MAREHEMU JOSEPH MUNGAI. |
Waziri na Mbunge wa zamani wa Jimbo la Mufindi Kaskazini mkoani Iringa, Joseph Mungai (73) amefariki dunia baada ya kuugua ghafla.
Taarifa za kifo cha Mungai, zilianza kusambaa jana jioni majira ya saa 12 na baadaye Ofisa Uhusiano wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Aminiel Aligaesha alithibitisha kupokelewa kwa mwili wa kiongozi huyo wa zamani.
Aligaesha alisema Mungai hakuwa amelazwa hospitalini hapo, ila mwili wake ulipokelewa Idara ya Magonjwa ya Dharura na kuthibitishwa kuwa alifariki saa 11:20 jioni.
“Ni kweli tumepokea mwili wa Joseph Mungai katika idara yetu ya magonjwa ya dharura na kuthibitisha kifo saa 11:20jioni,” alisema Aligaesha. Aligaesha alisema mwili wa marehemu umehifadhiwa chumba cha kuhifadhi maiti Hospitali ya Taifa Muhimbili. Taarifa zaidi za chanzo cha kifo chake na mambo mengine, zitatolewa kesho.
Mungai alipata kuwa Waziri wa Kilimo katika Serikali ya Awamu ya Kwanza na Waziri wa Elimu kwa vipindi viwili vya mwaka 1972-1975 na 1980-1982. Mungai pia alikuwa Mwenyekiti wa Baraza la Michezo la Taifa mwaka 1976-1980. Pia aliwahi kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Ndege Tanzania (ATC), ambalo sasa ni ATCL.
Katika Serikali ya Awamu ya Tatu, Joseph Mungai alipata kuwa Waziri wa Elimu na Utamaduni. Mungai alishiriki kuanzisha Mfuko wa Elimu wa Mufindi, ambao umefanikiwa kusomesha watoto wengi wa wilaya ya Mufindi na hivi sasa vijana hao wanashika nyadhifa za juu serikalini, mashirika ya kimataifa na nje ya nchi.
Pia, Mungai alikuwa mstari wa mbele katika kuboresha kilimo na kuanzisha viwanda katika wilaya ya Mufindi, hatua ambayo imetatua tatizo la ajira kwa vijana wengi. Pia Mungai alishiriki kuanzisha Benki ya Wananchi wa Mufindi.
Kwa sasa Mufindi ni moja ya wilaya chache nchini, zilizopiga hatua kubwa katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Kwa upande wa elimu, Mungai alisoma katika Shule ya Sekondari Mkwawa mkoani Iringa, kisha kwenda Chuo cha Colorado na baadaye Chuo Kikuu cha Harvard nchini Marekani kwa masomo zaidi. Bwana Alitoa na Bwana Ametwaa. Jina la Bwana Lihimidiwe.
No comments:
Post a Comment