Wakazi wa kata ya Kipawa jijini Dar es Salaam wameingiwa na hofu baada ya kuibuka kijana anayejiita ‘Rambo mkata mapanga’ anayedaiwa kufanya uhalifu kwa kujeruhi watu kwa kuwakata mapanga kisha kuwapora fedha na mali zao.
Kijana huyo ambaye jina lake halisi ni Abdul Chata ameibuka ikiwa ni wiki kadhaa zimepita tangu kuibuka kwa sakata la ‘Scorpion’ aliyeshtakiwa kwa tuhuma za uporaji na kujeruhi ikiwamo kutoboa macho.
Miongoni mwa watu waliovamiwa, kukatwa mapanga na kuporwa na anayedaiwa kuwa Rambo mkata mapanga ni walimu watatu wa Shule ya Msingi Mogo, iliyopo kata ya Kipawa.
Wakizungumza na Mwananchi kwa nyakati tofauti, wakazi wa eneo hilo walisema tangu kuibuka kwa mkata mapanga wiki mbili zilizopita, hali ya amani ya eneo hilo imekuwa mbaya kiasi cha kushindwa kutembea usiku kuanzia saa moja.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Karakata, Kata ya Kipawa Andrew Olutu alisema hadi sasa ofisi yake imethibitisha zaidi ya matukio manne ya watu kuporwa kisha kujeruhiwa kwa mapanga.
“Ni mtu hatari na amewapa hofu kubwa wananchi kwa sababu hawezi kupora kitu chochote bila kukukata mapanga, tumekumbwa na taharuki,” alisema Olutu.
Alisema kijana huyo hutembea na mapanga mawili ambayo huyaficha mgongoni na kwamba huwa haijalishi muda gani anaweza kufanya tukio japo, matukio mengi yamefanyika usiku.
Akisimulia zaidi, mwenyekiti huyo alisema tukio jingine lilitokea usiku wa kuamkia Novemba 3, ambapo kijana huyo aliteka bodaboda kisha kumjeruhi dereva kwa panga usoni akimlazimisha ampakie na kumpeleka eneo analotaka. “Inavyoonekana kulikuwa na mvutano baina ya Rambo na dereva wa bodaboda, kwa sababu tulikuwa tunalinda sungusungu tukasikia kelele na kwenda haraka na kumkuta bodaboda akivuja damu. Alikuwa amecharangwa mapanga usoni,” alisema.
Hata hivyo, alisema hawakufanikiwa kumkamata ‘Rambo’ ambaye alikimbia baada ya kuona sungusungu lakini walitoa taarifa za tukio hilo polisi na kumpeleka majeruhi hospitali.
Olutu alisema kutokana na hali kuwa mbaya zaidi, wamelazimika kuunda vikosi vya sungusungu viwili vikiongozwa na kamati ya ulinzi na usalama ya mtaa ili kuwanusuru watu wanaovamiwa.
Baadhi ya wananchi walisema kutokana na hali hiyo wanalazimika kurejea majumbani mapema ili kukwepa mapanga ya Rambo anayeonekana kuwa tishio.
Mkazi wa Mtaa wa Mkarakata, Sam Aidan alisema alinusurika kucharangwa mapanga ya ‘Rambo’ mwishoni mwa wiki iliyopita na kilichomuokoa siku hiyo ni gari lililotokea mbele yao.
“Ilikuwa saa mbili maeneo ya mji mpya nikakutana na ‘Rambo’, nashukuru Mungu muda huo huo lilitokezea gari akakimbia na kuniacha salama. Tangu hapo ni bora nilale huko huko au nikodi teksi ili nirejee nyumbani, kama nikiona giza limeingia,” alisema.
Aliliomba jeshi la Polisi lisaidie kumkamata mhalifu huyo ili wapate amani.
Diwani wa Kata ya Kipawa, Kennedy Simon alisema kijana huyo alianza kufanya matukio ya uhalifu mwaka jana akiwajeruhi wananchi na kuwapora mali zao.
Alidai hali hiyo iliwafanya kumvizia siku moja na kumkamata kisha kumpiga kabla hajaokolewa na polisi.
Simon alisema alifikishwa kituoni, kisha mahakamani ambako alihukumiwa kifungo jela.
“Wiki mbili zilizopita tumeshangaa amerejea mtaani kwa kasi kubwa, safari hii anaitwa ‘Rambo mkata mapanga’ na ukikutana naye, ni bora ujaliwe kutimua mbio kwa sababu hawezi kukuibia bila kukuachia alama ya panga,” alisema.
Alisema taarifa za matukio hayo zimeripotiwa polisi na wanaendelea kumtafuta japo hadi sasa hajakamatwa.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Salum Hamduni alithibitisha kuwapo kwa kijana huyo anayejiita ‘Rambo mkata mapanga’ na kusema tukio linalofahamika hadi sasa ni lile la uvamizi wa shule.
Aliwataka wananchi kusaidia kutoa taarifa za eneo analopatikana mtuhumiwa huyo ili wamkamate.
“Taarifa za ‘Rambo mkata mapanga’ ninazo, tumeshaweka mitego mbalimbali ili kumkamata na niwasihi wananchi wakimuona tu watoe taarifa ili adhibitiwe,” alisema.
Tukio shuleni
Wanafunzi wa Shule ya Msingi ya Mobo, jijini Dar es Salaam walisema wanasoma kwa hofu tangu walimu wao walipovamiwa, kuporwa na kuibiwa.
“Alikuja kama saa 10:00 jioni, akaenda moja kwa moja kwenye eneo walikokuwa walimu akawaumiza na kuwapokonya vitu vyao zikiwamo simu, tunaogopa kwa sababu anaweza kuja tena,” alisema.
Mwalimu mkuu wa shule hiyo, Magreth Fredrick alithibitisha kutokea kwa tukio la kujeruhiwa walimu watatu na kwamba taarifa zaidi zimefikishwa kwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala.
No comments:
Post a Comment