Wednesday, October 26, 2016

YANGA WAMLILIA PLUIJM.

Siku moja baada ya aliyekuwa Kocha Mkuu wa Yanga, Hans Pluijm, kuandika barua ya kujiuzulu kuwafundisha mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara, kundi la mashabiki wa timu hiyo wameonesha kutoridhishwa na uamuzi huo na kuutupia lawama uongozi kwa kusababisha kuondoka kwa mpendwa wao huyo.
Pluijm ameifundisha timu hiyo kwa misimu miwili na kuipa mafanikio makubwa ikiwemo kucheza hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika mwaka huu hatua ambayo ilikuwa haijafikiwa na timu hiyo kwa kipindi cha miaka 18 nyuma.
Wakizungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti mashabiki hao hawajaridhishwa na uamuzi wa uongozi wao wa juu na wengine kudai hawatoona ajabu kwa timu hiyo kushindwa kutetea ubingwa wake kutokana na kubadilisha kocha wakati ligi ikiendelea.
Hamisi Abdallah mwanachama wa Yanga kutoka tawi la Buguruni, alisema binafsi angependa Kocha Pluijm aendelee kuifundisha timu hiyo kwa sababu bado hajaona mabaya aliyoyafanya na hasa ukizingatia mafanikio aliyowapa kwa kipindi cha miaka miwili iliyopita.
Abdallah alisema kama uongozi ulitaka kumbadilisha kocha huyo ungesubiri wakati wa dirisha dogo na siyo kipindi hiki, ambacho ligi ipo kwenye ushindani na wapinzani wao Simba wameonekana kujipanga kuwapoka ubingwa wao.
Naye Emmanuel Mgamilo, shabiki wa Yanga kutoka Magomeni alisema kitendo wanachokifanya viongozi wa Yanga kinaweza kuitafuna timu hiyo kushindwa kupata taji lolote msimu huu, kwani kumbadilisha Kocha Pluijm na kuleta kocha mpya ni sawa na kuwachanganya wachezaji.
Mgamilo, alisema kwa mafanikio ambayo wameyapata chini ya Pluijm kocha huyo alikuwa na nafasi ya kuendelea kuifundisha timu hiyo na sababu ambazo uongozi wao umezichukua hata kumtimua kocha huyo hazina mashiko kwani ni sawa na kumdhalilisha kwani rekodi zake zinajieleza wazi.
Kwa upande wake Hamisi Makilo alisema yeye ni shabiki mkubwa wa klabu ya Simba lakini hajafurahishwa na maamuzi ya watani wao Yanga kumruhusu Kocha Pluijm kuondoka kwa sababu amewapa mafanikio makubwa tangu alipoanza kuifundisha timu hiyo na kuendelea kubaki kwake kungeweza kuifikisha mbali zaidi timu hiyo siku zijazo.
Kocha Pluijm aliamua kuandika barua ya kuacha kazi muda mfupi baada ya kupata taarifa ya kuwasili Kocha wa Zesco United, Mzambia George Lwandamina, ambaye kwa muda wa wiki sasa taarifa zake zilizagaa nchini kuja nchini kuziba nafasi ya Mdachi huyo ambaye alitua Yanga kwa mara ya kwanza mzunguko wa pili wa msimu wa 2013/14 akichukua mikoba ya Mholanzi mwenzake Ernie Brandts na aliweza kumaliza nafasi ya pili nyuma ya waliokuwa mabingwa wa msimu huo Azam.
Kabla ya msimu wa 2014/15 kuanza kocha huyo aliomba kuvunja mkataba wake na kuondoka baada ya kupata timu ya kufundisha nchini Saudi Arabia ‘Al Shaola FC’ na alimchukua aliyekuwa msaidizi wake Boniface Mkwasa, lakini hawakudumu sana alitimuliwa huko na kuamua kurudi Ghana anapoishi wakati huo Yanga ikimchukua Mbrazil Marcio Maximo aliyeziba nafasi yake lakini baada ya uongozi wa Yanga kutoridhishwa na mwenendo wa timu yao kwenye ligi uliamua kuachana na Maximo karibu na mwishoni mwa mzunguko wa kwanza mwa
msimu huo na kumrudisha Pluijm na Mkwasa ambao walifanya kazi nzuri na kuipa ubingwa timu wa Ligi Kuu timu hiyo.
Msimu uliofuata wa 2015/16 Pluijm aliiwezesha Yanga kutetea ubingwa huo akiwa ameanza nayo mwanzo na kusajili yeye nyota kadhaa akiwemo Donald Ngoma, Thabani Kamusoko, Hajji Mwinyi na nyota wengi ambapo mbali na kutetea ubingwa pia walibeba Kombe la FA lililofanyika kwa mara ya kwanza baada ya kusimama kwa muda na pia aliweza kuifikisha timu hiyo raundi ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika na kutolewa kwa mabao 2-1 na Al Ahly ya Msri na kuangukia kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho ambapo walifanikiwa kutinga hatua ya makundi.
Pluijm mwenyewe alisema kilichomfanya aandike barua ya kujiuzulu ni dharau aliyooneshwa na viongozi wa Yanga kwa kumleta nchini kocha mpya bila kumtaarifu yeye na amewaomba radhi mashabiki na wanachama wa timu hiyo na kuwataka waendelee kuipa sapoti timu hiyo huku wakisahau mafanikio yake kwani kocha ni mtu wa kuja na kuondoka ila klabu itaendelea kuwepo siku zote.

RAIS MAGUFULI AONGOZA KATIKA TUZO ZA FORBES.

Rais John Magufuli
Jarida maarufu la Forbes limewateua viongozi mbalimbali watano wa Afrika akiwemo Rais John Magufuli, kuwania Tuzo ya Heshima ya Forbes Afrika Mwaka 2016 (Forbes Africa’s Person Of The Year 2016), na upigaji kura umeanza huku Dk Magufuli akiongoza kwa zaidi ya asilimia 70 ya kura.
Jarida hilo maarufu nchini Uingereza, lilifungua kazi ya upigaji kura na hadi jana jioni, kati ya viongozi hao watano, Rais Magufuli alikuwa akiongoza kwa wingi wa kura. Tuzo hiyo hutolewa kwa kiongozi au mtu binafsi aliyejitoa kwa kuhakikisha analeta manufaa ya kibiashara kwa wanaomzunguka.
Kwa mwaka huu, walioteuliwa kuwania tuzo hiyo wako watano ambao ni pamoja na Rais Magufuli, ambaye ameteuliwa kuwania tuzo hiyo kutokana na mapambano yake ya kuinua uchumi wa nchi.
Tangu aingie madarakani takribani mwaka mmoja sasa, Dk Magufuli amesimamia uadilifu katika utumishi wa umma na kurejesha utendaji kazi wenye ufanisi, lakini akiziba mianya ya rushwa na upotevu wa mapato na kuwezesha kuongezeka kwa makusanyo ya kodi na hivyo uchumi wa Tanzania kuendelea kukua kwa kasi.
Wateuliwa wengine katika tuzo hiyo ni Mwanzilishi wa Benki ya Capitec ya Afrika Kusini, Michiel Le Roux aliyefanya benki hiyo kuwafikia wananchi wengi nchini humo; Mwendesha Mashtaka wa Umma, Thuli Madonsela wa Afrika Kusini aliyekabiliana na vitisho vya kifo akitetea haki.
Pia yupo Rais wa Mauritius, Ameenah Gurib anayepambana kulinda mazingira nchini mwake.
Aidha, walioteuliwa wengine ni wananchi wa Rwanda kwa hatua iliyofikiwa na serikali ya nchi hiyo kwa ajili ya kupigania usawa wa kijinsia.
Forbes kupitia mtandao wa poy2016.com hadi jana jioni ulikuwa umefunguliwa na kazi ya kupiga kura ikiendelea huku Dk Magufuli akiongoza kwa asilimia 72 ya kura.
Watu wa Rwanda walifuatia kwa asilimia 21, Madonsela alifuatia kwa asilimia nne huku Gurib na Roux wakiwa na asilimia mbili kila mmoja hadi jana jioni.
Tuzo ya Heshima ya Forbes Afrika 2016 kwa mwaka huu itatolewa Novemba 11 jijini Nairobi nchini Kenya.
Kwa mwaka jana tuzo hiyo ilinyakuliwa na Mtanzania, mfanyabiashara Mohammed Dewji ambaye ni Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Mohammed Enterprises (MeTL).


Tuzo hizo zilianza kutolewa mwaka 2011 na tangu kutolewa kwake zimekuwa zikiwavutia watu mashuhuri na waliofanya mengi katika kukuza uchumi wao na mataifa yao.

MISHAHARA YA WAFANYAKAZI WA SERIKALI KUPANGWA UPYA.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akionesha kitabu Kiitwacho ‘From Lumumba Street to the Hill and Beyond’ baada ya kukizindua katika kilele cha maadhimisho ya Miaka 55 ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) katika ukumbi wa Nkhrumah chuoni hapo jana. Kushoto kwake ni Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Rwekaza Mukandala, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Dk Leonard Akwilapo na Naibu Makamu Mkuu wa UDSM, Profesa Florens Luoga. (Picha na Robert Okanda).
Serikali imeahidi kuboresha na kuimarisha maslahi kwa watumishi wote wa umma kupitia Bodi ya Mishahara na motisha mara watakapokamilisha uhakiki wa taarifa za kiutumishi kwa wafanyakazi wa umma, ambao utawezesha kupanga upya mishahara na motisha kwa watumishi.
Aidha, imesema italipa madeni yote inayodaiwa na watumishi wake wote mara itakapomaliza kufanya uhakiki huo ili kubaini watumishi hewa.
Ahadi hiyo ilitolewa jana na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati wa kilele cha maadhimisho ya miaka 55 ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Udsm).
Katika hotuba yake, Majaliwa alisema Serikali ya Awamu ya Tano imedhamiria kuhakikisha inaondoa malimbikizo ya madai kwa watumishi wote wa umma, na mojawapo ya mikakati hiyo ni uhakiki, ambao unaendelea wa watumishi wa umma. Alisema hadi Oktoba 20, mwaka huu watumishi hewa, ambao wamebainika kutokana na uhakiki huo walikuwa ni 16,500.
“Baada ya uhakiki huo tutarudia uhakiki wa madeni yote yaliyowasilishwa serikalini na kisha tutalipa madeni ya watumishi wote yakiwemo madeni yanayodaiwa na wanataaluma,” alisema Waziri Mkuu Majaliwa.
Kwa muda mrefu sasa, serikali inaendesha uhakiki wa watumishi wa umma baada ya kubainika kuwapo na watumishi hewa wengi wanaolipwa fedha nyingi kila mwezi, hivyo kuipotezea mapato serikali ambayo yangetumika kwa kazi nyingine, zikiwamo za kuboresha mishahara ya watumishi na huduma za kijamii.
Akizungumzia changamoto zinazokikabili Chuo Kikuu cha Dar es Salam likiwemo suala la uhaba wa wahadhiri waandamizi pamoja na tatizo la mikopo kwa wanafunzi, Majaliwa alisema serikali itaendelea kuweka kipaumbele cha upatikanaji wa fedha za kutosha kwa ajili ya mafunzo.
Lakini, pia amevitaka vyuo vya umma, kuhakikisha taratibu na mipango endelevu ya kurithishana kwani bila kufanya hivyo wakati wote kutakuwa na mapungufu katika utoaji wa taaluma. Alisema serikali itaendelea kuwaajiri wanataaluma na watumishi wengine wapya pale wanapohitajika.
Alitoa ahadi hiyo baada ya kuelezwa na Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Rwekaza Mukandala kuwa chuo hicho kwa sasa kinakabiliwa na uhaba mkubwa wa wahadhiri waandamizi kutokana na wengi wao kustaafu.
Kuhusu changamoto ya mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu, Majaliwa alisema Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi inaendelea kufanya uhakiki wa taarifa za waombaji wa mikopo na akasema kufikia kesho asilimia 90 ya waombaji ambao wametimiza masharti watakuwa wameshalipwa fedha zao.
Aliwataka watumishi wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu kutimiza wajibu wao kuhakikisha kwamba, kwa wale ambao uhakiki wao umekamilika wapatiwe mikopo hiyo kwa wakati. Alisema kamwe serikali haitawavumilia watumishi ambao watachelewesha kwa makusudi mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu.
“Kama kuna taarifa itolewe ndani ya serikali haraka ili ifanyiwe kazi kuzuia mgogoro kati ya wanafunzi na serikali yao,” alisema Majaliwa.
Awali, Profesa Mukanda alisema changamoto kubwa inayokikabili chuo hicho kwa sasa ni uhaba wa wanataaluma waandamizi katika fani mbalimbali tatizo ambalo alisema linatokana na serikali kusitisha ajira kwa miaka 10 na hivyo kutoajiriwa wanataaluma chipukizi.
Alisema hali ilivyo kwa sasa katika vyuo vya umma nchini ni mamia ya wanataaluma wazoefu kustaafu kwa wakati mmoja na wanataaluma walioajiriwa katika miaka ya hivi karibuni, bado wako masomoni au wangali chipukizi katika taaluma zao na hivyo kutokuwa na uwezo wa kutosha kubeba majukumu ya kufundisha shahada za umahiri na uzamivu.
Alisema licha ya serikali kuruhusu utoaji wa ajira za mikataba kwa wanataaluma wanaostaafu, lakini bado idara nyingi zinakabiliwa na uhaba mkubwa wa wanataaluma waandamizi.
Alisema hali hiyo inatishia kukwamisha utekelezaji wa azma na mpango mkakati wa chuo hicho ambao ni kupanua programu za mafunzo ya digrii katika ngazi za umahiri na uzamivu.
Kwa hali hiyo aliiomba serikali kutoa mwongozo utakaosaidia vyuo vikuu vya umma vinavyokabiliwa na changamoto hiyo ili viweze kuepuka hatari iliyopo ya kushuka kwa viwango ya utoaji maarifa.
“Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kiko tayari kutoa mchango wa mawazo kuhusu namna ya kuruka kizingiti hicho,” alieleza

