10 WAPOTEZA MAISHA KWENYE AJALI LINDI.
Watu 10 wamekufa na wengine 44 kujeruhiwa katika ajali ya basi la Kampuni ya Barcelona lililokuwa likitokea Dar es Salaam kwenda Newala mkoani Mtwara jana.
Ajali hiyo ni ya jana saa 5 asubuhi katika kijiji cha Miteja wilayani Kilwa mkoani Lindi, umbali wa kilometa 30 kutoka mkoa wa Pwani na miongoni mwa waliopoteza maisha wamo watoto wadogo watatu.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Lindi, Renata Mzinga akizungumza jana, alisema uchunguzi wa awali unaonesha kuwa chanzo cha ajali ni mwendo kasi wa dereva ambaye bado wameshindwa kumhoji kwa kuwa ni miongoni mwa majeruhi na mpaka jana jioni alikuwa amepoteza fahamu. “Ni kweli ajali imetokea asubuhi saa tano leo (jana), dereva alikuwa katika mwendo kasi, basi likapasuka tairi la mbele, likapinduka. Majeruhi wapo 44 na waliokufa ni 10, wanawake sita na mwanamume mmoja, mtoto wa kike mmoja na wakiume wawili,” alisema Kamanda Mzinga.
Kamanda Mzinga alilitaja basi hilo kuwa ni lenye namba za usajili T110 CUU Youtong, mali ya Kampuni ya Barcelona.
No comments:
Post a Comment