Tuesday, October 18, 2016
10 WAPOTEZA MAISHA KWENYE AJALI LINDI.
Watu 10 wamekufa na wengine 44 kujeruhiwa katika ajali ya basi la Kampuni ya Barcelona lililokuwa likitokea Dar es Salaam kwenda Newala mkoani Mtwara jana.
Ajali hiyo ni ya jana saa 5 asubuhi katika kijiji cha Miteja wilayani Kilwa mkoani Lindi, umbali wa kilometa 30 kutoka mkoa wa Pwani na miongoni mwa waliopoteza maisha wamo watoto wadogo watatu.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Lindi, Renata Mzinga akizungumza jana, alisema uchunguzi wa awali unaonesha kuwa chanzo cha ajali ni mwendo kasi wa dereva ambaye bado wameshindwa kumhoji kwa kuwa ni miongoni mwa majeruhi na mpaka jana jioni alikuwa amepoteza fahamu. “Ni kweli ajali imetokea asubuhi saa tano leo (jana), dereva alikuwa katika mwendo kasi, basi likapasuka tairi la mbele, likapinduka. Majeruhi wapo 44 na waliokufa ni 10, wanawake sita na mwanamume mmoja, mtoto wa kike mmoja na wakiume wawili,” alisema Kamanda Mzinga.
Kamanda Mzinga alilitaja basi hilo kuwa ni lenye namba za usajili T110 CUU Youtong, mali ya Kampuni ya Barcelona.
ATCL YATOA OFA KWA ABIRIA WA MWANZA.
Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL) imetoa ofa ya mwezi moja kwa abiria wanaosafiri kutoka Dar es Salaam kwenda Mwanza kulipa nauli ya Sh 160,000 kwa safari moja.
Kauli hiyo ilitolewa jana jijini Dar es Salaam na Kaimu Ofisa Mawasiliano wa Kampuni hiyo, Lily Fungamtama wakati akizungumza na Idara ya Habari (MAELEZO).
Fungamtama alisema ndege za kampuni hiyo, zimeanza kutoa huduma kuanzia Jumamosi iliyopita, kama ilivyobainisha kupitia vyombo vya habari.
Safari hizo zilianza kwa kutoa huduma ya kusafirisha abiria kuelekea nchini Comoro, na hapa nchini inatoa safari katika mikoa ya Mwanza, Arusha na Kigoma.
Alisema kwa kuanzia walianza na mazoezi ya vitendo kwa marubani na wafanyakazi wa ndani ya ndege, na hatimaye walianza safari za biashara ya kusafirisha abiria Oktoba 15, mwaka huu kama ilivyopangwa.
Aliongeza kuwa ATCL imeboresha huduma zake kwa kiasi kikubwa kwa kuwapatia wateja wake ofa ya kubeba kilo 20 za mizigo na kilo saba za mzigo wa mkononi bure pamoja na kutoa vinywaji na ubadilishaji wa tiketi ni bure ndani ya mwezi.
Alikanusha taarifa potofu kuwa zimekwama kuanza safari zilizopangwa. Alisema habari hizo sio za kweli, kwani hivi sasa wameshaanza huduma katika mikoa hiyo mitatu.
ATCL kwa sasa ina ndege tatu, zikiwemo mbili aina ya Bombadier Dash8-Q400 zenye uwezo wa kubeba abiria 76 kila moja, na Dash8-Q300 yenye uwezo wa kubeba abiria 50.
RAIS MAGUFULI AONGOZA MAMIA YA WATU KUAGA MWILI WA MASABURI.
Rais John Magufuli jana aliongoza mamia ya wakazi wa Jiji la Dar es Salaam katika kuaga mwili wa aliyekuwa Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Dk Didas Massaburi aliyefariki Alhamisi iliyopita kwa ugonjwa wa ini.
Dk Magufuli aliwaongoza waombolezaji kutoa heshima za mwisho kwa mwili wa Dk Massaburi (56) kwenye Viwanja vya Karimjee, Dar es Salaam, na alipopewa nafasi ya kuzungumza, alisisitiza familia za marehemu kuishi kwa kushikamana.
“Nawaombeni familia mkashikamane, shetani hujitokeza wakati wa msiba, watoto mumtangulize Mungu, baba aliwapenda wote na hakuwabagua, watoto mkishikamana na mama zenu pia watashikamana. Naomba mtoto mkubwa ukawe nguzo ya familia ili pawe na umoja na Mungu atawasimamia,” alisema Dk Magufuli ambaye alisema anachofahamu marehemu ameacha wake wanne hadi watano na watoto zaidi ya 20.
Akisoma wasifu, kaka wa marehemu, Machabe Massaburi alisema Didas alizaliwa mwaka 1960 Serengeti mkoani Mara akiwa mtoto wa 10 katika familia ya John Massaburi.
Alisema Dk Massaburi amewahi kuwa Diwani wa Kata ya Kivukoni na Meya wa Jiji la Dar es Salaam kuanzia 2010 hadi 2015 na pia Mwenyekiti wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT), Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki na hadi mauti yanamfika alikuwa Mkurugenzi na Mwenyekiti wa Chuo chake cha ugavi IPS kilichopo Chanika.
Alisema marehemu ameacha wajane, watoto, wajukuu kadhaa na kwamba alifunga ndoa na Janeth Massaburi ambaye ni Mbunge wa zamani wa Viti Maalumu.
Dk Magufuli alisema alimfahamu Dk Massaburi kama mpiganaji wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na mengi aliyafanya wakati akiwa Meya wa Jiji la Dar es Salaam na akaongeza kuwa historia yake haiwezi kufutika katika siasa za Tanzania.
Tukio hilo la kuaga lilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa kitaifa na kutoa heshima za mwisho akiwemo Rais mstaafu Jakaya Kikwete na aliyewahi kuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa.
Viongozi wengine ni Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi, Makamu wa Rais mstaafu wa Awamu ya Nne, Dk Mohamed Gharib Bilal, Mama Salma Kikwete, viongozi wa mkoa wa Dar es Salaam, mawaziri mbalimbali, wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano na wabunge wa Bunge la Afrika Mashariki.
Akizungumza kwa niaba ya Bodi ya Wadhamini wa Jumuiya ya Wazazi Taifa, Dk Charles Tizeba alisema wamepoteza rafiki, ndugu na mtu waliyemtegemea zaidi katika uendeshaji wa jumuiya hiyo.
Alitoa mwito kwa familia kuwa kifo hicho, kisiwe chanzo cha ugomvi na mifarakano na kwamba waimarishe umoja.
Msemaji wa Familia, Otieno Igogo alisema kifo hicho ni pigo kubwa na kimekuja katika wakati mgumu kwa kuwa Dk Massaburi amefariki dunia wiki moja na kaka yake, na hakuweza kulifahamu hilo kwa kuwa alikuwa taabani.
Alisema aliacha wosia wa maneno kuwa pindi akifariki, azikwe katika mji wake ulioko Chanika, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam, na kwamba zisifuatwe mila za kabila la Wajaluo kuwa hawazikwi ugenini.
Baada ya kuaga mwili wa marehemu, ulipelekwa katika mji wake eneo la Chanika kwa ajili ya maziko kama alivyowausia mwanasiasa huyo.
WALIOIBA MAKONTENA BANDARINI WAJISALIMISHA.
Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage amesema tayari baadhi ya watu waliotorosha makontena bandarini bila kukaguliwa, wameitikia agizo lake la kuwataka kujisalimisha na kufanyika ukaguzi ili kujiridhisha bidhaa zilizokuwemo ndani ya makontena hayo.
Mwishoni mwa wiki, Mwijage alitoa siku nne kwa wafanyabiashara ambao wanadaiwa kutorosha makontena 100 bandarini, wajisalimishe Shirika la Viwango Tanzania (TBS) ili yakaguliwe. Ili kutekeleza agizo hilo waziri huyo aliweka dawati la dharura kutoa huduma hiyo katika siku za mapumziko.
Alisema wafanyabiashara ambao wangekaidi agizo hilo, wangechukuliwa hatua stahiki, ikiwa ni pamoja na kulipa faini ya asilimia 15. Ukaguzi huo ulitakiwa kufanywa na TBS kwa kushirikiana na Tume ya Ushindani (FCC). Lengo la ukaguzi huo ni kubaini bidhaa zilizoingizwa nchini na ubora wake.
Alisema kuna wafanyabiashara wanaleta makontena yana nguo, ambazo zina kiwango cha chini na wengine hawalipi kodi, wengine wanaleta vilainishi vya magari wakati hapa nchini, pia kuna kiwanda cha kuzalisha vilainishi hivyo, hivyo kuruhusu makontena kupita bila kukaguliwa ni kuua viwanda vya ndani.
Aidha, alisema anaipenda sana kazi yake ya uwaziri, ndio maana analazimika kufanya kazi za chini, ambazo zingefanywa na ofisa wa kawaida wa Shirika la Viwango (TBS).
Akizungumza jana wakati wa kuzindua Sensa ya Uzalishaji Viwandani ya Mwaka 2013, Mwijage alisema ili asiondolewe kwenye wadhifa huo na aliyemteua (Rais John Magufuli), ni lazima afanye kazi hata ya kukagua makontena kwani anafanya hivyo kwa lengo la kulinda viwanda vya ndani.
“Aliyenipa kazi hii tajiri namba moja, ameniagiza nifanye hivyo, ndio maana naenda hadi mitaani kukagua makontena kazi ambayo ingefanywa na ofisa wa kawaida wa TBS,” alisema Mwijage na kutamba kwamba kazi yake hiyo imezaa matunda.
Alisema licha ya kuwepo baadhi ya watu kumkebehi kwenye mitandao ya kijamii kuhusu hatua yake ya kwenda mitaani kukagua makontena, alisema hatishiki kwani yeye kazi yake ya kwanza kuifanya ilikuwa ni ya ukaguzi na hivyo anaifahamu vyema kazi hiyo.
“Nawaambia hivi nitaendelea kwenda kukagua makontena, niacheni nifanye kazi yangu, acheni kuniandika kwenye mitandao,” alisema Mwijage.
Aliongeza “Nilianza kazi nikiwa navaa khaki wakati nafanya kazi hiyo ya ukaguzi, licha ya kuwa leo hii mimi ni waziri, ndio maana niliwaambia wafanyakazi wa TBS wasiwe na haraka ya kupanda vyeo, nani angejua mvaa kaki angepanda hadi kuwa waziri.”
Alisema kuna bidhaa zinatoka nje zikiwa hafifu na hazina ubora, zinaingizwa nchini na kubandikwa lebo ya bandia.
“Kwa mfano kuna tomato zinatoka nje hazina ubora, lakini wanaweka lebo ya bandia, sasa tusipokagua kontena hizi zinaonekana ni bidhaa za maana kuliko tomato za nyanya za Morogoro ambazo zina ubora wa asili.
“Natoa mwito kwa Watanzania kununua bidhaa zinazozalishwa nchini kwani zina ubora kuliko bidhaa zinazotoka nje. Tunataka waje na ukaguzi ufanyike kwa usahihi ili kujua ubora wao, na sisi tutaendelea kunadi tomato yetu ya hapa nchini na matokeo tukutane huko sokoni,” alisema.
Alisisitiza kuwa yeye pamoja na wizara yake wataendelea kufuatilia kila kontena linaloingizwa nchini ili kujua ubora wa bidhaa pamoja na ulipaji wa kodi.
Alisema hana nia mbaya na wafanyabiashara ila anachowataka ni kutaka wafanye biashara katika uwanja sawa wa kibiashara.
Pia alitoa mwito kwa wafanyabiashara kuhakikisha kwamba hawaleti nchini bidhaa, ambazo zinatengenezwa na viwanda ambavyo vimeajiri watu wengi nchini.
Alisema kuruhusu kuleta bidhaa hizo nchini ni kuua viwanda vya ndani na matokeo yake ndio kunazalishwa vijana wahalifu, kama wale wa kundi la Panya Road.
LIVERPOOL 0 - 0 MANCHESTER UNITED
Mchezo wa kusisimua wa ligi kuu ya soka England umemalizika kwa suluhu ya bila kufungana.
Katika mchezo huo kipindi cha kwanza timu zote zilishambuliana kwa zamu huku kipindi cha pili Liverpool ikishambulia zaidi lango la United.
Kocha wa Liverpool Jurgen Klopp amesema kuwa hakukasirika lakini pia hakufurahishwa na kiwango cha uchezaji wa timu yake.
Klopp pia ameisifu safu ya ulinzi ya Man U na kusema ilikuwa vigumu kushinda kutokana na ulinzi ulivyokuwa imara.
Kwa upande wake meneja wa Man U Jose Mourinho amesema licha ya kutopata matokeo aliyoyataka lakini ameridhishwa na matokeo hayo.
Amesema si matokeo mabaya kwani waliweza kumzuia hasimu wao wa jadi kuondoka na alama tatu nyumbani kwake.
Katika mchezo huo Ander Herrera aliibuka kuwa mchezaji bora huku akiwa mchezaji aliyegusa mpira mara nyingi kuliko mchezaji yoyote , aligusa mpira mara tisini
MKE WA DONALD TRUMP AMTETEA MUMEWE.
Mke wa mgombea urais wa chama cha Republican Donald Trump, Melania, amesema wanawake wanaomtuhumu mumewe kwa kuwadhalilisha kingono ni wanasema uongo, na kusisitiza kwamba Bw Trump ni "mwanamume mstaarabu".
Amesema hata hivyo kwamba matamshi ambayo Bw Donald Trump aliyatoa kwenye kanda ya video ya mwaka 2005 kuhusu wanawake hayakubalini, ingawa amesema hayaonyeshi mwanamume ambaye yeye amemfahamu.
Mgombea huyo wa chama cha Republican ana makosa ya kushiriki "mazungumzo ya wavulana faraghani" lakini alichochewa na mtangazaji wa runinga Billy Bush, Bi Trump amesema.
Kanda hiyo ya ivdoe iliwafanya viongozi wengi wakuu wa chama cha Republican kuacha kumuunga mkono.
Kwenye video hiyo, Bw Trump anaonekana akimwambua Bw Bush, ambaye alikuwa mtangazaji wa kipindi cha Access Hollywood cha NBC, kwamba anaweza kujilazimisha kimapenzi kwa wanawake kwa sababu yeye ni nyota.
Tangu kutolewa kwa kanda hiyo, wanawake kadha wamejitokeza na kudai Bw Trump alidhalilisha kimapenzi, madai ambayo mgombea huyo amekanusha.
"Najua yeye huwaheshimu wanawake lakini anajitetea kwa sababu yanayosemwa ni uongo," Bi Trump amesema kwenye mahojiano na CNN.
"Namwamini mume wangu," amesema.
"Mume wangu ni mkarimu na mwanamume mstaarabu. Hawezi kufanya hayo."
Amedai kashta hiyo "imepangwa na kuandaliwa ili kumzuia kushinda" na kundi la kampeni la mpinzani wake Hillary Clinton na wanahabari.
"Kwa maelezo waliyopata (wanahabari) hawafanyi uchunguzi zaidi kuhusu wanawake hawa? Hawana maelezo ya kweli," ameongeza.
Akiongea kwa mara ya kwanza tangu madai hayo kutokea, Bi Trump amesema mumewe hajawahi kuwadhalilisha wanawake.
Anasema mara kwa mara wanawake walimwendea mumewe mbele yake wakitaka awape namba yake ya simu kwa njia isiyofaa.
Akiongea kuhusu kanda hiyo ya mwaka 2005 ya Access Hollywood ambay ilitolewa kwa wanahabari siku 10 zilizopita, amesema: "Nilimwambia mume wangu, wajua, lugha uliyoitumia haikufaa. Haikubaliki."
"Na nilishangaa kwa sababu huyo si mwanamume ninayemfahamu."
Bi Trump anaamini Billy Bush, ambaye alifutwa kazi na NBC kuhusu kanda hiyo, ndiye wa kulaumiwa.
Bw Trump, alisema, "alihadaiwa, na kupotoshwa na mtangazaji huyo aseme mambo mabaya".
Zimesalia wiki tatu kabla ya uchaguzi na kura za maoni zinaonesha Bw Trump yuko nyuma mpinzani wake wa Democratic Hillary Clinton katika majimbo muhimu yanayoshindaniwa.
Subscribe to:
Posts (Atom)

