Tuesday, November 15, 2016

UTAFITI:TANZANIA INA JUMLA YA WAGONJWA 822,880 WA KISUKARI.

UMMY MWALIMU.
Tanzania ina wagonjwa wa kisukari wapatao 822,880 kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2015, huku ugonjwa huo pamoja na magonjwa mengine yasiyo ya kuambukiza yakiwamo kisukari, magonjwa ya moyo na mishipa ya damu, kansa na magonjwa sugu ya mfumo wa hewa yakiongezeka kwa kasi zaidi nchini.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu amesema jana kuwa utafiti uliofanyika mwaka 2012 na kuhusisha wilaya 50 nchini, ulionesha kuwa asilimia 9.1 ya Watanzania wenye umri wa miaka 25-64 wana ugonjwa wa kisukari.
Ugonjwa wa kisukari ni hali ambayo hutokea wakati sukari katika damu inapokuwa nyingi kupita kiwango cha kawaida kwa muda mrefu.
Sukari hutumiwa na mwili ili kupata nishati lishe. Ili mwili uweze kutumia sukari inayotokana na vyakula, unahitaji kichocheo cha insulini. Insulini husaidia sukari kuingia kwenye chembechembe hai ili kutengeneza nishati lishe.
Ugonjwa wa kisukari unasababishwa na kichocheo hicho kupungua au kutofanya kazi kama inavyotakiwa, hivyo kiwango cha kisukari kinabaki kikubwa kwenye damu kwa sababu sukari haikuwezeshwa kuingia kwenye chembechembe hai za mwili.
Akitoa tamko la Siku ya Kisukari Duniani inayoadhimishwa duniani kote kila Novemba 14, Waziri Ummy alisema takwimu za watoto wenye kisukari mwaka 2015 ni kati ya asilimia 15 mpaka 20 ya wagonjwa wote wa kisukari ambao wanatibiwa kwenye kliniki nchini.
“Lakini wapo wengine wengi hawajitokezi kwenye kliniki kwa sababu mbalimbali zikiwemo imani potofu, gharama pamoja na umbali wa huduma za afya zilipo pamoja na ukosefu wa elimu juu ya tatizo hili,” alieleza Ummy.
Akifafanua zaidi takwimu, Ummy alisema asilimia 80 ya wagonjwa wote wa kisukari ulimwenguni wanaishi katika nchi zinazoendelea, ikiwemo Tanzania.
“Tafiti za ugonjwa wa kisukari zinaonesha kuwa mwaka 2007 kulikuwa na wagonjwa milioni 246 duniani. Takwimu za mwaka 2015 kutoka kwenye Atlas ya kimataifa ya kisukari zinaonesha kuwa kulikuwa na wagonjwa milioni 415 duniani kote. Ifikapo mwaka 2040 inatarajiwa kuwa na wagonjwa milioni 642,” alieleza Ummy na kuongeza:
“Katika Bara la Afrika kulikuwa na wagonjwa wa kisukari milioni 14.2 mwaka 2015 na idadi hii itaongezeka na kufikia milioni 34.2, na kwa Tanzania mpaka mwaka 2015 kulikuwa na jumla ya wagonjwa 822,880 wa kisukari.”
Kaulimbiu ya maadhimisho ya Siku ya Kisukari Duniani mwaka huu ni “Macho yote kwenye Kisukari” na waziri huyo alisema kaulimbiu hiyo inalenga katika kuwafumbua macho zaidi wananchi kwamba kisukari ni tatizo linalopamba moto siku hata siku, hivyo nguvu ziongezwe kuhakikisha wanajikinga na tabia zinazosababisha upatikanaji wa tatizo hilo.
Alisema macho hayo yaangalie zaidi katika tabia za ulaji unaofaa, kufanya mazoezi, kuepuka matumizi ya pombe kupita kiasi na matumizi ya tumbaku.
Alifafanua kuwa ulaji unaofaa ni pamoja na kula chakula mchanganyiko cha kutosha kukua na kuwa na uzito wa kawaida na chenye virutubisho vyote vinavyohitajika mwilini.
“Kwa mfano vyakula vya wanga vinasaidia kuupa mwili nguvu na joto, protini husaidia kujenga mwili na kutengeneza vichocheo mbalimbali, matunda, mboga, vitamini na madini hulinda mwili dhidi ya magonjwa,” alieleza Ummy.
Alisema ili kuzuia ugonjwa wa kisukari na maradhi mengine yasiyo ya kuambukiza ni muhimu kufuata kanuni za afya ambazo ni ulaji bora, na mtindo bora wa maisha ambao ukifuatwa vyema huweza kuzuia mtu kupata kisukari au kwa mtu ambaye tayari ana ugonjwa wa kisukari hupunguza uwezekano wa kupata madhara makubwa ya kiafya.
Alitaja madhara za ugonjwa wa kisukari kuwa ni upofu, mtoto wa jicho, shinikizo la damu kuwa juu, kiharusi, ugonjwa wa figo, kupungua nguvu za kiume, upungufu wa kinga mwilini, kuwa na vidonda hasa miguuni visivyopona pamoja na ganzi ya miguu au mikono.

No comments: