Thursday, October 20, 2016

MTANZANIA KUIWAKILISHA AFRIKA KWENYE SHINDANO LA MAPISHI.

Mkazi wa Kinondoni jijini Dar es Salaam, Fred Uisso anatarajiwa kuiwakilisha Afrika kwenye fainali za mashindano ya upishi duniani zinazotarajiwa kufanyika Novemba 8 hadi 15, mwaka huu huko Alabama, Marekani baada ya kufanya vizuri katika upishi wa nyama na mkate wa kuchanganya.
Uisso, Mtanzania anayefanya kazi katika mgahawa wa Afrikando uliopo Kinondoni, atakuwa Mwafrika wa kwanza kupata nafasi ya kushiriki katika mashindano hayo. Akizungumza jana wakati wa kukabidhiwa Bendera ya Taifa, Uisso alisema alipata nafasi hiyo baada ya kushiriki katika mchakato kupitia mitandao ya kijamii.
“Walinitambua kupitia kazi zangu ambazo nilizifanya mtandaoni katika dunia nzima tulikuwa zaidi ya watu 3,700 na kila mmoja alionesha uwezo wake wa kupika vyakula mbalimbali, tukachujwa tukabaki 100 na baadaye hadi 21,” alisema.
Alisema kushiriki mashindano hayo ni moja ya mwanga wa ndoto zake. Anatarajiwa kuondoka nchini Oktoba 28, baada ya kupata udhamini na ubalozi kupitia Kampuni ya usindikaji matunda na mboga ya Redgold.
Mshindi wa jumla kwenye mashindano hayo atajinyakulia dola za Marekani 100,000 (Sh milioni 210) na mshindi wa kila kipengele atajishindia dola 10,000 (Sh milioni 21).
Akizungumza kwa niaba ya serikali, Ofisa Uhusiano wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Geofrey Tengeneza alisema ni jambo la kujivunia kwa Mtanzania huyo kuwakilisha Afrika na kumtaka kutumia fursa hiyo kwenda kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo nchini. Uisso atachuana na wapishi kutoka mataifa mengine ikiwemo Haiti, Ukraine, Marekani, Canada na Puerto Rico.

No comments: