Wednesday, September 7, 2016

MWANAMKE AKAMATWA AKIUZA MABINTI.

Jeshi la polisi katika mkoa wa Mara linamshikiria Juritha Lucas (60) mkazi wa kijiji cha Masinki Wilaya ya Serengeti mkoani humo, kwa tuhuma ya kufanya biashara haramu ya binadamu kinyume cha sheria.

Kamanda wa polisi mkoani Mara, kamishina msaidizi mwandamizi wa Polisi Ramadhani Ng'azi alisema mwanamke huyo alikamatwa na polisi akiwa na mabinti watano wenye umri kati ya miaka 15 na 23 alokuwa anataka kuwauza.

Kamanda Ng'azi alisema mabinti hao ni wakazi wa kijiji cha Muruvyagiza, Wilaya ya Ngara mkoani Kagera, ambako ndiko mwanamke huyo aliwatoa na kuwasafirisha hadi katika kijiji cha Masinki Wilayani Serengeti, kwa nia ya kuwauza kwa kuwaozesha kwa wanaume kwa bei kati ya 150,000 hadi 300,000 kila mmoja kulingana na umri, uzuri na tabia ya binti husika.

Polisi walipata taarifa kutoka kwa wasamalia wema kuhusu biashara hiyo, waliweka mtego na ndipo Septemba 4 mwaka huu walimkamata mwanamke huyo na kumhoji na akakiri kuwachukua mabinti hao kutoka mkoani Kagera kwa ajili ya kuwauza.

Jitihada zinafanyika ili kuwasiliana na wazazi wa mabinti hao ili kuwachukua.

Kamanda Ng'azi hakuwataja majina kwa ajili ya usalama, lakini walisema wanaendelea na uchunguzi wa kina na kuwa baada ya upelelezi kukamilika watamfikisha mahakamani kujibu tuhuma ya kufanya biashara ya binadamu kinyume cha sheria.


No comments: