Thursday, October 20, 2016

TCU KUANZA KUSAJILI WANAFUNZI WA ELIMU YA JUU KWA AWAMU YA PILI NA YA MWISHO.

Image result for tcu image tanzania
Tume ya vyuo vikuu nchini (TCU), imefungua awamu nyingine ya udahili ili kuwapa nafasi wanafunzi ambao hawakuchaguliwa katika awamu zilizopita kutuma maombi upya.

Akizungumza na waandishi wa habari, Mkurugenzi wa Udahili na Nyaraka TCU Dk. Kokuberwa Mollel amesema awamu hiyo ya mwisho itakayodumu kwa siku tatu itaanza Oktoba 24 hadi 26.

Amesema udahili huo utahusisha waombaji waliokwisha tuma maombi yao lakini walishindwa kuchaguliwa kutokana na kukosa sifa za kuingia katika kozi walizoomba.

''Awamu hii itawahusisha wahitimu wa kidato cha sita, stashahada na sifa linganishi, wengi wao walishindwa kuchaguliwa kutokana na ushindani mkubwa katika programu walizoomba, kushindwa kukamilisha taratibu za uombaji na waombaji kukosa sifa kwa kozi walizoomba'' Alisema.

Hadi sasa wanafunzi 61590 wameshachaguliwa kujiunga na vyuo mbalimbali na wanafunzi 17717 wenye sifa za kujiunga na vyuo vikuu bado wapo kwenye mfumo wa uchakataji.

MGAO WA MKOPO KWA WANAFUNZI WA ELIMU YA JUU KUPITIWA UPYA.


Jumuiya ya wanafunzi wa Taasisi za Elimu ya juu Tanzania (TAHLISO), imekubaliana na Wizara ya Elimu kupitia upya mchakato wa mgao uliofanyika kwa mara ya kwanza ili kuondoa kasoro zilizojitokeza mara ya kwanza.

Mwenyekiti wa jumuiya hiyo, Stanslaus Kadugazile amesema makubaliano hayo yamefikiwa baada ya kukutana leo Alhamisi na viongozi wa Wizara hiyo pamoja na wahusika wanaopokea, kupanga na kutoa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu.

''Tumejadiliana juu ya changamoto zote zilizojitokeza kwenye mgao uliokwenda vyuoni pamoja na viwango vidogo vya fedha walizopangiwa wanafunzi kwa ajili ya chakula na malazi, vitabu na viandikwa pamoja na ada na kuona ipo haja ya kufanya marekebisho ya viwango hivyo vilivyopangwa kwa wanafunzi hao ili kuweza kukidhi mahitaji halisi kwa kila mwanafunzi anayestahili kupata mkopo na kutoa mgao mpya tofauti na wa kwanza''. Alisema.

MSAMI AELEZA SABABU ZA KUACHANA NA UWOYA.

 MSAMI
Mtu wangu kama wewe utakuwa ni mpenzi wa kufuatilia mahusiano ya mastaa basi penzi la Mrembo kutoka Bongomovie (Irene Uwoya) na Mkali kutoka Bongoflevani (Msami)  litakuwa sio penzi geni kwenye macho yako leo  October 19 2016 Msami ameweka wazi sababu za kuachana na Ireen Uwoya
kuachana kama kuachana mimi sioni kama tumeacha kwasababu mimi na Ireen bado tunawasiliana sema tu mimi niliona kuna vitu haviendi sawa nikaamua kukaa pembeni yaani sina sababu maalumu ila niliamua tu mwenyewe

WANAVYUO 66,000 WAKOSA MIKOPO.

Dar es Salaam. Ahadi iliyotolewa na Rais John Magufuli wakati wa kampeni mwaka jana kwamba katika Serikali yake hakuna mwanafunzi atakayekosa mkopo wa masomo ya elimu ya juu imekuwa ngumu kutekelezeka.
Uchunguzi wa Mwananchi umebaini kwamba kati ya wanafunzi 88,000 walioomba mikopo kutoka Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), wengi hawatapata.
Uwezo wa bodi hiyo ni kutoa mikopo kwa wanafunzi 21,500 pekee sawa na asilimia 24 na waliopatiwa hadi sasa ni wanafunzi 11,000 sawa na asilimia 12.
Takwimu hizi zinaonyesha kwamba zaidi ya robo tatu ya wanafunzi wanaohitaji mikopo watakosa kutokana na uwezo mdogo wa kifedha.