Tuesday, October 25, 2016

WAFUASI WA DONALD TRUMP WAKAMATWA UGANDA.

Mgombea wa urais nchini Marekani Donald Trump

Maafisa wa polisi nchini Uganda wamewakamata vijana wawili waliokuwa wakimfanyia kampeni mgombea wa urais nchini Marekani Donald Trump katika ubalozi wa Marekani mjini Kampala.
Mtandao unaounga mkono serikali Chimp Riports umesema kuwa Vijana watano wa kundi la Young Democrats nchini humo walijaribu kuingia katika ubalozi wa Marekani.
Gazeti la Daily Monitor limechapisha ujumbe wa Twitter likionyesha picha za waandamanaji hao.
Wafuasi hao wa Trump waliambiwa na maafisa wa polisi kwamba hawataruhusiwa ndani ya ubalozi kwa sababu walikuwa hawajapata rukhusa,kulingana na mtandao wa Chimp Report.
Trump katika manifesto yake alisema kuwa atakabiliana na marais waliohudumu kwa muda mrefu kutoka Afrika akiwemo rais Museveni.
''Lazima tuonyesha umoja wetu na Trump'',Hakim Kizza ,mmoja wa wanachama wa kundi hilo alinukuliwa akisema.

MAKONDA: NITAMSAIDIA REHEMA KUTIMIZA NDOTO ZAKE ZA KUWA MWALIMU.



Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amesema yuko tayari kumsaidia Rehema Mwilu (16) ili atimize ndoto yake ya kusoma na kuwa mwalimu, baada ya kushindwa kufanya hivyo kutokana na umasikini wa wazazi wake.
Rehema ni binti anayeishi Mtoni Kijichi Dar es Salaam, alihitimu elimu ya msingi katika Shule ya Mtoni Kijichi mwaka 2013 na kufaulu na alichaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza katika Shule ya Sekondari ya Kibada.
Lakini, alishindwa kuripoti shuleni kutokana na ugumu wa maisha na shule kuwa mbali, hali iliyosababisha aendelee kukaa nyumbani hadi leo. Baada ya kukaa nyumbani kwa muda, alitokea mwanaume aliyezungumza na wazazi wake na kupeleka barua ya posa na wazazi waliridhia Rehema kuolewa, kutokana na kutokuwa na pa kwenda, lakini alikataa kwa kuwa malengo yake yalikuwa ni kusoma.
Akizungumzia suala hilo, Makonda alisema ipo haja ya kujipanga kuona ni kwa namna gani Rehema ataweza kusaidiwa kusoma na kutimiza ndoto zake na aweze kusoma shule ya kulala ili kuepuka usumbufu.
“Ni kweli anahitaji msaada, lakini nitajitahidi kuweka mkakati ambao utamsaidia ili mwakani aanze shule na sio shule ya kutwa kama ilivyokuwa ile aliyochaguliwa, ni vyema atafutiwe shule ya kulala ili aweze kutulia huko na asome kukidhi matakwa yake,” alisema Makonda.
Alisema kama atasoma shule ya kutwa, itamfanya akumbane na changamoto mbalimbali, kama vile kutafuta usafiri wa daladala kwenda shule na kurejea nyumbani na pia inaweza kuwa ni gharama zaidi ya kusoma shule ya bweni.
“Ni kweli aliweza kuhimili changamoto hizo kwa miaka mitatu, lakini ili aweze kutimiza kiu yake ya kusoma ni vyema kwenda shule ya bweni,” alisema Makonda.
Aliongeza kuwa kama atakuwa tayari, awasiliane naye kwa kusaidiwa na gazeti hili. Hata hivyo, Makonda alisema yapo mambo mengi katika jamii, yanayochangia watoto kushindwa kutimiza malengo yao, ikiwa ni pamoja na kuwepo wenye mfumo dume, wakiamini sio vyema kwa mtoto wa kike kusoma na umaskini, ambao husababisha wazazi kuwaozesha watoto wao.
Alisema kwa upande wa Rehema, yumkini hawakutoa taarifa hata kwa uongozi wa mtaa na ni vyema kutambua kuwa kusema ndio sehemu sahihi ya mwenye kutafuta msaada kuweza kusaidiwa.
Kwa miaka yote mitatu, Rehema amekuwa nyumbani, akiwaza kuwa ipo siku atasoma na hiyo ni moja ya sababu ya yeye kukataa kuozwa, kwa kuwa anaamini ipo siku atasoma na elimu hiyo itakuwa mkombozi kwake. 

KIM KARDASHIAN AONDOA KESI YA WIZI MAHAKAMANI.

Kim Kardashian West

Nyota wa uigizaji katika televisheni Marekani Kim Kardashian West ameondoa mahakamani keshi dhidi ya tovuti ya habari za udaku ya MediaTakeOut.
Alikuwa ameishtaki tovuti hiyo kwa kudai kwamba aliigiza kisha ambapo aliporwa vito hotelini Paris.
Lakini sasa mawakili wake wanasema wameafikiana na tovuti hiyo kutatua mzozo huo nje ya mahakama.
Tovuti hiyo ya MediaTakeOut pia imechapisha taarifa ya kuomba msamaha.
Rue Tronchet
Kando na kudai kwamba Kim Kardashian alikuwa ameigiza wizi huo, tovuti hiyo pia ilidai kwamba alikuwa amewasilisha ombi la ulaghai la malipo ya bima kuhusiana na vito vyake vya mamilioni ya dola vilivyoibwa.
Polisi mjini Paris walisema watu wawili wenye silaha, waliokuwa wamevalia mavazi ya polisi, waliiba sanduku lililokuwa na vito vya Kim Kardashian West vya thamani ya hadi o $6.7m (£5.2m).
Mumewe Kardashian West, Kanye West, ambaye alikuwa akitumbuiza New York wakati wa kutekelezwa kwa vizi huo, alikatiza utumbuizaji wake.
Baadhi wamesema huenda nyota huyo wa uigizaji alijichongea mwenyewe kwa kufichua eneo alimokuwa akiishi na hata kupakia mtandaoni picha za vito alivyokuwa navyo siku chache kabla ya kuvamiwa na wezi ao.
Tangu wakati huo, amekuwa kimya sana mitandao ya kijamii.

TIZAMA VIDEO MPYA KUTOKA WCB......MUGACHELELE BY QBOY ft RAYVANN, SHETTA.