Thursday, October 20, 2016

WANAOANZA DARASA LA KWANZA MWAKA 2017 KWENDA NA MCHE MMOJA WA MTI

Serikali imeagiza halmashauri zote nchini kuhakikisha kuanzia mwakani kila mwanafunzi anayeanza darasa la kwanza katika shule za serikali na binafsi afike shuleni kwake na mche mmoja wa mti.
Aidha, imebainisha kuwa kwa upande wa shule za sekondari kila mwanafunzi atapaswa kwenda na miche mitatu wakati wa kuanza masomo.
Hayo yalisemwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, January Makamba wakati akishiriki katika upandaji miti na wanafunzi katika Shule ya Msingi Mlandege iliyopo katika Kata ya Kwakilosa, Manispaa ya Iringa ambako aliongozana na viongozi mbalimbali wa mkoa huo wa Iringa jana.
Alisema agizo hilo ni kwa mujibu wa Ofisi ya Makamu wa Rais, Mazingira na linapaswa kutekelezwa mara moja; na kwamba maelekezo ya agizo hilo yatapelekwa Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa. “...Kuanzia mwakani kila mwanafunzi wa darasa la kwanza akiripoti atatakiwa kuja na mche wa mti na ataupanda na kuutunza kwa miaka yote saba na hatapewa cheti cha kumaliza darasa la saba kabla hajaonyesha mti wake,” alisisitiza January.
Alisema katika shule zenye maeneo madogo, miti hiyo itapandwa kwenye maeneo yatakayoelekezwa na Serikali za Vijiji na Mitaa.
“Kuanzia Novemba 5 hadi 6 tumewaita wakuu wa wilaya, wakurugenzi na wenyeviti na mameya wote Arusha, kwa ajili ya kuwapa mafunzo na maelekezo mahsusi yanayohusu suala la hifadhi ya mazingira, ikiwemo upandaji miti na utunzaji wa vyanzo vya maji,” alisema.
Waziri huyo alisema lengo la kushiriki katika upandaji miti pamoja na wanafunzi hao ni kutuma ujumbe mahsusi na wa uhakika kwamba uhifadhi, usimamizi na utunzaji wa mazingira ni jukumu la msingi kwa manufaa ya kizazi kinachokuja na ndio sababu hasa ya kushiriki na wanafunzi ili waweze kujifunza na kuelewa.

No comments: