Sunday, August 28, 2016

ASKARI AFYATUA RISASI WODINI.

Kamanda wa polisi George Kyando

Kitendo cha askari huyo kilizua taharuki kubwa kwenye wodi namba 9 ya wanawake na watoto, ambapo wakina mama walipiga mayowe kwa hofu huku wakikimbia na kujificha kwenye chumba cha muuguzi wa zamu wakiwaacha watoto zao vitandani.

Kamanda wa polisi mkoa wa Rukwa George Kyando, alithibitisha kutokea kwa tukio na kueleza kuwa lilitokea jana alfajiri.

"Chanzo ni ulevi wa kupindukia, tulimpima kipimo kikaonesha kiwango cha ulevi kilikuwa juu kupita kiasi alama zikiwa 300 huku kiwango cha kawaida cha kipimo ni alama kati ya 70 na 40....katika tukio hilo hakuna aliyejeruhiwa na bunduki yake ilikuwa na risasi 10", alisema.

Kamanda Kyando alisema siku ya tukio askari huyo akiwa na wenzake alikuwa katika lindo akilinda makazi ya Kamanda wa magereza wa mkoa, lakini alitoroka lindo na kwenda hospitalini wodi namba 9, ambako mkewe alikuwa akimuuguza mwanawe aliyekuwa amelazwa hapo kwa matibabu.

Mke wa mtuhumiwa huyo Theresia Kalonga ambaye ni askari magereza, alikuwa amelazwa na mtoto wao wa kike mwenye umri wa mwaka mmoja na miezi kumi.

"Mtuhumiwa huyo tunamshikiria huku taratibu  za kumkabidhi kwa kamanda wa magereza mkoa wa Rukwa ili aweze kushtakiwa kwa taratibu za jeshi lao, kabla ya kufikishwa kwenye mahakama za kiraia, zinaendelea", alisema kamanda Kyando.

Akizungumza hospitalini hapo, Mganga mkuu wa mkoa wa Rukwa Dk.John Gurisha alisema, askari huyo baada ya kuingia wodini aliweka siraha yake chini, akafunua chandarua na kuanza kuzungumza na mwanawe, kisha katoka nje kafyatua risasi hewani na kutoboa paa.

"Mtuhumiwa huyo alizua kizaazaa kwani askari wetu waliokuwa lindo hapa hospitalini walilazimika kukimbia ili kuokoa maisha yao baada ya kusikia mlio huo wa risasi na kumuona askari huyo akielekea walipokuwa wamekaa", alisema na kuongeza kuwa askari huyo aliletwa wodini hapo na mwendesha bodaboda ingawa hakuna mtu yoyote aliyejeruhiwa, lakini alisababisha taharuki kubwa wodini.

"Askari wa kikosi cha kutuliza ghasia FFU waliwahi kufika hospitalini hapo na kumtia nguvuni na bunduki yake ilipokaguliwa ilikutwa na risasi kumi" alisema.

Muuguzi wa zamu wodini humo, Rose Katabi, alisema askari huyo alipofyatua risasi akina mama wodini humo walianza kupiga mayowe ya kuomba msaada huku wakikimbia na kuwaacha watoto wao vitandani na kuvamia chumba cha muuguzi ili kusalimisha maisha yao.

Waliingia walinzi wetu wawili wodini ndipo akaanza kusema atarudi tena, akatoka nje akiwa katikati ya mlango wa wodini alikoki bunduki yake na kufyatua risasi hewani kisha akaondoka na kutokomea gizani" alisema muuguzi.


No comments: