Mahakama ya Wilaya ya Ilala, Dar es Salaam jana imefuta na kumsomea upya mashitaka ya unyang’anyi wa kutumia silaha, mshitakiwa Salum Njwete (34) maarufu kama Scorpion anayedaiwa kumtoboa macho Said Mrisho.
Hata hivyo, mshitakiwa huyo alikana kuitwa Scorpion na kuieleza mahakama kuwa anaitwa Salum Njwete Salum.
Awali, saa 3:30 asubuhi, mshitakiwa huyo alipandishwa kizimbani mbele ya Hakimu Mkazi, Adelf Sachore ambapo Wakili wa Serikali, Munde Kalombola aliiomba mahakama hiyo kuondoa mashitaka hayo kwa sababu hawana nia ya kuendelea na kesi hiyo.
Kalombola alidai kuwa wameomba kufuta mashitaka hayo kwa kuzingatia kifungu namba 91 kifungu kidogo cha kwanza cha Sheria ya Makosa ya Jinai.
Katika kifungu hicho, kinampa mamlaka Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) kuondoa mashitaka mahakamani muda wowote ili mradi kama kesi hiyo haijatolewa hukumu lakini pia kinampa mamlaka DPP kumshitaki mshitakiwa endapo kama ana nia ya kuendesha mashitaka hayo. Kutokana na maombi hayo, Hakimu Sachore alikubaliana na maombi hayo na mshitakiwa alirudishwa mahabusu.
Hata hivyo, mshitakiwa huyo alitolewa mahabusu akiwa chini ya ulinzi mkali wa polisi huku akiwa amevalia kanzu na baraghashia na kupandishwa kizimbani mbele ya Hakimu Mkazi, Flora Haule na kusomewa mashitaka ya unyang’anyi wa kutumia silaha kinyume na kifungu cha 287 (a) cha Sheria ya kanuni ya adhabu.
Akisoma mashitaka hayo, Wakili wa Serikali, Chesensi Gavyole alidai mshitakiwa alitenda makosa hayo Septemba 6 mwaka huu, maeneo ya Buguruni Sheli wilayani Ilala. Alidai kuwa mshitakiwa aliiba cheni ya silver yenye gramu 38 ikiwa na thamani ya Sh 60,000, bangili ya mkononi, fedha taslimu Sh 331,000 pamoja na pochi vyote vikiwa na thamani ya Sh 476,000, mali ya Said Mrisho.
Pia alidai kabla na wizi huo alimtishia mlalamikaji (Mrisho) na kisha kumchoma kisu machoni, tumboni na mabegani ili kujipatia vitu hivyo.
Wakili Gavyole, alidai kuwa upelelezi wa mashitaka hayo haujakamilika na kuomba mahakama ipange tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.
Mshitakiwa huyo pia alikana mashitaka hayo na Hakimu Haule aliiambia mahakama kuwa kwa mujibu wa Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, kifungu cha 148 kifungu kidogo cha 5 (a) mashitaka hayo hayana dhamana, hivyo mshitakiwa alitakiwa kurudi rumande na kuahirisha kesi hiyo hadi Novemba 2, mwaka huu itakapotajwa.
No comments:
Post a Comment