Miss Tanzania afanye anachokiamini na kupuuzia maneno ya watu kwa sababu yanaweza kumtoa katika njia yake.

“Njia ya mafanikio ni ngumu, kwako Miss Tanzania wetu fanya kile unachokiamini, usikubali maneno haya ya watu yakuondoe katika mstari, kwa Watanzania wenzangu tujitahidi kuyaunga mkono yaliyo mazuri, tusibomoe…Tujenge,” alisema.

Akizungumzia ushindi wake, Diana alisema amejipanga kulitumikia vyema hasa kukomesha vitendo vya ukeketaji katika jamii ya Kimasai.


MWANAFUNZI ALIGONGA GARI LA POLISI KWA SABABU YA KUJIPIGA SELFIE.

Mwanafunzi mmoja wa chuo kikuu nchini Marekani aligongesha gari lake kwa lile la polisi, wakati akijipiga picha za selfie huku akiendesha gari.
Miranda Rader mwenye umri wa miaka 19, aligonga gari polisi alipokuwa akimtumia mpenzi wake picha za utupu kupitia kwa mtandao wa Snapchat.
Ajali hiyo iliyotokea eneo la Bryan umbali wa kilomita 160 Kaskazini mwa mji wa Houston, ilisababisha mfuko wa hewa kuchomoka
Mwanafunzi huyo pia alipatikana na chupa ya mvinyo ndani ya gari lake kwa mujibu wa polisi. Hakuna mtu aliyejeruhiwa.
Polisi ambaye gari lake liligongwa alikaribia gari la Bi Rader na kumpata akijaribu kuvaa nguo. Alipoulizwa mbona, alijibu akisema kuwa alikuwa akijipiga picha za selfie za kumtumia mpenzi wake.
Alikamatwa kwa kushukiwa kuendesha gari akiwa mlevi na kuachiliwa kwa dhamana ya dola 2000.