Tuesday, November 15, 2016

UTAFITI:24% YA WANAWAKE HUFARIKI DUNIA WAKATI WA KUJIFUNGUA.

dk-nguke-mwakatundu
DK.NGUKE MWAKATUNDU.
Wanawake 8,000 nchini   (wastani wa wanawake 24 kwa siku), hufariki dunia wakati wakijifungua, kwa mwaka.
Idadi hiyo inaifanya Tanzania kushika nafasi ya nne Afrika na ya sita duniani kwa vifo vya wajawazito na watoto, kwa mujibu wa utafiti mbalimbali duniani.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Shirika la Thamini Uhai, Dk.Nguke Mwakatundu alisema katika kuthamini uhai wa binadamu, shirika limesaidia kuboresha vituo vya afya vijijini na kuwasaidia wanaojifungua kuepuka hatari wakati wa kujifungua.
Alisema nchi nyingine zinazoongoza kwa tatizo hilo ni India, Ethiopia na Pakistan hivyo ni vema serikali ikaendelea kuiangalia kwa karibu sekta hiyo muhimu ya afya na kuipa kipaumbele.
“Kwa kubaini tatizo hilo shirika letu liliona haja ya kuokoa, kuhifadhi na kuboresha maisha ya wanawake na watoto wachanga katika mikoa ya Kigoma, Morogoro na Pwani likishirikiana na serikali tangu mwaka 2008.
“Kwa kushirikiana na wadau tumejitahidi kuboresha upatikanaji wa huduma za dharura za uzazi katika vituo vya afya 19 vijijini,” alisema Dk. Mwakatundu.
Alisema mwaka 2014 shirika lilianza kampeni  ya kuhamasisha jamii mambo mbalimbali ya uzazi yanayolenga kupunguza vifo vya wajawazito na watoto wachanga.
Mambo hayo ni pamoja na  kuhamasisha kujifungulia kwenye vituo vya afya, kufanya matayarisho ya kujifungua na kuwahi kwenye kituo mara wanapokuwa na dalili za hatari.
“Serikali ina mikakati mingi ya kukabiliana na tatizo la vifo vya wanawake na watoto ila utendaji bado ni mdogo.
“Hiyo ni  kwa sababu ya changamoto mbalimbali zinazovikabili vituo vya afya ikiwamo uchache wa watoa huduma na vifaa tiba hivyo ni vema kuwekwa mikakati thabiti ya kumaliza tatizo hilo.
Kaimu Mkurugenzi Msaidizi kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, kitengo cha afya ya mama na mtoto, Dk. Koheleth Winani, alisema kila mwananchi ajitahidi kuwa  na ushirikiano kupunguza vifo vya wanawake na watoto.
“Twakwimu zinaonyesha kuwa asilimia 85 ya wanawake wanaofika vituo vya afya hujifungua bila matatizo na asilimia 15 hupata matatizo kwa sababu mbalimbali zikiwamo upungufu wa damu, shinikizo la damu, malaria, ukosefu wa dawa na vifaa tiba na mengineyo,” alisema.
Alisema wanawake wakipatiwa huduma muhimu wana uwezo wa kujifungua salama hivyo iko haja kwa jamii kushirikiana na serikali kuboresha huduma hizo na kila mmoja kwa upande wake aone ana wajibu wa kuokoa vifo vya wanawake na watoto.

No comments: