Wednesday, September 7, 2016

AFIKISHWA MAHAKAMANI KWA KUMTUSI MAGUFULI.

Mfanyabiashara Leonard Materu (31) amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu mkazi Kisutu akikabiliwa na mashtaka ya kutuma ujumbe wa kumtishia Rais John Pombe Magufuli kwenye mtandao wa Whatsapp.

Materu ambaye ni mkazi wa Moshi bar kwa diwani, alifikishwa mahakamani hapo na kusomewa mashitaka yake na Wakili wa Serikali, Diana Lukondo mbele ya hakimu mkazi Magreth Bankika.

Akisoma mashtaka wakili Diana alidai mshtakiwa huyo amefunguliwa kesi hiyo kwa kuchapisha taarifa za uongo kwenye mtandao wa Whatsapp chini ya sheria ya mtandao ya mwaka 2015.

Ilidaiwa kuwa Julai 17 mwaka huu jijini Dar es salaam Materu aliandika ujumbe wenye lengo la kudanganya umma kupitia Whatsapp ukisomeka; Magu ajiandae tunaenda kupindua mpaka Ikulu.

Inadaiwa kuwa maneno hayo yalikuwa na lengo la kumtishia Rais Magufuli. Baada ya kusomewa mashtaka, mshitakiwa alikana kosa hilo na upande wa Jamhuri ulidai kuwa upelelezi wa kesi haujakamilika na kuombwa tarehe nyingine kutajwa.

Mshitakiwa aliachiwa kwa dhamana ya kutimiza masharti ya dhamana ya kuwa na wadhamini wawili ambao kila mmoja alisaini hati ya sh. Milioni 5. Kesi itatajwa tena Septemba 20 mwaka huu.


No comments: