Wednesday, October 26, 2016

RAIS MAGUFULI AONGOZA KATIKA TUZO ZA FORBES.

Rais John Magufuli
Jarida maarufu la Forbes limewateua viongozi mbalimbali watano wa Afrika akiwemo Rais John Magufuli, kuwania Tuzo ya Heshima ya Forbes Afrika Mwaka 2016 (Forbes Africa’s Person Of The Year 2016), na upigaji kura umeanza huku Dk Magufuli akiongoza kwa zaidi ya asilimia 70 ya kura.
Jarida hilo maarufu nchini Uingereza, lilifungua kazi ya upigaji kura na hadi jana jioni, kati ya viongozi hao watano, Rais Magufuli alikuwa akiongoza kwa wingi wa kura. Tuzo hiyo hutolewa kwa kiongozi au mtu binafsi aliyejitoa kwa kuhakikisha analeta manufaa ya kibiashara kwa wanaomzunguka.
Kwa mwaka huu, walioteuliwa kuwania tuzo hiyo wako watano ambao ni pamoja na Rais Magufuli, ambaye ameteuliwa kuwania tuzo hiyo kutokana na mapambano yake ya kuinua uchumi wa nchi.
Tangu aingie madarakani takribani mwaka mmoja sasa, Dk Magufuli amesimamia uadilifu katika utumishi wa umma na kurejesha utendaji kazi wenye ufanisi, lakini akiziba mianya ya rushwa na upotevu wa mapato na kuwezesha kuongezeka kwa makusanyo ya kodi na hivyo uchumi wa Tanzania kuendelea kukua kwa kasi.
Wateuliwa wengine katika tuzo hiyo ni Mwanzilishi wa Benki ya Capitec ya Afrika Kusini, Michiel Le Roux aliyefanya benki hiyo kuwafikia wananchi wengi nchini humo; Mwendesha Mashtaka wa Umma, Thuli Madonsela wa Afrika Kusini aliyekabiliana na vitisho vya kifo akitetea haki.
Pia yupo Rais wa Mauritius, Ameenah Gurib anayepambana kulinda mazingira nchini mwake.
Aidha, walioteuliwa wengine ni wananchi wa Rwanda kwa hatua iliyofikiwa na serikali ya nchi hiyo kwa ajili ya kupigania usawa wa kijinsia.
Forbes kupitia mtandao wa poy2016.com hadi jana jioni ulikuwa umefunguliwa na kazi ya kupiga kura ikiendelea huku Dk Magufuli akiongoza kwa asilimia 72 ya kura.
Watu wa Rwanda walifuatia kwa asilimia 21, Madonsela alifuatia kwa asilimia nne huku Gurib na Roux wakiwa na asilimia mbili kila mmoja hadi jana jioni.
Tuzo ya Heshima ya Forbes Afrika 2016 kwa mwaka huu itatolewa Novemba 11 jijini Nairobi nchini Kenya.
Kwa mwaka jana tuzo hiyo ilinyakuliwa na Mtanzania, mfanyabiashara Mohammed Dewji ambaye ni Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Mohammed Enterprises (MeTL).


Tuzo hizo zilianza kutolewa mwaka 2011 na tangu kutolewa kwake zimekuwa zikiwavutia watu mashuhuri na waliofanya mengi katika kukuza uchumi wao na mataifa yao.

No comments: