Mke wa Rais, Mama Janeth Magufuli aliyekuwa amelazwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), ameruhusiwa na kurejea nyumbani leo (Ijumaa), baada ya afya yake kuimarika.
Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu Gerson Msigwa imesema kuwa kabla ya kuondoka katika wodi ya Sewahaji alikokuwa amelazwa Mama Janeth Magufuli amewashukuru madaktari na wauguzi wa hospitali hiyo kwa matibabu mazuri aliyoyapata na pia amewashukuru Watanzania wote kwa kumuombea afya njema.
"Namshukuru sana Mungu kwamba afya yangu imeimarika, pia napenda kuwashukuru madaktari na wauguzi, nimepata huduma nzuri sana maana siku nilipoletwa hapa nilikuwa sina fahamu na hali yangu ilikuwa mbaya lakini mmenipigania na leo narudi nyumbani nikiwa na afya imara.
"Naomba pia niwashukuru Watanzania wote kwa kuniombea, nawahakikishie kuwa sasa nipo vizuri na madaktari wameniruhusu nirudi nyumbani ambako nitamalizia matibabu yangu" amesema Mama Janeth.
Mama Janeth alilazwa MNH tangu juzi baada ya kuugua ghafla na kupoteza fahamu.
No comments:
Post a Comment