MKUU WA MKOA WA DAR ES SALAAM, PAUL MAKONDA. |
Mkoa wa Dar es Salaam unatarajia kujenga vituo vikubwa vya Polisi 20 ili kuimarisha ulinzi, pamoja na kuondoa changamoto ya ubovu wa vituo kwa vilivyopo, ambayo imegeuka kero kwa askari na wananchi wa mkoa huo wanaovitumia.
Hayo yalisemwa na Mkuu wa Mkoa huo, Paul Makonda wakati alipofanya ziara katika vituo vidogo vya Polisi vilivyopo katika mkoa huo.
Makonda alisema vituo vyote vinatarajia kutumia Sh bilioni 10 hadi kukamilika na kila kimoja kitakuwa na uwezo wa kuwa na askari 100.
“Najua serikali haikuwa na bajeti hii na hatuwezi kusubiri bajeti huku wananchi na askari wetu wakiteseka, mkoa huu una wadau wengi wenye uwezo na wanapenda kuona hali ya ulinzi ikiwa shwari, hivyo naamini tutajenga na tutafanikiwa,” alisema Makonda.
Alisema uwepo wa vituo hivyo utasaidia kuondoa changamoto ya wizi wa silaha zilizokuwa zikuibwa na majambazi waliokuwa wakivamia vituo na kuwaua askari.
“Tunategemea kila wilaya itakuwa na vituo vinne vya kisasa vitakavyokuwa na sehemu nzuri kwa ajili ya kuhifadhi silaha, askari wetu hawatakutana tena na changamoto ya kuuawa na kuibiwa silaha,” aliongeza.
Aidha, Makonda alitoa mwito kwa wananchi kushirikiana kuwafichua wezi wanaotumia pikipiki, majambazi na wauza dawa za kulevya ili wachukuliwe hatua za kisheria na Dar es Salaam ibaki kuwa safi.
“Hatuwezi kuwaachia polisi wenyewe lazima na sisi wananchi tushiriki kutoa taarifa Polisi, naamini kwa kufanya hivyo kutasaidia kupunguza vitendo vya uhalifu na mkoa utakuwa shwari hata ukisahau simu mahali na ukarudi ukaikuta,” alisema.
No comments:
Post a Comment