MTANZANIA KUIWAKILISHA AFRIKA KWENYE SHINDANO LA MAPISHI.

Mkazi wa Kinondoni jijini Dar es Salaam, Fred Uisso anatarajiwa kuiwakilisha Afrika kwenye fainali za mashindano ya upishi duniani zinazotarajiwa kufanyika Novemba 8 hadi 15, mwaka huu huko Alabama, Marekani baada ya kufanya vizuri katika upishi wa nyama na mkate wa kuchanganya.
Uisso, Mtanzania anayefanya kazi katika mgahawa wa Afrikando uliopo Kinondoni, atakuwa Mwafrika wa kwanza kupata nafasi ya kushiriki katika mashindano hayo. Akizungumza jana wakati wa kukabidhiwa Bendera ya Taifa, Uisso alisema alipata nafasi hiyo baada ya kushiriki katika mchakato kupitia mitandao ya kijamii.
“Walinitambua kupitia kazi zangu ambazo nilizifanya mtandaoni katika dunia nzima tulikuwa zaidi ya watu 3,700 na kila mmoja alionesha uwezo wake wa kupika vyakula mbalimbali, tukachujwa tukabaki 100 na baadaye hadi 21,” alisema.
Alisema kushiriki mashindano hayo ni moja ya mwanga wa ndoto zake. Anatarajiwa kuondoka nchini Oktoba 28, baada ya kupata udhamini na ubalozi kupitia Kampuni ya usindikaji matunda na mboga ya Redgold.
Mshindi wa jumla kwenye mashindano hayo atajinyakulia dola za Marekani 100,000 (Sh milioni 210) na mshindi wa kila kipengele atajishindia dola 10,000 (Sh milioni 21).
Akizungumza kwa niaba ya serikali, Ofisa Uhusiano wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Geofrey Tengeneza alisema ni jambo la kujivunia kwa Mtanzania huyo kuwakilisha Afrika na kumtaka kutumia fursa hiyo kwenda kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo nchini. Uisso atachuana na wapishi kutoka mataifa mengine ikiwemo Haiti, Ukraine, Marekani, Canada na Puerto Rico.

SCORPION AFUNGULIWA MASHTAKA MENGINE.

Mahakama ya Wilaya ya Ilala, Dar es Salaam jana imefuta na kumsomea upya mashitaka ya unyang’anyi wa kutumia silaha, mshitakiwa Salum Njwete (34) maarufu kama Scorpion anayedaiwa kumtoboa macho Said Mrisho.
Hata hivyo, mshitakiwa huyo alikana kuitwa Scorpion na kuieleza mahakama kuwa anaitwa Salum Njwete Salum.
Awali, saa 3:30 asubuhi, mshitakiwa huyo alipandishwa kizimbani mbele ya Hakimu Mkazi, Adelf Sachore ambapo Wakili wa Serikali, Munde Kalombola aliiomba mahakama hiyo kuondoa mashitaka hayo kwa sababu hawana nia ya kuendelea na kesi hiyo.
Kalombola alidai kuwa wameomba kufuta mashitaka hayo kwa kuzingatia kifungu namba 91 kifungu kidogo cha kwanza cha Sheria ya Makosa ya Jinai.
Katika kifungu hicho, kinampa mamlaka Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) kuondoa mashitaka mahakamani muda wowote ili mradi kama kesi hiyo haijatolewa hukumu lakini pia kinampa mamlaka DPP kumshitaki mshitakiwa endapo kama ana nia ya kuendesha mashitaka hayo. Kutokana na maombi hayo, Hakimu Sachore alikubaliana na maombi hayo na mshitakiwa alirudishwa mahabusu.
Hata hivyo, mshitakiwa huyo alitolewa mahabusu akiwa chini ya ulinzi mkali wa polisi huku akiwa amevalia kanzu na baraghashia na kupandishwa kizimbani mbele ya Hakimu Mkazi, Flora Haule na kusomewa mashitaka ya unyang’anyi wa kutumia silaha kinyume na kifungu cha 287 (a) cha Sheria ya kanuni ya adhabu.
Akisoma mashitaka hayo, Wakili wa Serikali, Chesensi Gavyole alidai mshitakiwa alitenda makosa hayo Septemba 6 mwaka huu, maeneo ya Buguruni Sheli wilayani Ilala. Alidai kuwa mshitakiwa aliiba cheni ya silver yenye gramu 38 ikiwa na thamani ya Sh 60,000, bangili ya mkononi, fedha taslimu Sh 331,000 pamoja na pochi vyote vikiwa na thamani ya Sh 476,000, mali ya Said Mrisho.
Pia alidai kabla na wizi huo alimtishia mlalamikaji (Mrisho) na kisha kumchoma kisu machoni, tumboni na mabegani ili kujipatia vitu hivyo.
Wakili Gavyole, alidai kuwa upelelezi wa mashitaka hayo haujakamilika na kuomba mahakama ipange tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.
Mshitakiwa huyo pia alikana mashitaka hayo na Hakimu Haule aliiambia mahakama kuwa kwa mujibu wa Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, kifungu cha 148 kifungu kidogo cha 5 (a) mashitaka hayo hayana dhamana, hivyo mshitakiwa alitakiwa kurudi rumande na kuahirisha kesi hiyo hadi Novemba 2, mwaka huu itakapotajwa.

WANAOANZA DARASA LA KWANZA MWAKA 2017 KWENDA NA MCHE MMOJA WA MTI

Serikali imeagiza halmashauri zote nchini kuhakikisha kuanzia mwakani kila mwanafunzi anayeanza darasa la kwanza katika shule za serikali na binafsi afike shuleni kwake na mche mmoja wa mti.
Aidha, imebainisha kuwa kwa upande wa shule za sekondari kila mwanafunzi atapaswa kwenda na miche mitatu wakati wa kuanza masomo.
Hayo yalisemwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, January Makamba wakati akishiriki katika upandaji miti na wanafunzi katika Shule ya Msingi Mlandege iliyopo katika Kata ya Kwakilosa, Manispaa ya Iringa ambako aliongozana na viongozi mbalimbali wa mkoa huo wa Iringa jana.
Alisema agizo hilo ni kwa mujibu wa Ofisi ya Makamu wa Rais, Mazingira na linapaswa kutekelezwa mara moja; na kwamba maelekezo ya agizo hilo yatapelekwa Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa. “...Kuanzia mwakani kila mwanafunzi wa darasa la kwanza akiripoti atatakiwa kuja na mche wa mti na ataupanda na kuutunza kwa miaka yote saba na hatapewa cheti cha kumaliza darasa la saba kabla hajaonyesha mti wake,” alisisitiza January.
Alisema katika shule zenye maeneo madogo, miti hiyo itapandwa kwenye maeneo yatakayoelekezwa na Serikali za Vijiji na Mitaa.
“Kuanzia Novemba 5 hadi 6 tumewaita wakuu wa wilaya, wakurugenzi na wenyeviti na mameya wote Arusha, kwa ajili ya kuwapa mafunzo na maelekezo mahsusi yanayohusu suala la hifadhi ya mazingira, ikiwemo upandaji miti na utunzaji wa vyanzo vya maji,” alisema.
Waziri huyo alisema lengo la kushiriki katika upandaji miti pamoja na wanafunzi hao ni kutuma ujumbe mahsusi na wa uhakika kwamba uhifadhi, usimamizi na utunzaji wa mazingira ni jukumu la msingi kwa manufaa ya kizazi kinachokuja na ndio sababu hasa ya kushiriki na wanafunzi ili waweze kujifunza na kuelewa.