Monday, November 7, 2016

SIMBA CHALII, YANGA WANACHEKA.

WACHEZAJI WA YANGA WAKISHANGILIA.
Simba jana ilionja joto ya kufungwa kwenye Ligi Kuu bara baada ya kukubali kichapo cha bao 1-0 kutoka kwa African Lyon katika mechi iliyochezwa kwenye Uwanja wa Uhuru Dar es Salaam.
Wakati Simba ikionja joto hiyo, mtani wake wa jadi, Yanga ilichanua kwa ushindi wa bao 1-0 ugenini uwanja wa Sokoine Mbeya dhidi ya Prisons huku Azam ikikubali kipigo cha mabao 2-1 kutoka kwa Mbao kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.
Kwenye Uwanja wa Uhuru Dar es Salaam, iliichukua dakika ya 90 Lyon kupata ushindi huo dhidi ya vinara wa ligi, Simba kwa bao lililofungwa na Abdullah Msuhi aliyeunganisha pasi ya Raizan Hafidh kabla ya kuujaza mpira wavuni. Simba ilikuwa ikishambulia muda wote wa mchezo huo huku Lyon iliyocheza mchezo wa kujihami zaidi ikishambulia kwa kushtukiza.
Katika dakika ya 38, Lyon walifanya mashambulizi kupitia kwa mchezaji wake Miraji Selemani, lakini mpira wake wa adhabu aliopiga uligonga mwamba na kutoka nje. Janvier Bukungu nusura aipatie Simba bao katika dakika ya 48 lakini shuti lake lilipaa juu.
Laudit Mavugo nusura afunge katika dakika ya 60 lakini akiwa kwenye nafasi nzuri mpira wake unawahiwa na mabeki wa Lyon na kuuondosha eneo la hatari. Matokeo hayo yanaifanya Simba iendelee kuongoza msimamo wa ligi ikiwa na pointi zake 35.
Kwenye uwanja wa Sokoine Mbeya, shujaa wa mabingwa watetezi Yanga, alikuwa Simon Msuva aliyefunga bao la mkwaju wa penalti katika dakika ya 74. Mwamuzi wa mchezo huo alitoa penalti hiyo baada ya mchezaji wa Yanga, Obrey Chirwa kuchezewa vibaya katika eneo la hatari.
Awali, Prisons ilipata penalti kipa wa Yanga, Beno Kakolanya akaokoa mkwaju huo na hivyo kuiacha timu ikiwa salama. Yanga sasa imeendelea kuwa nafasi ya pili kwenye msimamo ikiwa na pointi 30, tofauti ya pointi tano dhidi ya vinara Simba.
Mshindi wa pili wa msimu uliopita, Azam bado imeendelea kupata matokeo ya homa za vipindi baada ya jana kuchapwa na Mbao Fc mabao 2-1 kwenye uwanja wa CCM Kirumba Mwanza. Matokeo hayo yanaifanya Azam ibaki na pointi 22 huku Mbao ikifikisha pointi 16.


Mbao iliandika bao lake la kwanza katika dakika ya 30 likifungwa na Venance Ludovick aliyeunganisha pande la Boniphace Maganga kabla ya kuujaza mpira wavuni. Dakika ya 50 Maganga aliifungia Mbao bao la pili na dakika ya 67 Francesco Sekumbawira aliifungia Azam bao la kufutia machozi.

No comments: