Tuesday, October 25, 2016

MAKONDA: NITAMSAIDIA REHEMA KUTIMIZA NDOTO ZAKE ZA KUWA MWALIMU.



Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amesema yuko tayari kumsaidia Rehema Mwilu (16) ili atimize ndoto yake ya kusoma na kuwa mwalimu, baada ya kushindwa kufanya hivyo kutokana na umasikini wa wazazi wake.
Rehema ni binti anayeishi Mtoni Kijichi Dar es Salaam, alihitimu elimu ya msingi katika Shule ya Mtoni Kijichi mwaka 2013 na kufaulu na alichaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza katika Shule ya Sekondari ya Kibada.
Lakini, alishindwa kuripoti shuleni kutokana na ugumu wa maisha na shule kuwa mbali, hali iliyosababisha aendelee kukaa nyumbani hadi leo. Baada ya kukaa nyumbani kwa muda, alitokea mwanaume aliyezungumza na wazazi wake na kupeleka barua ya posa na wazazi waliridhia Rehema kuolewa, kutokana na kutokuwa na pa kwenda, lakini alikataa kwa kuwa malengo yake yalikuwa ni kusoma.
Akizungumzia suala hilo, Makonda alisema ipo haja ya kujipanga kuona ni kwa namna gani Rehema ataweza kusaidiwa kusoma na kutimiza ndoto zake na aweze kusoma shule ya kulala ili kuepuka usumbufu.
“Ni kweli anahitaji msaada, lakini nitajitahidi kuweka mkakati ambao utamsaidia ili mwakani aanze shule na sio shule ya kutwa kama ilivyokuwa ile aliyochaguliwa, ni vyema atafutiwe shule ya kulala ili aweze kutulia huko na asome kukidhi matakwa yake,” alisema Makonda.
Alisema kama atasoma shule ya kutwa, itamfanya akumbane na changamoto mbalimbali, kama vile kutafuta usafiri wa daladala kwenda shule na kurejea nyumbani na pia inaweza kuwa ni gharama zaidi ya kusoma shule ya bweni.
“Ni kweli aliweza kuhimili changamoto hizo kwa miaka mitatu, lakini ili aweze kutimiza kiu yake ya kusoma ni vyema kwenda shule ya bweni,” alisema Makonda.
Aliongeza kuwa kama atakuwa tayari, awasiliane naye kwa kusaidiwa na gazeti hili. Hata hivyo, Makonda alisema yapo mambo mengi katika jamii, yanayochangia watoto kushindwa kutimiza malengo yao, ikiwa ni pamoja na kuwepo wenye mfumo dume, wakiamini sio vyema kwa mtoto wa kike kusoma na umaskini, ambao husababisha wazazi kuwaozesha watoto wao.
Alisema kwa upande wa Rehema, yumkini hawakutoa taarifa hata kwa uongozi wa mtaa na ni vyema kutambua kuwa kusema ndio sehemu sahihi ya mwenye kutafuta msaada kuweza kusaidiwa.
Kwa miaka yote mitatu, Rehema amekuwa nyumbani, akiwaza kuwa ipo siku atasoma na hiyo ni moja ya sababu ya yeye kukataa kuozwa, kwa kuwa anaamini ipo siku atasoma na elimu hiyo itakuwa mkombozi kwake. 

No comments: