Rais John Magufuli jana aliongoza mamia ya wakazi wa Jiji la Dar es Salaam katika kuaga mwili wa aliyekuwa Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Dk Didas Massaburi aliyefariki Alhamisi iliyopita kwa ugonjwa wa ini.
Dk Magufuli aliwaongoza waombolezaji kutoa heshima za mwisho kwa mwili wa Dk Massaburi (56) kwenye Viwanja vya Karimjee, Dar es Salaam, na alipopewa nafasi ya kuzungumza, alisisitiza familia za marehemu kuishi kwa kushikamana.
“Nawaombeni familia mkashikamane, shetani hujitokeza wakati wa msiba, watoto mumtangulize Mungu, baba aliwapenda wote na hakuwabagua, watoto mkishikamana na mama zenu pia watashikamana. Naomba mtoto mkubwa ukawe nguzo ya familia ili pawe na umoja na Mungu atawasimamia,” alisema Dk Magufuli ambaye alisema anachofahamu marehemu ameacha wake wanne hadi watano na watoto zaidi ya 20.
Akisoma wasifu, kaka wa marehemu, Machabe Massaburi alisema Didas alizaliwa mwaka 1960 Serengeti mkoani Mara akiwa mtoto wa 10 katika familia ya John Massaburi.
Alisema Dk Massaburi amewahi kuwa Diwani wa Kata ya Kivukoni na Meya wa Jiji la Dar es Salaam kuanzia 2010 hadi 2015 na pia Mwenyekiti wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT), Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki na hadi mauti yanamfika alikuwa Mkurugenzi na Mwenyekiti wa Chuo chake cha ugavi IPS kilichopo Chanika.
Alisema marehemu ameacha wajane, watoto, wajukuu kadhaa na kwamba alifunga ndoa na Janeth Massaburi ambaye ni Mbunge wa zamani wa Viti Maalumu.
Dk Magufuli alisema alimfahamu Dk Massaburi kama mpiganaji wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na mengi aliyafanya wakati akiwa Meya wa Jiji la Dar es Salaam na akaongeza kuwa historia yake haiwezi kufutika katika siasa za Tanzania.
Tukio hilo la kuaga lilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa kitaifa na kutoa heshima za mwisho akiwemo Rais mstaafu Jakaya Kikwete na aliyewahi kuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa.
Viongozi wengine ni Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi, Makamu wa Rais mstaafu wa Awamu ya Nne, Dk Mohamed Gharib Bilal, Mama Salma Kikwete, viongozi wa mkoa wa Dar es Salaam, mawaziri mbalimbali, wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano na wabunge wa Bunge la Afrika Mashariki.
Akizungumza kwa niaba ya Bodi ya Wadhamini wa Jumuiya ya Wazazi Taifa, Dk Charles Tizeba alisema wamepoteza rafiki, ndugu na mtu waliyemtegemea zaidi katika uendeshaji wa jumuiya hiyo.
Alitoa mwito kwa familia kuwa kifo hicho, kisiwe chanzo cha ugomvi na mifarakano na kwamba waimarishe umoja.
Msemaji wa Familia, Otieno Igogo alisema kifo hicho ni pigo kubwa na kimekuja katika wakati mgumu kwa kuwa Dk Massaburi amefariki dunia wiki moja na kaka yake, na hakuweza kulifahamu hilo kwa kuwa alikuwa taabani.
Alisema aliacha wosia wa maneno kuwa pindi akifariki, azikwe katika mji wake ulioko Chanika, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam, na kwamba zisifuatwe mila za kabila la Wajaluo kuwa hawazikwi ugenini.
Baada ya kuaga mwili wa marehemu, ulipelekwa katika mji wake eneo la Chanika kwa ajili ya maziko kama alivyowausia mwanasiasa huyo.
No comments:
Post a Comment