Thursday, September 15, 2016

TRUMP AKATISHWA KUTOA HOTUBA NA MCHUNGAJI BAADA YA KUANZA KUMKASHIFU MGOMBEA MWENZAKE CLINTON.

Mchungaji wa kanisa moja la watu weusi katika jimbo la Michigan, Marekani amemkatisha Donald Trump akihutubia alipoanza kumshutumu mpinzani wake Hillary Clinton.

Mchungaji Faith Green Timmons alimkatisha Trump alipomshutumu mgombea huyo wa chama cha Democratic kuhusu mikataba ya kibiashara.

"Trump nilikualika hapa uje utushukuru kwa juhudi ambazo tumefanya Flint, si kutoa hotuba ya kisiasa" alisema mchungaji huyo wa kanisa la Bethel United Methodist.

Trump aliendelea na kuzungumza kwa kifupi kuhusu kutatua tatizo la maji safi Flint, lakini baadhi ya watu kwenye umati wakaanza kumzomea.

Mwanamke mmoja alisema kwa sauti kwamba mfanyabiashara huyo tajiri alitumia njia za kibaguzi katika kampeni yake.

Mfanyabiashara huyo alimjibu "haiwezekani umekosea, nisingeweza kufanya hivyo".

Mchungaji huyo aliingia tena na kuwashutumu waliokuwa wanamzomea Trump na kusema "yeye ni mgeni katika kanisa langu na inabidi mumuheshimu".

Trump mwishowe alilazimika kukatiza ghafla hotuba yake ambayo ilidumu kwa dakika sita hivi.


MWANAMKE AKAMATWA KWA KUIBA MTOTO MWENYE SIKU 10.

Polisi mkoani Morogoro inamshikilia Anna Luambano (33) ambaye ni mkazi wa Kipawa jijini Dar es salaam kwa tuhuma za wizi wa mtoto Angel Meck mwenye umri wa siku 10 baada ya kumlaghai mama wa mtoto huyo Maimuna Mohammed mkazi wa Chamwino katika manispaa ya Morogoro.

Kamanda wa polisi wa mkoa Ulrich Matei amesema wizi huo ulitokea Septemba 13, saa tano asubuhi katika mtaa wa Kilimahewa manispaa ya Morogoro.

Akielezea mazingira ya wizi huo, Kamanda Matei alisema mtuhumiwa alimdanganya mama wa mtoto huyo wakiwa njiani kutoka kituo cha Afya Mafiga, akimwomba ampe mtoto wake akamwoneshe mume wake kuwa huyo ni mtoto wa mdogo wake, ambaye amejifungua ili awape fedha za hongera kisha wagawane.

Amesema mtuhumiwa huyo baada ya kupewa mtoto alipotea katika mazingira ya kutatanisha.

Mama mtoto baada ya kugundua kuwa ameibiwa alienda kutoa taarifa kituo cha polisi. Ndipo polisi walipoanza kufanya msako kwenye mabasi yote ya abiria yanayosafiri maeneo mbalimbali na kufanikiwa kumkamata mtuhumiwa katika basi la Upendo eneo la Mdaula mkoani Pwani akienda mkoani Dar es salaam.

Mtuhumiwa alikiri na kusema hakuwa na nia mbaya bali alitaka kwenda kumlea huyo mtoto.


LOWASA AMKOSOA RAIS MAGUFULI.

Lowassa

Kiongozi wa upinzani nchini Tanzania Edward Lowasa amemkosoa mpinzani wake rais Magufuli kwa kile alichokitaja ni udikteta nchini humo.

Akizungumza na mwandishi wa BBC nchini Kenya, alisema kuwa alitarajia kwamba Magufuli angeondoa urasimu serikalini lakini kuna mambo mengi hayajakwenda sawa, japokuwa alikataa kutoa mifano alipotakiwa kufanya hivyo.

Lowasa alikuwa katika chama tawala alipokuwa Waziri Mkuu, lakini mwaka uliopita alijiunga na upinzani wa CHADEMA ambapo alishindwa na Rais Magufuli wakati wa uchaguzi.

Magufuli alipewa jina tinga (Bulldozer) anajulikana kufanya maamuzi yanayopendwa tangu achukue madaraka mwaka uliopita, kama vile kufutilia mbali sherehe za Uhuru ili kuhifadhi pesa.


Wednesday, September 14, 2016

VIDEO YA WIMBO WA RARUA WA MALAIKA WAZUA UTATA.

Malaika

Wiki iliyopita video ya wimbo wa Rarua wa mwanamziki Malaika ulitoka huku Hanscana akiwa ni director wa video hiyo.

Taharuki imetokea pale ambapo aliyekuwa mpenzi wa Malaika, kijana Eddy ambaye siku za nyuma alikataza nyimbo hiyo kutoka, kutokana na kulipa gharama zote lakini Malaika akamzingua kwa kumshitaki polisi kuwa alimtishia maisha.

Leo katika kipindi cha XXL kinachorushwa na Clouds Fm, Eddy alisikika kwenye Uheard akisema wimbo huo haukutakiwa kutoka na walikubaliana na Hanscana wasitoe nyimbo hiyo mpaka watakapokubaliana.

Lakini wimbo umetolewa na Eddy katishia kuufunga kwani umetolewa bila makubaliano na yeye ndiye aliyegharamia wimbo mzima.


MHANDISI ASAFIRI KWA KUTUMIA BAJAJI ISIYOTUMIA MAFUTA KUTOKA INDIA MPAKA UINGEREZA.

Mhandisi kutoka India ambaye amekuwa akiendesha bajaji ya kutumia makawi ya jua amewasili Uingereza baada ya safari iliyodumu miezi saba.

6,200 mile (9,978km) umbali wa safari.

Naveen Rabelli ambaye ni mzaliwa wa Australia aliendesha bajaji yake kutoka kwenye feri dover, Uingereza akiwa amechelewa kwa siku tano.

Alitarajia kufika mapema lakini akakwama kwa mda Paris baada ya pasipoti na kipochi chake kupotea.

Lengo lake la kufanya ziara hiyo ilikuwa kuhamasisha watu kutumia magari yanayotumia kawi mbadala kama vile sola na umeme.

Anapanga kuhitimisha safari yake katika kasri la Buckingham, London.

Alianza safari yake Bangalore nchini India kisha akaendea Iran, alipitia Uturuki, Bulgaria, Serbia, Austria, Uswizi, Ujerumani na Ufaransa.


WABUNGE WA UINGEREZA WATAKA BANGI KUHALALISHWA.

Mmea wa bangi.

Kundi moja la wabunge nchini Uingereza limetoa wito wa kuhalalishwa kwa matumizi ya bangi kwa sababu za matibabu nchini humo.

Kundi hilo linalojumuisha wabunge mbalimbali kutoka vyama vya siasa na ambalo limekuwa likitetea mageuzi kuhusu matumizi ya dawa, limesema kuna ushahidi bayana kwamba matumizi ya bangi huwa na manufaa katika kutibu baadhi ya magonjwa ya kiafya, yakiwemo maumivu makali na kutatizwa na wasiwasi.

Wabunge hao wanasema tayari maelfu ya watu huvunja sheria kwa sasa na kutumia bangi kama dawa.

Lakini wizara ya mambo ya ndani nchini humo imesema kufikia sasa hakuna mipango ya kuhalalisha matumizi ya dawa hiyo hatari.

Mmea wa bangi huwa na karibu na kemikali 60.

Wabunge hao wanataka serikali iondoe bangi kutoka kwa kitengo nambari moja hadi kitengo  nambari nne.

Kitengo hicho kina dawa nyingine zikiwemo homoni, vitamin na dawa za kupunguza maumivu.

Hii itawawezesha madaktari kumpendekezea mgonjwa kutumia bangi kama dawa.

Taasisi ya Afya ya Uingereza imetahadharisha kwamba bangi huwa na madhara makubwa kwa mwili, ikiwemo kutatiza uwezo wa mtu kuendesha gari na kudhuru mapafu na afya ya kiakili, kuathiri uwezo wa mtu kuzaa na kuathiri pia watoto ambao hawajazaliwa.

Bangi pia huwa na kiwango cha utegemezi cha 9%, ingawa si cha juu sana kulinganisha na tumbaku 32% na pombe 15%.

Lakini wabunge hao wanasema wametathimini ushahidi kutoka kwa wagonjwa 623 pamoja na kuzungumza na wataalamu kutoka nchi nyingi duniani na wamegundua bangi inaweza kufaa sana kama dawa.

Nchi kumi na moja zimehalalisha kutumia bangi kwa sababu za kiafya.

Majimbo 24 nchini Marekani na pia nchini Canada na Israel wamehalalisha matumizi ya bangi.


MWANARIADHA MLEMAVU KUTOKA NCHINI KENYA AMESHINDA DHAHABU KATIKA MASHINDANO YA PARALIMPIKI.

Mwanariadha mlemavu kutoka nchini Kenya Samwel Mushai Kimani ameshindia Kenya dhahabu nyingine baada ya kuibuka mshindi wa mbio za wanaume mita 1,500 kitengo T11 Paralimpiki.

Kimani aliandikisha muda wa 4:03,25 muda bora zaidi msimu huu.

Mbrazil Odair Santos alimaliza wa pili.

Mbio hizo hata hivyo hazikuwa za kasi kama za kitengo T13 ambapo wanariadha wanne waliomaliza wa kwanza waliandikisha muda bora kushinda wa mshindi wa mbio za Olimpiki mita 1,500.

Kimani alikuwa ameishindia Kenya dhahabu ya kwanza katika michezo ya Olimpiki ya walemavu wa Rio 2016 kwa ushindi katika mbio za mita 5,000 kitengo T11.

Kenya ilishinda dhahabu mbili Paralimpiki za London na kubeba medali sita kwa ujumla.