RAIS JOHN POMBE MAGUFULI. |
Rais John Magufuli amekutana na vyombo vya habari Ikulu jijini Dar es Salaam katika tukio ambalo limehusisha wahariri na kutumia dakika 160 kuelezea mambo yaliyojitokeza katika mwaka mmoja wa utawala wake.
Katika mkutano huo ulioanza saa 3:58 asubuhi mpaka saa 6.40 mchana, Magufuli aliyekuwa akizungumza kwa upole na masihara mara kadhaa, mbali na suala la muswada wa Sheria ya habari, mambo mengine yaliyoulizwa na kupata ufafanuzi ni mchakato wa Katiba Mpya, Tanzania ya viwanda, mgawanyo wa madaraka, ubora wa elimu, ugumu wa maisha na mgogoro wa Zanzibar.
Akijibu swali la muswada wa sheria ya habari hilo, Rais Magufuli amesema sheria hiyo kama zilivyo nyingine zimefuata utaratibu wa kupelekwa bungeni na kuwa ukipitishwa na kuwa sheria atausaini haraka.
“Sheria ya habari imeanza nafikiri kuanzia mwaka 2011, baadaye ukatolewa kwamba tujiandae zaidi. Sasa kama ndiyo hivyo kuanzia mwaka 2011 watu hawakujiandaa, mpaka leo 2016 hawakujiandaa maana yake hata wakipewa miezi mitatu hawawezi kujiandaa.
“…Mimi nakwambia bila unafiki, siku ukiletwa kwangu nitaisaini, ili kusudi kama mnataka kuibadilisha mkaibadilishe. Sitaki ku-frustrate (kupinga) maamuzi ya Bunge.Mnaweza kujikuta mnazungumza kwa sababu ya wamiliki wa vyombo fulani fulani, mtakuwa mmepotea. Kwa sababu katika rasimu niliyoiona, sifahamu wabunge watakachoamua, lakini pia ni ya kulinda masilahi ya waandishi wa habari na mnakuwa na vyombo vyenu,” amesema.
Kuhusu madai ya kuwapo kwa rushwa kwa wabunge ili muswada huo upitishwe, Rais Magufuli amesema kuna vyombo vya kupambana na rushwa vitashughulikia.
Wakati kukiwa na manung’uniko miongoni mwa wananchi kuhusu hali ngumu ya maisha, Rais Magufuli amesisitiza wanaolalamika hivyo ni watu waliozoea ‘kupiga dili’ kwa njia chafu.
“Mifuko imekauka, imekaukaje? Maana yake ulikuwa unapata fedha za ajabu ajabu. Sasa tumia mbinu nyingine ya kupata hela. Ndiyo maana nimetoa mfano wa ndugu zetu wa Lindi kule, mwaka jana waliuza korosho kwa kilo Sh600 hadi 700 mpaka 1,000. Leo kilo moja ya korosho wanauza kwa Sh4,000, four times (mara nne). Sasa huyo ukisema hela hamna atakushangaa,” amesema.
Hata hivyo, hotuba ya Rais Magufuli haikupita bila wadau kutoa maoni yao.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu(LHRC), Dk Hellen Kijo-Bisimba amesema Rais Magufuli kusitisha mchakato wa Katiba ni kulitia Taifa hasara.
“Inasikitisha sana kusikia Rais hana mpango na mchakato wa Katiba wakati ulitugharimu pesa nyingi kama Taifa kuufikisha mahali ulipofikia na ukweli ni kwamba nchi inahitaji Katiba Mpya,” amesema.
Profesa Abdallah Safari amesema, “Magufuli anairudisha nyuma Tanzania badala ya kuipeleka mbele, pesa nyingi zilitumika mchakato wa kuandika Katiba, iweje asitishe kwa urahisi namna hii.”
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Benson Bana amesema ni vyema Watanzania wakatambua kuwa Katiba inatakiwa kuandikwa kwa utulivu na usahihi, hivyo ni vyema wakajipa muda.
No comments:
Post a Comment