Wakati klabu ya Liverpool ikiwa kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu England (EPL), ushindani wa timu gani itaibuka bingwa mpya ifikapo Mei mwakani umeongezeka kuliko ilivyokuwa mwaka jana.
Kipigo cha mabao 6-1 ilichokitoa kwa Watford, Jumapili kilitosha kuiweka kileleni Liverpool ikiwa na pointi 26 na kufuatiwa na Chelsea yenye pointi 25 baada ya Jumamosi kuiadhibu Everton 5-0. Hizo, zinafuatiwa na Manchester City, Arsenal, zenye pointi 24, timu mbili zilizozuiwa na wapinzani wao, Middlesbrough na na Tottenham kwa sare ya bao 1-1, zinafuatiwa na Spurs yenye pointi 21.
Ligi hiyo itasimama mwishoni mwa wiki ili kupisha michezo ya kimataifa, imeshuhudia mabadilio ya uongozi wake wa juu baada ya Manchester City iliyoanza vyema kwa ushindi wa mechi saba kupoteza mwelekeo kwenye mechi kadhaa zilizopita.
Chelsea yenye kiwango bora kwa sasa ikiwa chini ya kocha Antonio Conte imerejesha ushindani ilioupoteza msimu uliopita.
Ndani ya saaa 24, siku za Jumamosi na Jumapili zilishuhudia uongozi wa ligi hiyo ukihama kutoka City, Chelsea, hadi Liverpool. Lakini, vijana wa kocha Jurgen Klopp, Liverpool wanaocheza vizuri msimu huu wataiongoza ligi hiyo hadi Novemba 19.
Klopp alihitimisha mafanikio ya klabu yake akiesema: “Tuliwaangalia Chelsea, walicheza vizuri. Manchester City walicheza vizuri dhidi ya Barcelona. Tusiwadharau Manchester United. Tottenham ni timu nzuri. Kwa jumla, ligi ina timu nzuri.”
Tofauti ya pointi mbili kati ya Liverpool, Chelsea, City na Arsenal kileleni mwa ligi inatosha kuwa ushahidi mwingine wa ushindani ambao umeshika kasi mapema, ingawa Spurs na United, pia zinanyemelea, endapo timu yoyote iliyoko juu ikiteleza, zenyewe zitapanda juu.
Ni nafasi gani timu yako inapewa kutwaa ubingwa EPL?
Liverpool
Kwa sasa ndiyo vinara wa EPL, wana kasi inayobebwa na washambuliaji wakali walioiangamiza Watford Jumapili.
Tangu Agosti mwaka jana, Klopp hajaonja uchungu, anaiongoza timu inayofunga mabao mengi itakavyo ana imani ya mashabiki kuendelea kutamba msimu huu.
Sare dhidi ya Manchester United mwezi uliopita ilitibua ushindi wake wa asilimia 100, ingawa klabu hiyo ya Anfield inajiamini kuwa itaendeleza makali.
Inakabiliwa na mechi zijazo: Southampton (ugenini), Novemba 19; Sunderland (nyumbani), Novemba 26; Bournemouth (ugenini), Desemba 4; West Ham (nyumbani), Desemba 11; Middlesbrough (ugenini), Desemba 14; Everton (ugenini), Desemba 19.
Alama: 8/10
Chelsea
Kocha Conte ameibadili klabu hiyo ya Stamford Bridge kuwa mshindani wa kweli kwa kuondoa udhaifu wa msimu uliopita na kuwa moto wa kuotea mbali, ikitumia mfumo mpya wa 3-4-3.
Tangu ianze kutumia mfumo huo, Chelsea haijapoteza mchezo, kufungwa bao, imefunga mabao 16 kwenye mechi tano, ambako kiungo Eden Hazard na mshambuliaji Diego Costa wanatisha.
Mechi zijazo zitakuwa baina ya Middlesbrough (ugenini), Novemba 20; Tottenham (nyumbani), Novemba 26; Manchester City (ugenini), Desemba 3; West Brom (nyumbani), Desemba 11; Sunderland (ugenini), Desemba 14; Crystal Palace (ugenini), Desemba 17.
Alama: 8.5/10
Manchester City
Baada ya kuilaza Barcelona 3-1 kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya ilidhaniwa kuwa Manchester City imeimarika, lakini Jumamosi ilizuiwa na Middlesbrough kwa bao la dakika za majeruhi.
Rekodi ya ushindi wa mechi sita za kwanza imeanza kupotea, kocha Pep Guardiola amepata ushindi mmoja pekee kwenye mechi tano zilizopita. Ni wazi kuwa Manchester City bado inao uwezo wa kushinda taji, lakini lazima ipigane
Mechi zijazo: Crystal Palace (ugenini), Novemba 19; Burnley (ugenini), Novemba 26; Chelsea (nyumbani), Desemba 3; Leicester City (ugenini), Desemba 10; Watford (nyumbani), Desemba 14; Arsenal (nyumbani), Desemba 18.
Alama: 6.5/10
Arsenal
Sare ya 1-1 dhidi ya Tottenham Jumapili ulimwacha kocha Arsene Wenger akiwa mwenye hasira na kukosa nafasi ya kukaa kileleni, ikiwa imepata sare mbili kwenye mechi mbili kati ya tano.
Inao Alexis Sanchez na Mesut Ozil ambao wanang’ara msimu huu, imempata tena Olivier Giroud akiwa na kiwango kizuri, kiasi cha kuongeza chachu kwenye safu yao ya ushambuliaji. Msimu huu, Arsenal imeimarika zaidi kwenye ulinzi.
Safari ya kwenda Old Trafford ambako Wenger atakutana na mbabe wake, Jose Mourinho ni kipimo kingine cha ukakamavu wa Arsenal msimu huu. Pia, lazima Arsenal iweke kando matokeo mabaya ya mwezi Novemba, ambao umekuwa mbaya kwake kwa miaka mingi.
Mechi zijazo: Manchester United (ugenini), Novemba 19; Bournemouth (nyumbani), Novemba 27; West Ham (ugenini), Desemba 3; Stoke (nyumbani), Desemba 10; Everton (ugenini), Desemba 13; Manchester City (ugenini), Desemba 18.
Alama: 7/10
Tottenham
Hadi sasa, Spurs ndiyo pekee haijapoteza mechi EPL, lakini inakwenda mapumziko ya mechi za kimataifa ikiwa na ndoto ya kuifikia Liverpool ambayo imeipita kwa pointi tano.
Kocha Mauricio Pochettino hawezi kubadili sare ambazo Spurs imekuwa ikipata katika mechi zake za karibuni kuwa ushindi ili kuzikamata timu zilizo juu yake.
Kurejea uwanjani kwa Harry Kane, anayekaribia kuwa fiti na pengine atakuwa tayari kuiongoza safu ya ushambuliaji dhidi ya West Ham wiki mbili zijazo, Spurs inataka mageuzi.
Mechi zijazo: West Ham (nyumbani), Novemba 19; Chelsea (ugenini), Novemba 26; Swansea (nyumbani), Desemba 3; Manchester United (ugenini), Desemba 11; Hull (nyumbani), Desemba 14; Burnley (nyumbani ), Desemba 14.
Alama: 6/10
Manchester United
Ushindi wa kwanza katika mechi tano kwa kuilaza Swansee City mabao 3-1 Jumapili ulipoza vidonda ya mashabiki ambao hata hivyo hawana imani na kocha Jose Mourinho, bosi ambaye bado anauguza kidonda.
Alikuwa na wakati mgumu dhidi ya mabeki wake, Chris Smalling na Luke Shaw ambao aliwaeleza kuwa waoga wanapokaribia mechi. Pia, kiwango cha mshambuliaji wake mkongwe, Zlatan Ibrahimovic na kiungo Paul Pogba waliofunga mabao dhidi ya Swansea kinamfariji, ingawa lazima wakaze buti kwenye mchezo ujao dhidi ya Arsenal.
Mechi zinazofuata: Arsenal (nyumbani), Novemba 19; West Ham (nyumbani), Novemba 27; Everton (ugenini), Desemba 4; Tottenham (nyumbani ), Desemba 11; Crystal Palace (ugenini), Desemba 14; West Brom (ugenini), Desemba 17.
No comments:
Post a Comment