Polisi wawili wanaodaiwa kuwapiga na kuwadhalilisha wanafunzi wa Sekondari ya Isuto mkoani Mbeya, wamefukuzwa kazi.
Askari hao ni wale waliokuwa wakisimamia mitihani ya kidato cha nne katika shule hiyo ambao inaelezwa kuwa waliwashambulia wanafunzi wa kike kwa bakora na adhabu nyingine.
Waliofukuzwa kazi kutokana na tuhuma hizo ni Konstebo Petro Magana wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia Mkoa wa Mbeya na Konstebo Lukas Ng’weina wa Wilaya ya Kipolisi Mbalizi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Dhahir Kidavashari amesema kuwa licha ya askari hao kufukuzwa kazi, watafikishwa mahakamani wakati wowote ili sheria ichukue mkondo wake.
Polisi hao wamekumbwa na kashfa ya kuwacharaza bakora na kuwapa adhabu nyingine wanafunzi wa kike wa shule hiyo, baada ya jaribio lao la kutaka kufanya ngono na mabinti wawili wa shule hiyo kushindikana.
Kidavashari amedai kuwa Novemba 4, saa 5:00 usiku, askari hao walituhumiwa kuwafanyia vitendo vibaya kinyume cha maadili wanafunzi wa kike wa shule hiyo.
“Inadaiwa kuwa, askari hao kwa pamoja wakiwa kwenye ulinzi wa mitihani ya Taifa ya kidato cha nne waliwatoa kwenye hosteli wanafunzi wa kike kwa kile walichodai kupiga kelele, baada ya kuwatoa waliwapeleka eneo la kufoleni na kuanza kuwapa adhabu mbalimbali,” amedai kamanda huyo.
No comments:
Post a Comment