Monday, October 31, 2016

WANAOSOMEA CHINI YA MWEMBE WAONGOZA KIMKOA.

Shule ya msingi Kashifa katika wilaya ya Tanganyika mkoani Katavi licha ya kukabiliwa na uhaba wa madarasa na walimu, imeshika nafasi ya kwanza kiwilaya na kimkoa katika matokeo ya darasa la saba mwaka 2016.
Katika matokeo ya mwaka 2015 shule hiyo, ilishika nafasi ya pili kiwilaya na nafasi ya 18 kimkoa.
Shule hiyo yenye wanafunzi 600 ipo katika kata ya Ikola, mwambao mwa Ziwa Tanganyika.
Kwa miaka mitano mfululizo, wanafunzi wake wanasomea chini ya miti kutokana na kuwa na vyumba viwili vya madarasa na walimu saba tu.
Matokeo hayo yaliyotangazwa na Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA) hivi karibuni, yamebainisha kuwa shule hiyo imeshika nafasi ya kwanza kiwilaya kati ya shule 31 na nafasi ya kwanza kimkoa kati ya shule 92.
Shule hiyo imeshika nafasi ya 176 kitaifa kati ya shule 8,241 zilizofanya mtihani huo.
Ufaulu huo unaonesha kuwa wanafunzi 14 wakiwemo wasichana sita na wavulana wanane wamepata alama B katika somo la Kiingereza.
Katika Hisabati wanafunzi watatu wamepata alama A na 11 wamepata alama B.
Somo la Sayansi wanafunzi wanane wamepata alama A, sita wamepata alama B.
Diwani wa Kata ya Ikola, Philemon Moro amekiri kuwa shule hiyo inakabiliwa na uhaba wa vyumba vya madarasa na walimu wanafundisha chini ya miembe.

No comments: