Friday, September 16, 2016

HILLARY CLINTON AENDELEA NA KAMPENI BAADA YA KUUGUA.

Mgombea kupitia chama cha Democratic, Hillary Clinton.

Mgombea Urais kupitia chama cha Democratic nchini Marekani, Hillary Clinton amerejea katika kampeni baada ya kuugua homa ya mapafu.

Akiongea na mwandishi wa habari akiwa kwenye ndege kuelekea Greensboro North Carolina, Clinton alisema anajisikia vizuri baada ya mapumziko ya siku tatu.

Mpinzani wake wa chama cha Republican, Donald Trump ametoa barua kutoka kwa daktari wake kuonesha kuwa ana afya njema.

Barua hiyo inaonesha anatumia dawa ili kupunguza unene na kiwango kilichopitiliza cha uzito, lakini hatumii kilevi wala kuvuta sigara.

Uchaguzi wa Marekani utafanyika mwezi Novemba ambapo kampeni zake zimekuwa na vuta nikuvute kutoka vyama vikubwa viwili vya Democratic na Republican.


MANJI KUKODISHWA YANGA KWA MIAKA 10 KUANZIA OKTOBA.

Mwenyekiti wa Yanga, Yusuf Manji anatarajiwa kukabidhiwa timu hiyo baada ya mchezo wao wa ligi kuu na Simba, Oktoba mosi mwaka huu.

Habari zilizopatikana jana zinasema, bodi ya wadhamini wa Yanga chini ya Fatuma Karume na Francis Kifukwe imeridhia kumkodisha rasmi Manji timu hiyo kwa miaka 10 kama alivyoomba kupitia mkutano wa dharura wa wananchi wa klabu hiyo uliofanyika Juni 11 mwaka huu kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee, jijini Dar es salaam.

Manji aliomba apewe klabu hiyo kwa miaka 10 ambapo katika kipindi hiko atakuwa anachukua asilimia 75 ya mapato ya timu huku asilimia 25 ikibaki kwa wanachama, ambapo pia katika ukodishwaji huo timu ya soka na nembo ya klabu zote zitakuwa chini ya kampuni zake.

"Mkinikodisha ndani ya miaka mitatu nitahakikisha naingiza faida na asilimia 25 ya faida itaenda kwa wanachama wa klabu, ikiwa ni hasara nitabeba mimi na baada ya miaka kumi nitawarudishia klabu yenu, muanze kununua hisa" alisema Manji.


WABUNGE WA CUF HAWAMTAMBUI LIPUMBA.

Wabunge wote wa chama cha wananchi (CUF)  wametangaza rasmi kutomtambua aliyekuwa  mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba.

Wamemtaka msajiri wa vyama vya siasa nchini, Jaji Francis Mutungi kutomkumbatia mwanasiasa huyo aliyebobea katika uchumi, akielezwa kwa sasa hana sifa za kuwa mwenyekiti, labda aanze upya mchakato.

Wameeleza msimamo huo jana mjini Dodoma na Mbunge wa viti maalum, Riziki Mngwali ambaye pia ni kiongozi wa wabunge wa CUF katika mkutano baina ya waandishi wa habari za bunge na wabunge wa CUF isipokuwa mbunge wa jimbo la Kaliua, Magreth Sakaya aliyesimamishwa uanachama.

Mngwali alisema Lipumba amekuwa akikiyumbisha chama na hivi karibuni kudai amekaririwa akisema anasubiri barua ya msajili wa vyama vya siasa ya kuthibitishiwa kuendelea na uenyekiti wake.

"Wakati anajiuzuru uenyekiti Agosti 5 mwaka jana alitangazia umma na kudai anakwenda Rwanda kwa kazi aliyodai ya utafiti ili asaidie serikali, lakini inashangaza sasa anataka kujirejeshea uenyekiti, hilo hatukubali kwa kuwa chama kina taratibu zake" alisema.


Thursday, September 15, 2016

TRUMP AKATISHWA KUTOA HOTUBA NA MCHUNGAJI BAADA YA KUANZA KUMKASHIFU MGOMBEA MWENZAKE CLINTON.

Mchungaji wa kanisa moja la watu weusi katika jimbo la Michigan, Marekani amemkatisha Donald Trump akihutubia alipoanza kumshutumu mpinzani wake Hillary Clinton.

Mchungaji Faith Green Timmons alimkatisha Trump alipomshutumu mgombea huyo wa chama cha Democratic kuhusu mikataba ya kibiashara.

"Trump nilikualika hapa uje utushukuru kwa juhudi ambazo tumefanya Flint, si kutoa hotuba ya kisiasa" alisema mchungaji huyo wa kanisa la Bethel United Methodist.

Trump aliendelea na kuzungumza kwa kifupi kuhusu kutatua tatizo la maji safi Flint, lakini baadhi ya watu kwenye umati wakaanza kumzomea.

Mwanamke mmoja alisema kwa sauti kwamba mfanyabiashara huyo tajiri alitumia njia za kibaguzi katika kampeni yake.

Mfanyabiashara huyo alimjibu "haiwezekani umekosea, nisingeweza kufanya hivyo".

Mchungaji huyo aliingia tena na kuwashutumu waliokuwa wanamzomea Trump na kusema "yeye ni mgeni katika kanisa langu na inabidi mumuheshimu".

Trump mwishowe alilazimika kukatiza ghafla hotuba yake ambayo ilidumu kwa dakika sita hivi.


MWANAMKE AKAMATWA KWA KUIBA MTOTO MWENYE SIKU 10.

Polisi mkoani Morogoro inamshikilia Anna Luambano (33) ambaye ni mkazi wa Kipawa jijini Dar es salaam kwa tuhuma za wizi wa mtoto Angel Meck mwenye umri wa siku 10 baada ya kumlaghai mama wa mtoto huyo Maimuna Mohammed mkazi wa Chamwino katika manispaa ya Morogoro.

Kamanda wa polisi wa mkoa Ulrich Matei amesema wizi huo ulitokea Septemba 13, saa tano asubuhi katika mtaa wa Kilimahewa manispaa ya Morogoro.

Akielezea mazingira ya wizi huo, Kamanda Matei alisema mtuhumiwa alimdanganya mama wa mtoto huyo wakiwa njiani kutoka kituo cha Afya Mafiga, akimwomba ampe mtoto wake akamwoneshe mume wake kuwa huyo ni mtoto wa mdogo wake, ambaye amejifungua ili awape fedha za hongera kisha wagawane.

Amesema mtuhumiwa huyo baada ya kupewa mtoto alipotea katika mazingira ya kutatanisha.

Mama mtoto baada ya kugundua kuwa ameibiwa alienda kutoa taarifa kituo cha polisi. Ndipo polisi walipoanza kufanya msako kwenye mabasi yote ya abiria yanayosafiri maeneo mbalimbali na kufanikiwa kumkamata mtuhumiwa katika basi la Upendo eneo la Mdaula mkoani Pwani akienda mkoani Dar es salaam.

Mtuhumiwa alikiri na kusema hakuwa na nia mbaya bali alitaka kwenda kumlea huyo mtoto.


LOWASA AMKOSOA RAIS MAGUFULI.

Lowassa

Kiongozi wa upinzani nchini Tanzania Edward Lowasa amemkosoa mpinzani wake rais Magufuli kwa kile alichokitaja ni udikteta nchini humo.

Akizungumza na mwandishi wa BBC nchini Kenya, alisema kuwa alitarajia kwamba Magufuli angeondoa urasimu serikalini lakini kuna mambo mengi hayajakwenda sawa, japokuwa alikataa kutoa mifano alipotakiwa kufanya hivyo.

Lowasa alikuwa katika chama tawala alipokuwa Waziri Mkuu, lakini mwaka uliopita alijiunga na upinzani wa CHADEMA ambapo alishindwa na Rais Magufuli wakati wa uchaguzi.

Magufuli alipewa jina tinga (Bulldozer) anajulikana kufanya maamuzi yanayopendwa tangu achukue madaraka mwaka uliopita, kama vile kufutilia mbali sherehe za Uhuru ili kuhifadhi pesa.


Wednesday, September 14, 2016

VIDEO YA WIMBO WA RARUA WA MALAIKA WAZUA UTATA.

Malaika

Wiki iliyopita video ya wimbo wa Rarua wa mwanamziki Malaika ulitoka huku Hanscana akiwa ni director wa video hiyo.

Taharuki imetokea pale ambapo aliyekuwa mpenzi wa Malaika, kijana Eddy ambaye siku za nyuma alikataza nyimbo hiyo kutoka, kutokana na kulipa gharama zote lakini Malaika akamzingua kwa kumshitaki polisi kuwa alimtishia maisha.

Leo katika kipindi cha XXL kinachorushwa na Clouds Fm, Eddy alisikika kwenye Uheard akisema wimbo huo haukutakiwa kutoka na walikubaliana na Hanscana wasitoe nyimbo hiyo mpaka watakapokubaliana.

Lakini wimbo umetolewa na Eddy katishia kuufunga kwani umetolewa bila makubaliano na yeye ndiye aliyegharamia wimbo mzima.