Mkurugenzi wa Shirika la Habari Tanzania (TBC), Ayub Rioba amesema anatarajia kuanza kurudia kuonesha tena tamthiliya ya Jumba la Dhahabu iliyopata umaarufu mkubwa chini ya Kundi la Fukuto Arts.
Akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa TBC maeneo ya Mikocheni, alisema wameamua kuirudisha tena tamthiliya hiyo kutokana na maombi ya watazamaji wengi.
Alisema mchezo huo ambao unatarajiwa kuanza kuoneshwa wiki ijayo, ambao utakuwa ukioneshwa mara tano kwa wiki ili kuwapa nafasi watazamaji ambao kipindi cha nyuma hawakubahatika kuuona.
Rioba pia alizindua muswada mpya wa tamthiliya ya Ukurasa Uliofungwa ‘Closed Chapter’ ambayo, inatarajiwa kuoneshwa katika kituo hicho baada ya kufanyika usaili.
Kiongozi na mtunzi wa filamu ya Jumba la Dhahabu na Kurasa Uliofungwa ‘Closed Chapter’, Tuesday Kiangala, alisema amekubali kuirudisha tamthiliya hiyo kwakuwa alikuwa akiulizwa maswali mengi juu ya tamthiliya hiyo.
“Jumba la Dhahabu inarudi na sasa mashabiki watapata muda mwingi wa kuiangalia, kwa wale ambao waliitazama na ambao hawakupata nafasi ya kuitazama,” alisema.
Katika tamthiliya ya Jumba la Dhahabu kuna waigizaji waliofanya vizuri kama, Mzee Chilo, Joan, Badboy, Tuesday Kiangala, Capto Rado, Niva na wengine.
No comments:
Post a Comment