Staa wa Bongo anayetesa kwenye filamu, Kajala Masanja amevunja ukimya na kufunguka kuhusu maneno yanayozagaa mitaani yakimtaja kuwa kwenye uhusiano wa kimapenzi kwa nyakati tofauti na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda na mwanamuziki wa Bongo Fleva, Msamy Baby.
Kwa muda mrefu sasa, minong’ono hiyo imekuwa ikizagaa kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii tangu wakati Makonda akiwa Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni katika Serikali iliyopita ya Dk. Jakaya Kikwete.
Tetesi za uhusiano wake na RC Makonda, zilianza wakati Makonda (alipokuwa DC wa Kinondoni) akishirikiana na msanii huyo kwenye shindano la kusaka vipaji vya wasanii wa Wilaya ya Kinondoni lililojulikana kama Kinondoni Star Search.
Katika mahojiano na Polisi wa Swaggaz, Kajala alipoulizwa kuhusu madai ya kuwa na uhusiano na Makonda, alijibu kwa kifu sana: “Hapana sijawahi kutoka naye kabisa. Hilo halipo.”
Awali, RC Makonda aliwahi kuzungumzia madai hayo akiwa bado Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, ambapo alisema wabaya wake wa kisiasa wamekuwa wakisaka mbinu za kumchafua kila kukicha.
Makonda, alikwenda mbali zaidi akisema kuwa, propaganda ya kumchafua ilianza tangu wakati wa Bunge Maalum la Katiba, alipokwenda Bungeni na msanii mwingine wa filamu, Yobnesh Yusuf ‘Batuli’, akazushiwa kuwa alitoka naye.
Katika maelezo ya Makonda, alisema anawashangaa wengi wanavyomhusisha kuwa na uhusiano usiofaa na Kajala kwa vile ameshirikiana naye kwenye project hiyo ya kusaka vipaji wakati pia ameshirikiana na wasanii wengi wa kiume.
Kwa Kajala inakuwa mara ya kwanza kuzungumzia hilo katika mahojiano maalum na mwandishi wa Swaggaz.
Kuhusu msanii wa Bongo Fleva, Msami Baby Kajala alisema: “Hata huyo sijawahi kutembea naye, lakini nakiri kwamba ni rafiki yangu wa karibu kama msanii mwenzangu ila hatujawahi kuwa wapenzi hata siku moja.”
SWAGGAZ: Vipi kuhusu picha zilizozagaa kwenye mitandao ya kijamii zikiwaonesha wewe na Msami mkiwa sehemu mbalimbali za starehe?
KAJALA: Kwahiyo nikipiga picha na msanii basi natoka naye? Mtu unaweza kujisikia kupiga picha na yeyote kwa ajili ya kurusha Insta, kwahiyo ukifanya hivyo tu basi tayari unatoka naye?
Mfano leo (juzi Jumatano) nimepiga picha na Petty Man, kwahiyo nikiweka Insta basi itakuwa Kajala anatoka na Petty. Siyo jambo zuri, nadhani wangekuwa na uhakika kwanza, mimi sijawahi kutembea na Msami.
SWAGGAZ: Ok! Vipi kuhusu uhusiano wako na mzazi mwenzako P Funk kwa sasa?
KAJALA: Kawaida tu! Yeye ana maisha yake na mimi nina yangu, ameoa na mimi niko kivyangu.
SWAGGAZ: Umezungumzia upande wako, vipi kuhusu mwanenu Paula, anawasiliana na baba’ake?
KAJALA: Hapana na hiyo ni kwa sababu mtoto niko naye mimi.
SWAGGAZ: Kwahiyo tangu uachane na P Funk, mtoto hajawahi kwenda kumuona baba yake?
KAJALA: Aliwahi kwenda kipindi fulani na aliishi naye wakati huo, lakini nilipomchukua na kuishi naye hawajawahi kuonana naye tena.
SWAGGAZ: Labda P Funk amewahi kutaka kuonana na mwanaye?
KAJALA: Hapana… nadhani ni kwa kuwa ana watoto wengine anaona wanamtosha huyu hana haja naye. Lakini nisingependa kuendelea kuongelea hayo mambo tena.
SWAGGAZ: Vipi uhusiano wako na mumeo Faraji aliyeko gerezani? Je, huwa unakwenda kumtembelea?
KAJALA: Nilikuwa nakwenda kumwangalia lakini kwa sasa nisiwe muongo, nina muda kidogo kutokana na kazi za hapa na pale, nimejikuta sijaenda kumuona lakini mwanzo nilikuwa nakwenda kila Jumamosi na Jumapili.
SWAGGAZ: Mara ya mwisho kwenda ilikuwa lini?
KAJALA: Mwezi mmoja umepita sasa.
SWAGGAZ: Vipi mipango yako ya kiuhusiano? Maana mumeo yupo jela. Utamsubiri atoke muendelee na uhusiano wenu au unatarajia kuingia kwenye ndoa mpya? Nimekuuliza hili kwa sababu hivi karibuni ulisema unatamani kupata mtoto wa kiume.
KAJALA: Hiyo siwezi kuongelea in public (hadharani) kwa sababu ni maisha yangu binafsi.
SWAGGAZ: Ahsante sana kwa ushirikiano wako.
KAJALA: Nawe pia karibu tena.