MKUU WA MKOA WA ARUSHA MRISHO GAMBO.
Rais John Magufuli amemhakikishia Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo kuwa taarifa zilizozagaa katika mitandao ya kijamii kuwa amemuengua ukuu wa mkoa wa Arusha, sio za kweli, kwani ni uzushi unaopaswa kupuuzwa.
Hayo yalisemwa na Gambo, wakati akitoa maelezo ya mwisho katika kikao cha wafanyabiashara wakubwa wa mkoani Arusha, aliokutana nao kusikiliza changamoto, zinazowakabili na kuzifanyia kazi ili waweze kufanya kazi bila wasiwasi.
Gambo aliwaeleza wafanyabiashara hao kuwa Rais amempigia simu na kumhakikishia kuwa yeye ndiye Mkuu wa Mkoa wa Arusha; na hakuna mabadiliko yoyote kwa sasa, labda afikirie kumpandisha cheo zaidi; na sio kumuengua katika nafasi hiyo.
Mkuu huyo alisema baada ya kuzungumza kwa simu na Rais, Rais aliomba kuongea na kiongozi wa chama cha wafanyabiashara wa Mkoa wa Arusha na akamkabidhi simu Mwenyekiti wa Chama hicho Mkoani Arusha, Wolter Maeda.
Maeda alikiri kuongea na Rais Magufuli na kusema kuwa Rais amemwambia kuwa Arusha, inatakiwa kuwa ya amani na utulivu na aliwaasa kufanya biashara bila ya wasiwasi na kulipa kodi inayostahili.
Alisema pia kuwa wafanyabiashara, wasiogope chochote na iwapo watendaji wa serikali yake, watakuwa wakifanya kazi kwa vitisho, wanapaswa kutoa taarifa mara moja kwa viongozi wa juu wa mkoa, kwani wanapaswa kulipa kodi inayostahili kwa mujibu wa sheria.
Gambo aliwataka wafanyabiashara Arusha, kushirikiana na kufanya kazi kwa malengo ya kukuza uchumi wa Mkoa wa Arusha na sio vinginevyo na aliwaahidi kutoa ushirikiano wa hali na mali. Alisema kila mkazi wa Mkoa wa Arusha, anapaswa kufanya shughuli zake kwa mujibu wa sheria ;na hakuna aliye juu ya sheria.
Aliwataka wananchi wa Arusha, kufuata kazi na kuacha siasa kwenye mambo ya msingi ya kukuza uchumi wa Mkoa wa Arusha.
‘’Mimi ndio Mkuu wa Mkoa wa Arusha na ninafanya kazi kwa mujibu wa sheria na wenye kufanya kazi ya siasa, wafanye siasa na sio kuingilia utendaji kazi wa kila siku wa watendaji wa serikali,’’alisema.
Kusamba kwa nakala ya barua ya Ikulu, kulizua mtafaruku katika Jiji la Arusha mchana kutwa wa jana, kwani baadhi walionesha kufurahishwa, lakini wengine walionekana kusikitishwa na utenguzi huo.
No comments:
Post a Comment