Saturday, November 5, 2016

MAGUFULI: YANGA NA SIMBA MWIKO KUTUMIA UWANJA WA TAIFA.

Rais John Magufuli akiwa na msanii nguli wa mashairi nchini, Mrisho Mpoto, Ikulu, Dar es Salaam baada ya Rais kuzungumza na wahariri na waandishi wa habari jana. (Picha na Mroki Mroki).
RAIS MAGUFULI AKIWA NA MRISHO MPOTO, JANA IKULU.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John Pombe Magufuli amepigilia msumari wa mwisho kwa timu za Simba na Yanga na kuzitaka zifute ndoto za kutumia Uwanja wa Taifa.
Rais Magufuli alisema jana Ikulu Dar es Salaam, katika mkutano wake na wahariri wa vyombo mbali mbali vya habari na kudai kuwa anapenda kwenda uwanjani kuangalia mpira, lakini anashindwa kufanya hivyo kutokana na fujo ambazo zimekuwa zikizuka kwenye mchezo wa mpira wa miguu.
“Natamani kwenda Ndondo Cup kuangalia kuliko kwenda kuangalia timu ambazo wanashindana Uwanja wa Taifa, wakishindwa wanang’oa viti,”alisema Rais Magufuli na kuongeza: “Nimefurahi uamuzi wa Waziri (Nape) kufungia uwanja, ni lazima kujenga nidhamu, uwanja umejengwa kwa gharama kubwa, huwezi kung’oa viti, Ndondo ni bora kuliko hizo timu kubwa,”alisema.
Kauli ya Magufuli imekuja ikiwa ni siku za kadhaa baada ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye kuzifungia kutumia Uwanja wa Taifa kwa muda usiojulikana timu za Simba na Yanga kutokana na mashabiki wa timu hizo kung’oa viti katika mechi ya Ligi iliyofanyika Oktoba mosi na timu hizo kutoka sare ya bao 1-1.
Hata hivyo, vurugu kubwa ziliibuka kabla na baada ya mchezo huo ambao kabla ya mchezo mashine za tiketi za elektroniki zilishindwa kufanya kazi na kusababisha mlundikano kwenye mageti upande wa lango la Yanga na mashabiki kukosa uvumilivu na kuvunja mageti hayo.
Vurugu nyingine kubwa ilizuka dakika ya 26 ya mchezo baada ya mchezaji wa Yanga, Amis Tambwe kuifungia timu yake bao, akimalizia pasi ndefu ya beki Mbuyu Twite na kugeuka mbele ya beki wa Simba, Novat Lufunga kabla ya kufumua shuti lililomshinda kipa Vincent Angban.
Bao hilo lilizua utata, huku wachezaji wa Simba wakimvaa refa Martin Saanya wakidai mfungaji, Tambwe aliushika mpira kabla ya kufunga.
Katika vurugu hizo, Saanya alimtoa kwa kadi nyekundu nahodha wa Simba, Jonas Mkude dakika ya 29 kwa sababu ndiye aliyekuwa mstari wa mbele, hata hivyo Mkude alikuja kufutiwa adhabu yake na kamati ya saa 72.
Katika vurugu hizo, serikali iliamuru Simba kulipa gharama ya viti 1,781 vilivyoharibika, ikiwa ni pamoja na kuzuia mgawo wa Simba hadi walipe gharama za uharibifu, na Yanga ilitakiwa kulipa gharama ya mageti manne ya upande wa mashabiki wake 

No comments: