Tuesday, October 25, 2016

KOCHA PLUIJM AONDOLEWA YANGA.

Kocha Mkuu wa Yanga, Hans van Pluijm amesema ahofii lolote hata kama mabosi wake wameleta kocha mpya atakuwa tayari kuondoka.
Jana kwenye gazeti moja la michezo iliripotiwa kuwasili kwa kocha mpya Mzambia George Lwandamina ambaye anadaiwa kuletwa na Kampuni ya Yanga Yetu iliyoikodisha klabu ya Yanga.
Kwa zaidi ya mwezi sasa kumekuwa na tetesi za Yanga kubadili benchi la ufundi kwa madai ya kutoridhishwa na mwenendo wa timu kwa sasa.
Yanga iko nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu ikiwa na pointi 21 nyuma ya Simba inayoongoza kwa pointi 29.
Hata hivyo chini ya Pluijm, Yanga ilitwaa ubingwa wa Ligi Kuu misimu miwili mfululizo na kucheza hatua ya robo fainali ya michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika. Kocha huyo ambaye kwa sasa ana mkataba na Zesco ya Zambia, anadaiwa kuja kufanya mazungumzo ya mwisho na Yanga kabla ya kurudi tena Zambia kuweka mambo sawa na kisha kurudi rasmi kuwafundisha mabingwa hao wa soka Tanzania bara.
Akizungumza jana na gazeti hili, Pluijm alikiri kusikia taarifa za ujio wa kocha mpya kwenye vyombo vya habari. “Sina taarifa zozote kutoka kwa viongozi wala Mwenyekiti (Yusuf Manji), lakini sina wasiwasi na lolote kama watakuwa wamefikia uamuzi huo, nitakuwa tayari kuondoka, maisha lazima yaendelee,” alisema Pluijm ambaye amekuwa kipenzi cha mashabiki wa Yanga.
Alipoulizwa kuhusu hilo, Kaimu Katibu Mkuu wa Yanga, Baraka Deusdedit alisema hakuna taarifa yoyote ya ujio wa kocha mpya na kama kuna lolote kuhusu benchi lao la ufundi uongozi utatangaza rasmi.
“Suala la kocha bado hatuwezi kuingia mkataba na kocha mpya wakati Pluijm bado ana mkataba, lakini kama kuna chochote tutaweka wazi tu,” alisema.
Pluijm anakumbwa na dhahama hiyo ikiwa ametoka kuongeza mkataba wa miaka miwili kuifundisha timu hiyo mwanzoni mwa msimu huu.

SERIKALI ZA MITAA ZAONGOZA KWA RUSHWA.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angella Kairuki ameitaja Mamlaka ya Serikali za Mitaa kuwa ndio inayoongoza kwa vitendo vya rushwa kisekta nchini, kutokana na kuwa na majalada mengi ya kesi za rushwa zinazoendelea mahakamani.
Aidha, amebainisha kuwa Mahakama ya Ufisadi iko mbioni kuanza kazi, baada ya Jaji Mkuu kukamilisha kutengeneza kanuni za uendeshaji pamoja na mafunzo kwa majaji.
Akizungumza katika kikao kati ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali ya Mtaa mjini Dodoma jana, Kairuki alisema kwa mujibu wa mchanganuo wa kesi zilizopo mahakamani kisekta kuanzia Juni mwaka huu, zinaonesha mamlaka hiyo na sekta ya afya ndio zinaongoza kwa kuhusishwa na vitendo vya rushwa.
Alisema mchanganuo huo unaonesha kuwa hadi Juni mwaka huu, kesi zilizopo mahakamani za kisekta ni 509 na kati ya hizo kesi 209 sawa na asilimia 41 zinaihusu Serikali za Mitaa na kufuatiwa na sekta ya afya ambayo ina kesi 63 sawa na asilimia 12.
“Sekta hii pia kwa mwaka 2015/16 imeonekana kuongoza kwa kuwa na majalada mengi yanayohusu tuhuma za rushwa. Kati ya majalada 3,082 yanayoendelea na uchunguzi, majalada 1,357 sawa na asilimia 44 yanahusu mamlaka hii,” alisisitiza.
Alisema serikali inaendelea kuchukua hatua katika kuzuia na kupambana na rushwa katika eneo hilo hilo la mamlaka ya serikali za mitaa kutokana na kuongoza kwa kuwa na tuhuma na kesi nyingi za rushwa zinazoendelea mahakamani.
Kuhusu hatua za kuanzishwa kwa Mahakama ya Ufisadi zilipofikia, Kairuki alisema mahakama hiyo ipo mbioni kuanza kazi na mashauri yake yatachukua muda wa miezi tisa kusikilizwa na kutolewa maamuzi.
“Jaji Mkuu ameshamaliza kuandaa kanuni na majaji wameshapewa mafunzo na maelekezo kwamba ndani ya miezi tisa shauri ziwe zimekamilika,” alisema.
Kuhusu utendaji wa taasisi ya Takukuru, waziri huyo alisema kwa kipindi cha mwaka 2015/16 kesi mpya 424 zilifunguliwa katika mahakama mbalimbali nchini ikiwa ni ongezeko la kesi 110 ikilinganishwa na mwaka 2014/15.
Pia alifafanua kuwa kati ya kesi hizo, kesi 177 zilihusu kifungu cha 15 cha sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa sura ya 329 na kesi 247 zilihusu vifungu vingine, ambavyo mashitaka dhidi ya watuhumiwa mahakamani yanahitaji kibali cha Mkurugenzi wa Mashitaka ya Umma na katika kesi hizo kesi kubwa zilizokuwa 15. Pia alisema Takukuru imefanikiwa kuokoa Sh 43.78 ikiwa ni ongezeko la Sh 36.78 bilioni ziliozookolewa mwaka 2014/15.
Alisema fedha hizo zilitokana na kitendo cha taasisi hiyo kuanzisha kitengo cha ufuatiliaji wa fedha na mali za watuhumiwa zilizopatikana kwa njia ya rushwa kwa kutaifishwa kwa mali za watuhumiwa.
Kwa upande wa wajumbe wa kamati hiyo walibainisha kuwa adhabu inayotolewa kwa watu wanaotiwa hatiani kwa vitendo vya rushwa haiendani na kosa wanalolitenda.
Mwenyekiti wa kamati hiyo, Jasson Rweikiza aliishauri serikali kuchukua hatua za kudhibiti tatizo la rushwa kwa kuwaboreshea maslahi watendaji wadogo ili kuondokana na rushwa ndogondogo.
Alisema serikali inatakiwa iweke mikakati ya kudhibiti rushwa kuanzia ngazi za chini ikiwemo kuingiza somo la rushwa katika mitaala ya shule.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kitengo cha Uchunguzi wa Takukuru, Alex Mfungo alifafanua kuwa upelelezi wa kesi za rushwa, umekuwa ukichelewa kwa sababu wanataka kujiridhisha kwanza kabla ya kupeleka kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP).

KIKWETE: UDSM IPEWE TUZO YA HESHIMA.


                                                                                          JAKAYA MRISHO KIKWETE      .
Dar es Salaam. Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Jakaya Kikwete amependekeza chuo hicho kupewa tuzo ya heshima baada ya kutoa wahitimu walio na mchango katika nyanja mbalimbali nchini, akiwamo Rais John Magufuli na Waziri Mkuu Kasimu Majaliwa.
Kikwete amesema hayo jana alipokuwa akifungua maadhimisho ya miaka 55, tangu kuanzishwa  kwa  chuo hicho.
 “Chuo hiki kilianza na wanafunzi 14 kikiwa maeneo ya Lumumba ila kwa sasa tunahudumia wanafunzi 24,000 kutoka ndani na nje ya nchi, hii ni hatua kubwa, kimeleta mchango mkubwa sana kwa taifa,” amesema.

Monday, October 24, 2016

UN KUSOMESHA



Umoja wa Mataifa (UN), umejipanga kushirikiana na wadau wake kuwaelimisha vijana 50,000 hapa nchini ifikapo mwaka 2017.
Akizungumza kwenye maadhimisho ya miaka 71 ya UN Mratibu Mkazi wa umoja huo Alvaro Rodriguez alisema hatua hiyo ni endelevu kwani tayari vijana 10,000 wamewezeshwa kutambua malengo hayo hivyo itasaidia kuleta mabadiliko ya kiuchumi nchini.
"Tanzania ina changamoto kadhaa ikiwamo ya ongezeko la vijana na mahitaji yao tunahitaji kuhakikisha kwamba vijana nchini wanawajibika, katika kuejiendeleza na kuendeleza taifa ili kupata maendeleo chanya katika maisha yao.
Mgeni rasmi katika maadhimisho hayo, Waziri na Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Agustino Mahiga alisema UN imekuwa ikishirikia vyema na Tanzania kwa mambo mengi ya maendeleo, ulinzi na Usalama. 
Alisema UN imekuwa ikiitumia wanajeshi wa nchi nyingi ikiwamo Tanzania katika kulinda amani kwenye nchi zilizopo kwenye migogoro, hatua ambayo imekuwa ikisaidia vijana kupata ajira na ujuzi wa masuala ya kiusalama.

MTOTO AMBAE HAJAWAHI KUTEMBEA WALA KUKAA.

 Devotha Nagaikaya akiwa amepakatwa na shangazi yake Emma Nagaikaya.
Mtoto Devotha Lucanus Nagaikaya, anayeishi na shangazi yake katika mtaa wa Togo, kata ya Mahenge Mjini, wilaya ya Ulanga mkoani Morogoro ana umri wa miaka minne, lakini muda wote hubaki amelala kitandani.
Mtoto huyu hawezi kukaa, akacheza wala kutembea na shingo yake imelegea, mikono imekakamaa hivyo inawalazimu walezi wake kumlisha siku zote.
Wakati wote mtoto huyo analazimika kuwa na mwangalizi kwani anapojisaidia huhitaji kubadilishiwa nguo na kufuliwa.
Mtoto huyu analelewa na shangazi yake, Emma Nagaikaya baada ya mama wa mtoto huyu, Imelda Maumba, kumkimbia alipojifungua kutokana na kupatwa na ugonjwa wa kichaa.
Shangazi wa mtoto huyu anasema kutokana na ukosefu wa fedha na maisha duni ya familia yake, ameshindwa kumtibu mtoto huyo licha ya ushauri uliotolewa na madaktari wa kumfanyia mazoezi ya muda mrefu.
Imani ni kwamba pale mtoto huyo atakapofanyiwa mazoezi anaweza kujimudu baadhi ya mambo yeye mwenyewe.
“Mimi shangazi yake sina uwezo wa kifedha, nimeshindwa kumhudumia, muda wote ni kulala kitandani, kulishwa. Muda wote na kuwa chini ya uangalizi," anasema Nagaikaya.
Kutokana na hali duni ya kipato, ameshindwa kumpeleka mtoto huyo katika Hospitali ya CCBRT ya jijini Dar es Salaam alikoandikiwa kupatiwa mazoezi maalumu ya viungo tangu mwaka 2013 hadi sasa.
Kitendo cha kukosa fedha anasema kimemfanya kubaki mjini Mahenge bila ya kuwa na msaada wowote kwa kuwa Hospitali ya wilaya ya Ulanga haina wataalamu wala vifaa vya mazoezi maalumu ya viungo kwa mtoto huyo.
“Nimelazimika kubaki nyumbani nikihangaika na mtoto huyu na matatizo yake yanazidi kukua siku hadi kutokana na kukosa msaada wa kitabibu,” anasema Nagaikaya.
Nagaikaya anaeleza chanzo cha maradhi hayo akisema, mtoto aliyapata tangu akiwa na umri miezi mitano baada ya kuugua homa kali ambayo madaktari walipomchunguza waligundua aliugua homa ya uti wa mgongo.
“Tulimhangaikia kupata matibabu, lakini alipofikisha umri wa miezi minane alionesha dalili za kushindwa kukaa chini, kuongea, wala kushika kitu yenye mweyewe huku akilala muda wote kitandani,” anasema Nagaikaya.
Kutokana na uduni wa kipato, anasema inamlazimu kutumia takribani Sh 17,000 kwa ajili ya kununulia nepi maalumu zinazotosheleza kwa wiki moja pekee na fedha inapokosekana hana namna ya kufanya.
Nagaikaya, ambaye ni mama anayehudumia familia ya watoto 10 wakiwemo wanne wa mdogo wake, hana msaidizi mwingine isipokuwa kubeba majukumu hayo pekee.
Mama huyu anaishi katika nyumba ndogo na watoto hao wanaomtegemea kwa kila jambo. Anaomba jamii iweze kusaidia katika kumtibu mtoto huyo.
Wanafamilia hiyo, wanakiri mtoto huyo anayeumwa kuwa anapata mateso makubwa kutokana na maradhi hayo. Upendo Nagaikaya, anasema familia yao haina uwezo kifedha kugharimia matibabu na mazoezi ya mara kwa mara.
Anasema, baba wa mtoto huyo, Lucanus Nagaikaya mwenye watoto wanne hana uwezo na ameondoka nyumbani hapo muda mrefu kwenda kuishi katika Kijiji cha Ibuyu kutafuta maisha na kumwachia dadake amlee Devota.
Mama yake Devota, ambaye alipatwa na kichaa baada ya kujifungua mtoto huyo, yuko katika kijiji cha Kisewe ambako wanasikia bado yuko katika hali ya kuchanganyikiwa. Upendo, anasema jamii inayowazunguka imekuwa na mtizamo tofauti wakidai mtoto huyo apelekwe kupatiwa tiba za waganga wa jadi kwa madai kwamba amerogwa; kitendo kinachopingwa na familia yao.
Anasema baadhi ya majirani wengine wanaonesha kuguswa na ugonjwa wa mtoto huku wakimfariji shangazi yake.
Jamii inaombwa kumsaidia mtoto huyo kupitia simu ya mlezi wake, Emma Nakaikaya; 0712 801864 aweze kupata fedha za matibabu na pia kumhudumia.
Kwa mujibu wa wataalamu, ugonjwa unaomsumbua mtoto huyu ni matatizo kwenye ubongo (Cerebral Palsy). Huu ni ugonjwa ambao mtoto anaambukizwa akiwa ama tumboni au mara baada ya kuzaliwa kutokana na maambukizi ya bakteria wa ugonjwa huu.
Mtoto mwenye ugonjwa huu, anaweza kutambuliwa kabla ya kufikia umri wa miezi minne. Shingo yake hushindwa kusimama na hawezi kutembea anapofikia miezi 10 hadi mwaka mmoja.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dk Frank Jacob, anaelezea ugonjwa huu akisema watoto wenye nao, hutambulika kutokana na dalili za kushindwa kukua kulingana na umri na uwezo wa vitu anavyovifanya, kuchelewa kuongea au kushindwa kabisa kuongea.
Dk Jacob anasema dalili nyingine ni mtoto mwenye ugonjwa huu anapokuwa akishikwa, mikono yake na mwili wake unakuwa umekakamaa mithiri ya kuni.
Watoto wenye kuzaliwa kabla ya umri wao na wanaozaliwa pacha wapo katika athari za kupatwa na ugonjwa huu.
Wengine walio katika uwezekano wa kuupata, ni wale wanaopata homa kali, uti wa mgogo na kurithi katika familia. Dk Jacob anasema ugonjwa huu hauna matibabu kamili isipokuwa, mtoto anaweza kufanyiwa mazoezi maalumu na ya muda mrefu ili aweze kuimarika kimaumbile kumwezesha kuongea ama kutembea.
Ni kweli tatizo la ugonjwa huu wa ulemavu wa ubongo linawapata baadhi ya watoto mara nyingi akiwa tumboni mwa mwama mjamzito, mtoto anaabukizwa wakati wa msukukuko wa kujifungua ama baada ya muda mfupi kupita,” anasema Dk Jacob.
Dk Jacob anasema pamoja na ugonjwa huu kutokuwa matibabu yakuponyesha kabisa, lakini moja ya tiba inayoweza kuwasaidia watoto wenye ugonjwa huu ni kuwafanyia mazoezi maalumu ya viungo na ni kwa muda wa miaka miwili hadi mitatu.
Anasema kupitia wataalamu maalumu wa mazoezi ya viungo, wanaweza kuboresha upungufu yaliyomo kwa watoto wenye ugonjwa huo na hivyo kuwasaidia kupata unafuu wa kuongea ama kutembea na si kuliondoa kabisa tatizo hili.
“Mazoezi haya yanahitaji vitu vingi na fedha nyingi kwani yanachukua muda wa miaka miwili hadi mitatu kumwezesha mtoto aliyeathirika na ugonjwa huu kuboreka kiafya,” anasema.
Hivyo anasema, ndugu ama wazazi na walezi wa watoto wenye matatizo haya wengi kipato chao ni kidogo na wanaishi mbali na hospitali ya rufaa kuliko na wataalamu na vifaa vya mazoezi maalumu kwa watoto hao.
Matokeo yake, hushindwa kuwapeleka watoto wao kufanyiwa mazoezi hayo maalumu ya viungo ambayo ni ya muda mrefu.
“Mazoezi haya yanaweza kufanyika hata nyumbani kwa mgonjwa, tatizo ni vifaa na wataalamu wa aina hii, hivyo wazazi na walezi wenye watoto wenye ulemavu wa ubongo wamekata tamaa kuwahudumia kitabibu,” anasema Dk Jacob.
Pamoja na hayo, anasema lengo la serikali ni kusogeza huduma kama hivyo katika hospitali za wilaya za mkoa huu, lakini bado changamoto ni rasilimali fedha na wataalamu.

JUSTIN BIEBER AONDOKA JUKWAANI BAADA YA MASHABIKI KUPIGA KELELE WAKATI ANATUMBUIZA.

Justin Bieber

Justin Bieber aliondoka katika jukwaa la tamasha yake mjini Manchester baada ya kuwataka mashabiki kutopiga kelele wakati anapoimba.
Wakati wa tamasha zake tatu zilizopita katika mji huo ikiwa miongoni mwa ziara yake ya dunia nzima mwanamuziki huyo alisema : Nathamini msaada ninaopata, nathamini mapenzi mnayonipa na nathamini ukarimu wenu.Lakini kelele munazopiga wakati ninapoimba lazima zisitishwe.Tafadhali na ahsanteni.Sidhani ni muhimu ninapojaribu kusema kitu na nyinyi mnapiga kelele.
Na mashabiki hao walipokataa kusitisha kelele zao aliangusha kipaza sauti na kuondoka katika jukwaa,huku baadhi ya mashabiki wakimzomea.
Justin Bieber
Baadaye kijana huyo wa miaka 22 alirudi kuendelea na tamasha yake na kuelezea kwa nini aliondoka kwa hasira.
''Nahisi kwamba nataka wasiliana nanyi.Lengo hapa ninapowaangalia katika macho ,mnajua kwamba tuko katika wakati muhimu na kwamba tunawasiliana''.

MWANAMKE MNENE KULIKO WOTE DUNIANI.



Kwa mujibu wa jarida la Daily Mail, inaelezwa kuwa mwanamke huyo aitwaye Iman Ahmad Abdulati mwenye miaka 36 hajawahi kutoka ndani kwa miaka 25 na amekua akiongezeka uzito wake kwa haraka mpaka kufikia kilo 500 zinazompa shida ya kujifanyia usafi na hata kula. Ripoti ya madaktari inaonesha kuwa mwanamke huyu anasumbuliwa na maambukizi ya bakteria wanaoshambulia ukuaji wa mwili.

Akiwa na miaka 11 alianza kusumbuliwa na tatizo hilo ingawa wazazi wake wanakiri kuwa hawakudhani kuwa ni tatizo lakini siku zilivyozidi kwenda ndipo wakabaini kuwa halikua jambo la kawaida hivyo wakaamua kutafuta wataalamu ambao walitoa ripoti kuwa ana matatizo ya mwili wake kukaa na maji mengi bila kuyatoa nje kitu ambacho sio cha kawaida kwa binadamu.