Kocha Mkuu wa Yanga, Hans van Pluijm amesema ahofii lolote hata kama mabosi wake wameleta kocha mpya atakuwa tayari kuondoka.
Jana kwenye gazeti moja la michezo iliripotiwa kuwasili kwa kocha mpya Mzambia George Lwandamina ambaye anadaiwa kuletwa na Kampuni ya Yanga Yetu iliyoikodisha klabu ya Yanga.
Kwa zaidi ya mwezi sasa kumekuwa na tetesi za Yanga kubadili benchi la ufundi kwa madai ya kutoridhishwa na mwenendo wa timu kwa sasa.
Yanga iko nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu ikiwa na pointi 21 nyuma ya Simba inayoongoza kwa pointi 29.
Hata hivyo chini ya Pluijm, Yanga ilitwaa ubingwa wa Ligi Kuu misimu miwili mfululizo na kucheza hatua ya robo fainali ya michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika. Kocha huyo ambaye kwa sasa ana mkataba na Zesco ya Zambia, anadaiwa kuja kufanya mazungumzo ya mwisho na Yanga kabla ya kurudi tena Zambia kuweka mambo sawa na kisha kurudi rasmi kuwafundisha mabingwa hao wa soka Tanzania bara.
Akizungumza jana na gazeti hili, Pluijm alikiri kusikia taarifa za ujio wa kocha mpya kwenye vyombo vya habari. “Sina taarifa zozote kutoka kwa viongozi wala Mwenyekiti (Yusuf Manji), lakini sina wasiwasi na lolote kama watakuwa wamefikia uamuzi huo, nitakuwa tayari kuondoka, maisha lazima yaendelee,” alisema Pluijm ambaye amekuwa kipenzi cha mashabiki wa Yanga.
Alipoulizwa kuhusu hilo, Kaimu Katibu Mkuu wa Yanga, Baraka Deusdedit alisema hakuna taarifa yoyote ya ujio wa kocha mpya na kama kuna lolote kuhusu benchi lao la ufundi uongozi utatangaza rasmi.
“Suala la kocha bado hatuwezi kuingia mkataba na kocha mpya wakati Pluijm bado ana mkataba, lakini kama kuna chochote tutaweka wazi tu,” alisema.
Pluijm anakumbwa na dhahama hiyo ikiwa ametoka kuongeza mkataba wa miaka miwili kuifundisha timu hiyo mwanzoni mwa msimu huu.
No comments:
Post a Comment