Wednesday, September 7, 2016

WANAFUNZI WA DARASA LA SABA WAANZA MITIHANI LEO.

Dk. Charles Msonde

Watahiniwa 795,761 wanatarajia kufanya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi (PSLE) unaofanyika leo na kesho nchini kote.

Akizungumza Dar es salaam jana katibu mtendaji wa Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA), Dk. Charles Msonde alisema wanafunzi 372,883 ambao ni sawa na asilimia 46.86 ni wavulana na 422,878 ni wasichana sawa na asilimia 53.14.

Mwaka 2015 watahiniwa waliosajiliwa kufanya mtihani walikuwa 775,729 huku 763,602 ndio waliofanya mtihani huo na wanafunzi 518,034 walifaulu.

Msonde alisema watahiniwa 765,097 watafanya mtihani kwa lugha ya kiswahili na watahiniwa 30,664 watafanya mtihani kwa lugha ya kiingereza ambayo wamekuwa wakiitumia wakati wa kufundishwa. Masomo yatakayotahiniwa ni Kiswahili, Sayansi, Hisabati na Maarifa.

Amesema watahiniwa wasioona waliosajiliwa kufanya mtihani ni 95 wakiwemo wavulana 57 na wasichana 38 wakati wale wenye huoni hafifu wanaohitaji maandishi makubwa ni 810 ambao kati yao wavulana ni 402 na wasichana 408.

"Wasimamizi wanatakiwa kusimamia kwa umakini na uadilifu wa hali ya juu. Nawaasa kujiepusha na vitendo vya udanganyifu kwani Baraza litachukua hatua kali kwa yeyote yule atakayebainika kukiuka taratibu za uendeshaji wa mitihani ya Taifa" alisema Msonde.


No comments: