Bei ya unga wa sembe huenda ikapanda kutoka Sh1,200 hadi Sh2,000 kwa kilo kwenye maduka ya rejareja baada ya bei ya mahindi kupanda mara mbili ya bei ya awali.
Kwa sasa mahindi yanauzwa Sh760 kwa kilo kutoka Sh350 za awali.
Mwenyekiti wa Umoja wa Wamiliki na Wazalishaji sembe na dona (Uwawase), Oscar Munisi alisema jana kuwa kupanda kwa bei ya mahindi kumetokana na kuadimika kwa nafaka hiyo nchini, hususani inayotoka Dodoma na Ruvuma, mikoa ambayo alisema imekumbwa na ukame. “Bei ya kununulia mahindi imepanda mara mbili ya awali. Tunaiomba Serikali itusaidie tupate mahindi, hali ikizidi kuwa kama hivi sasa atakayeumia ni mwananchi wa kawaida,” alisema Munisi.
Munisi alisema umoja huo ndiyo unaosambaza unga kwa asilimia kubwa mikoa ya Dar es Salaam, Morogoro, Pwani, Tanga na Zanzibar hivyo kuiomba Serikali iingilie kati kuimarisha hali ya upatikanaji wa mahindi ili kusitokee mfumuko wa bei. Alisema sababu zinazosababisha uhaba wa mahindi mwaka huu ni Serikali kuchelewa kuzuia bidhaa hiyo kusafirishwa nje kwa kuwa mahindi yalikuwa yameshasafirishwa. Pia alisema migogoro baina ya wakulima na wafugaji ulisababisha mimea kukatwa au kuliwa na mifugo.
Munisi alisema tatizo hilo lilijitokeza pia mwaka jana ila hali haikuwa kama ya mwaka huu baada ya Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) kutoa mahindi na kuwauzia kwa bei ya Sh480 mpaka 500 kwa kilo.
Msimamizi wa Kampuni ya Msouth Extra Power Sembe, Evod Sanga alisema wameanza kuuza kiroba mara mbili ya bei ya awali ili kupata faida ya shughuli wanazofanya kuzalisha sembe.
“Tangu kuanza kwa hili tatizo, hata bei zetu tumepandisha. Kwa sasa, awali bei ya kiroba cha kilo tano ilikuwa Sh3,000 lakini sasa tunauza Sh6,000, cha kilo kumi kilikuwa kinauzwa Sh7,000 sasa Sh11,000 pia cha kilo 25 tulikuwa tunauza Sh17,000, lakini sasa ni Sh26,000 na cha kilo 50 ilikuwa Sh30,000 sasa imefikia Sh 53,000 na bado hatupati faida,” alisema Sanga.
Mshauri wa masuala ya fedha kutoka Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Revelian Ngaiza alisema wafanyabiashara na wananchi wanatakiwa kuwa wavumilivu kwani msimu mpya utaanza Februari mwakani hivyo upatikanaji wa mahindi utakuwa wa kawaida. “Mikoa ambayo wanaegemea kupata mahindi ni ile inayotegemea msimu mmoja kwa mwaka tofauti na Kanda ya Ziwa wanaotegemea misimu miwili. Pia hali hiyo inachangiwa na mahitaji na usambazaji wa mahindi maana watu ni wengi na hiki si kipindi cha mavuno,” alisema Ngaiza
Ngaiza aliongeza kuwa endapo hali itazidi kuwa mbaya, Serikali itaingilia kwa kuuza kwa wafanyabiashara mahindi yanayohifadhiwa na NFRA ili kukabiliana na hali hiyo.
No comments:
Post a Comment