Monday, September 5, 2016

DODOMA- WATOTO WA MITAANI KUONDOLEWA.

Dodoma

Serikali mkoani Dodoma itafanya operesheni ya kuwaondoa watoto wa mitaani, ambao wamekuwa kero kwa wapita njia na wateja wanaokula hotelini, ambao huwanyang'anya chakula na hata vinywaji wateja.

Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Christine Mndeme alisema watawaondoa watoto hao kutokana na kuwa hatari kwa maisha ya watu wengine. Mndeme alisema watoto hao wamekuwa wakikaa makundi na kuvuta dawa za kulevya aina ya gundi na wamekuwa wakiingia kwenye hoteli na kunyang'anya wateja chakula na vinywaji vyao.

"Idara ya maendeleo ya jamii itaanza kuwaondoa watoto wa mtaani wanaovuta bangi na petroli" alisema.

Alisema watoto hao wamekuwa wakikaa kwenye makundi na kuwa tishio kwa wapita njia hasa nyakati za jioni kutokana na kujihusisha na uhalifu.

"Tutazitambua familia za watoto hao wanapotoka, watarudishwa wanapotoka na wengine watapelekwa shuleni" alisema Mndeme.

Alisema wanachukua hatua hiyo kwa umakini ili watoto watakaoondolewa wasirudi tena mitaani, kwani inaonesha miaka ya nyuma lilifanyika lakini baada ya mda watoto hao walirudi tena mtaani.


No comments: