Monday, October 31, 2016

BREAKING NEWS:BONDIA THOMAS MASHALI AMEFARIKI.

thomas-2
Bondia maarufu wa ngumi za kulipwa nchini, Thomas Mashali amefariki dunia usiku wa kuamkia leo October 31 2016 maeneo ya Kimara DSM, Taarifa zinadai kuwa alishambuliwa na wananchi baada ya madai ya kuitiwa mwizi.
Taarifa kutoka kwa Promota wake, Siraji Kaike amesema watu aliokuwa anagombana nao walimwitia mwizi na wakawa wamemshambulia na baadaye wakawa wamemtupa na bodaboda waliokuwa wanamjua Thomas Mashali walimuokota na kumpeleka hospitali ambapo baadaye zilitolewa taarifa kuwa amefariki.

BONDIA MTANZANIA AMLAZA BONDIA MWENZAKE SAKAFUNI.

Bondia chipukizi kutoka Tanzania Abdallah Pazi Dulla Mbabe alimrambisha sakafu mwenzake kutoka China Zheng Chengbo katika pigano kali lililofanyika usiku wa Ijumaa katika ukumbi wa Diamond Jubilee mjini Dar es Salaam.

Ngumi nzito iliorushwa na Dulla ilimwangusha mpinzani wake na kumfanya kushindwa kuendelea na pigano hilo la uzani wa Light Heavy.

Pazi alianza pigano hilo kwa kasi na kufanikiwa kumwangusha bondia huyo wa China kwa sekunde kadhaa.

Hatahivyo Chengbo aliamka na kuendelea na pigano.

Bondia huyo wa Tanzania alifanikiwa kumweka Chengbo katika kona na kumrushia makonde makali akimwacha akitokwa na damu chungu nzima katika pua.

Ni wakati huohuo ambapo bondia huyo alishindwa kunyanyuka kutoka sakafuni ndiposa refa akamaliza pigano hilo na kumpatia ushindi wa Knock-out Dulla.

Bondia huyo sasa ameshinda mapigano 14 ,13 yakiwa katika njia ya Knockout na kushindwa mara tatu.


MAGUFULI KUZINDUA BARABARA NAIROBI.

Rais wa Tanzania John Magufuli anatarajiwa kuanza ziara yake ya kikazi katika nchi jirani ya Kenya leo.

Kwenye ziara hiyo ya siku mbili, Rais Magufuli anatarajiwa kufanya mazungumzo na mwenyeji wake na pia kuzindua barabara mchepuko ya Southern By-pass iliyopo Jijini Nairobi.

Barabara hiyo, ambayo inaunganisha maeneo mbalimbali ya jiji la Nairobi kwa barabara za juu na chini, ni moja kati ya miradi mbalimbali ya ujenzi wa barabara ambayo imekuwa ikitekelezwa na serikali ya Kenya kupunguza msongamano wa magari katika jiji hilo kuu.

Rais Magufuli anatarajiwa kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta Jijini Nairobi majira ya saa nne asubuhi na baadaye kupokelewa rasmi na mwenyeji wake Rais Kenyatta katika Ikulu ya Nairobi ambako viongozi hao watafanya mazungumzo rasmi.

"Katika ziara hii Rais Magufuli anatarajiwa kutembelea kiwanda cha maziwa cha Eldoville kilichopo Karen Jijini Nairobi, na pia anatarajiwa kuzindua barabara mchepuko ya Southern By-pass iliyopo Jijini Nairobi," taarifa kutoka ikulu ya Tanzania imesema.

Ziara hiyo ya Rais Magufuli inajiri wakati ambao anakaribia kumaliza mwaka mmoja madarakani.

Katika kipindi hicho, hajakuwa akizuru sana mataifa ya nje na uhusiano kati ya serikali yake na serikali ya Rais Kenyatta umeonekana kuwa 'baridi kiasi'.

Tangu aingie mamlakani mwezi Novemba mwaka jana, amezuru tu Rwanda na Uganda.

Kabla ya kuchaguliwa kuwa Rais, Dkt Magufuli alikuwa amehudumu serikalini kama waziri wa ujenzi.

Taarifa kutoka ikulu ya Tanzania inasema ziara yake imetokana na mwaliko wa Rais Kenyatta.

Kando na kutaka kuimarisha uhusiano baina ya nchi hizo mbili, wachanganuzi wanasema huenda Rais Kenyatta akaitumia kumpendekeza waziri wa mambo ya nje wa Kenya Bi Amina Mohammed ambaye anawania wadhifa wa mwenyekiti wa tume ya Umoja wa Afrika (AU).

Rais Uhuru Kenyatta atamkaribisha mgeni wake jijini Nairobi, baada ya Kenyatta kukamilisha ziara ya siku mbili huko Khartoum, alipokutana na Rais wa Sudan Omar Al- Bashir.


MISS TANZANIA WA SASA NI WA TOFAUTI.

Miss Tanzania 2016, Diana Edward ametangaza vipaumbe vyake  kuwa ni kupinga ukeketaji, mila potofu na ndoa za utotoni hasa kwenye jamii za Kimasai na nyinginezo.

Mrembo huyo wa Kinondoni, Diana alitwaa taji la Miss Tanzania 2016, usiku wa kuamkia Jumapili kwenye Ukumbi wa Rock City Mall jijini Mwanza.

Diana alinyakua taji hilo na kujitwalia gari aina ya Toyota IST na kitita cha Sh4 milioni baada ya kuwashinda warembo wenzake 29 kutoka mikoa mbalimbali nchini waliokuwa wakichuana kuwania taji hilo.

Akizungumza baada ya kutwaa taji hilo, Diana alisema haikuwa kazi rahisi kwani ushindani ulikuwa mkali ni mapenzi ya Mungu kumpa nafasi hiyo.


MCHUNGAJI RWAKATALE AZUILIWA KUWALIPIA FAINI WAFUNGWA.

GETRUDE RWAKATALE

Serikali imesitisha shughuli iliyokuwa ikiendeshwa na Mchungaji Getrude Lwakatare ya kuwalipia faini wafungwa waliopo magerezani hadi hapo utaratibu mwingine utakapotolewa.

Mpango huo unaofanywa na Lwakatare kwa kushirikiana na Mwenyekiti wa Taifa wa Bodi ya Parole, Augustine Mrema tayari umewezesha wafungwa 78 kutoka magerezani baada ya kuwalipia faini inayofikia Sh25 milioni.

Mkuu wa Magereza Mkoa wa Dodoma, Antonio Kilumbi alisema amepata maelekezo ya kusitishwa kwa mpango huo kutoka ngazi ya juu za jeshi hilo. 

Alisema wananchi wengine bado wanaweza kuwalipia faini hiyo ndugu zao.

Mrema alisema jana kuwa mpango huo ulilenga kupunguza msongamano magerezani na kuipunguzia Serikali gharama za kuwahudumia wafungwa.


APPLE YAONGEZA BEI YA LAPTOP NA KOMPYUTA ZAKE.

Kampuni ya teknolojia ya Apple imeongeza bei ya laptopu na kompyuta zake nchini Uingereza kwa pauni 100.

Siku ya Alhamisi ,kampuni hiyo ilizindua laptopu za Macbook Pro zikiwa na bei sawa na ile ya Marekani.

Lakini kampuni hiyo pia iliongeza bei ya tarakilishi zake ,ikiwemo ile ya Mac Pro ilio na miaka mitatu kwa pauni 100.

Mchanganuzi mmoja alisema kuwa wateja wanafaa kutarajia kuongezwa kwa bei hizo zaidi.


Sunday, October 30, 2016

MSAJILI WA MAHAKAMA AJITOA KATIKA KESI YA BABU TALE.

BABU TALE.

MSAJILI wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Projest Kahyoza amejitoa katika shauri la Mkurugenzi wa Kampuni ya Tiptop Connections, Hamis Taletale ‘Babu Tale’ anayetakiwa aieleze Mahakama ni kwa nini asifungwe jela baada ya kushindwa kulipa Sh milioni 250.

Babu Tale ambaye ni Meneja wa mwanamuziki wa kizazi kipya, Nasib Abdul‘ Diamond’, anatakiwa kujieleza kutokana na kushindwa kutii hukumu ya Mahakama iliyomtaka amlipe Mhadhiri wa Dini ya Kiislamu, Shehe Hashimu Mbonde fedha hizo baada ya kuuza kanda za mahubiri yake bila ridhaa yake.

Msajili Kahyoza alijitoa katika shauri hilo baada ya Shehe Mbonde kuandika barua kumtaka ajitoe kwa sababu hana imani naye.

Akiahirisha kesi hiyo, Msajili Kahyoza alisema, anajitoa kwa sababu kuna barua imemfikia kutaka ajiondoe katika shauri hilo, lakini aliongeza kuwa aliyeandika barua hiyo aelezwe ukweli kuhusu yeye kukutana na wakili wa wadaiwa kabla ya kesi kutajwa.

Katika barua hiyo, Shehe Mbonde ameomba msajili ajitoe kwa sababu hajaridhishwa na jinsi anavyoshughulikia shauri hilo tangu alipokee, pia kesi inavyoendelea anahisi haki aliyopewa na mahakama hiyo haitatendeka au itacheleweshwa.

Aliorodhesha baadhi ya mienendo inayomtia mashaka ikiwemo kesi hiyo kuahirishwa zaidi ya mara nane kwa sababu tofauti tofauti ikiwemo ya mawakili wa wadaiwa kutokufika mahakamani, pamoja na sababu nyingine bila kuwataka wahusika kueleza jinsi watakavyolipa fedha hizo.

Katika barua hiyo, Shehe Mbonde ameeleza kutiwa shaka na ukaribu kati ya msajili na wakili wa wadaiwa kwa kuwa amekuwa akishuhudia wakili huyo akiingia katika Ofisi ya Msajili kabla kesi haijatajwa mahakamani, jambo linalomfanya ahisi wanapanga jinsi kesi inavyokwenda.

Msajili Kahyoza aliahirisha shauri hilo hadi Novemba 8, mwaka huu, kwa ajili ya kutajwa na kupangiwa Msajili mwingine wa kusikiliza.